Yacouba Songne matumaini kibao Bongo

BAADA ya kukaa jukwaani katika mchezo uliopita dhidi ya Simba, nyota wa Tabora United, Yacouba Songne amesema alikuwa na shauku kubwa ya kucheza tena Ligi Kuu Bara, lakini sasa anahamishia nguvu kwa Namungo kuhakikisha anaisaidia timu yake kuanza vizuri msimu huu.

Tabora United ambayo msimu huu ni wa pili Ligi Kuu Bara, ilianza ligi kwa kufungwa mabao 3-0 ugenini na Simba huku ikiwakosa mastaa wake wengi wa kimataifa kutokana na kutokamilisha taratibu za usajili ambazo hivi sasa inaelezwa kila kitu kipo sawa.

Wachezaji wa kimataifa waliopo Tabora United walioshindwa kucheza kutokana na masuala ya usajili baadhi yao ni Heritier Makambo, Yacouba, Morice Chukwu na Faria Jobel Ondongo ambao ni wazoefu na Ligi Kuu Bara kutokana na kuzitumikia timu tofauti ikiwemo Yanga na Singida Black Stars.

Akizungumza na Mwanaspoti, Yacouba alisema aliumia kukosa mechi dhidi ya Simba kwani alikuwa jukwaani akishuhudia kikosi chake kikipoteza mchezo wa kwanza.

Alisema hayo tayari yamepita, lakini yameongeza morali zaidi katika mchezo ujao kwani watakuwa wamekamilika.

“Namungo wajipange tunakwenda kwa morali kubwa ya kutaka kuwaonyesha ukubwa wa kikosi chetu sasa, kwani tuna wachezaji wazuri ambao hawakucheza mchezo wa kwanza. Msimu huu tunataka kuipa nguvu timu kufanya vizuri zaidi. Tutakuwa tumekamilika,” alisema mshambuliaji huyo raia wa Burkina Faso aliyewahi kuitumikia Yanga na Ihefu SC.

Tabora United msimu uliopita ulikuwa wa kwanza kucheza Ligi Kuu, hata hivyo haikumaliza vizuri baada ya kudondokea katika mchujo (play off) na kubahatika kuifunga Biashara United ikafanikiwa kubaki.

Msimu huu katika mchezo wa pili wa ligi itakutana na Namungo, Jumapili ijayo, Agosti 25 kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.

Related Posts