Dar es Salaam. Hatimaye Kampuni ya State Oil Tanzania Limited imekubali yaishe mahakamani kuhusu malipo ya mkopo wa Dola 18.64 milioni za Marekani (Sh47 bilioni) za Benki za Equity, Equity Bank Tanzania Limited (EBT) na Equity Bank Kenya (EBK) uliokuwa unabishaniwa.
Hii inatokana na uamuzi wa kampuni hiyo kuiondoa mahakamani kesi iliyokuwa imeifungua ikipinga malipo ya mkopo huo kwa madai haikuwahi kukopeshwa na benki hizo, badala yake imekubali kuzilipa benki hizo Dola 13.5 milioni za Marekani (Sh35 bilioni).
Kampuni hiyo awali ilifungua kesi Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Dar es Salaam dhidi ya benki hizo ikipinga kudaiwa fedha yoyote na benki hizo.
Hata hivyo, benki hizo pia zilifungua madai kinzani zikidai kuwa zinaidai kampuni hiyo Dola 26.47 milioni za Marekani likiwa ni deni la mkopo ambao ziliipatia kampuni hiyo Novemba 21, 2018.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake ilikubaliana na madai ya kampuni hiyo na kuipa ushindi ikieleza benki hizo hazikuwahi kuikopesha kiasi hicho cha fedha.
Benki hizo zilikata rufaa Mahakama ya Rufani zikipinga hukumu hiyo ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake ilioutoa Mei 16, 2024 ilibatilisha hukumu hiyo ya Mahakama bila hata kusikiliza hoja za msingi za rufaa ya benki hizo.
Uamuzi huo ulitolewa na jopo la majaji watatu, Rehema Mkuye (Kiongozi wa joo), Abraham Mwampashi na Zainabu Muruke, Alhamisi, baada ya kubaini kasoro katika mwenendo wa kesi hiyo ya msingi.
Kasoro hiyo ilikuwa ni Mahakama Kuu kuendelea kusikiliza na kuamua kesi hiyo bila hati ya madai kufanyiwa marekebisho baada ya wadaiwa katika kesi ya msingi kuongezeka kutoka mmoja na kuwa wawili.
Mahakama hiyo ilisema kasoro hiyo inavunja masharti ya lazima ya amri ya 1 Kanuni ya 10 (4) ya Sheria ya Kanuni za Madai (CPC) na kwamba pia kumeathiri Mwenendo na vilevile hukumu iliyotokana na Mwenendo huo.
Hivyo, Mahakama ya Rufani ilitengua hukumu hiyo na kurejesha kumbukumbu (jalada) za kesi ya kibiashara namba 105 ya mwaka 2020, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara kwa ajili ya kesi kusikilizwa upya baada ya kukidhi matakwa ya Amri ya 1 Kanuni ya 10 (4) ya CPC.
Hata hivyo, badala ya kuendelea na usikilizwaji upya kampuni hiyo imefanya majadiliano na benki hizo na kufikia makubaliano na benki hizo, na sasa imekubali kudaiwa na benki hizo na imekubali kulipa Dola 13.5 milioni za Marekani (Sh35 bilioni)
Makubaliano hayo yamefikiwa na pande zote Agosti 16, 2024, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya hatua ya usuluhishi mbele ya Naibu Msajili Joyce Minde.
Majadiliano hayo baina ya wadaiwa (pande zote mbili) yalifanyika mbele ya wakili wa kampuni hiyo, Frank Mwalongo na mawakili wa benki hizo, Mpaya Kamara na Tumaini Michael na wawakilishi wa kampuni hiyo, Nilesh Kumar Suchak na Anil Nilesh Suchak.
Makubaliano hayo yamesajiliwa na kuwa amri ya Mahakama hiyo ambayo inapaswa kutekelewa kulingana na makubaliano hayo.
Kwa mujibu wa amri hiyo ya Mahakama ya Agosti 16, 2024, inayotokana na makubaliano hayo, State Oil imekubali kuzilipa benki hizo kiasi hicho cha fedha, Dola za Marekani 13.5 milioni kwa awamu mbili.
Katika awamu ya kwanza imekubali kulipa Dola 6.75 milioni za Marekani zitalipwa Juni 30, 2025 au kabla ya tarehe hiyo na awali ya pili imekubali pia kulipa kiasi kama hicho Dola 6.75 mpaka kufikia au kabla ya Juni 30, 2026.
“Mdaiwa hata hivyo atakuwa huru kulipa kiasi chote kilichokubaliwa katika makubaliano hayo au sehemu yake wakati wowote hata mapema kabla ya muda uliopangwa kama ulivyoelezwa hapo juu,” inaeleza amri hiyo ya mahakama.
Vilevile Mahakama hiyo katika amri yake hiyo imeamuru dhamana zilizokuwa zimewekwa na wadaiwa wa mkopo huo (state oil na wadhamini wake) zitaachiliwa na benki hizo baada ya kampuni hiyo kukamilisha malipo yote.
Pia, Mahakama hiyo imebainisha isipokuwa kama kutakuwa na ukiukwaji wa makubaliano hayo, malipo hayo yaliyobainishwa katika awamu hizo mbili hayatakuwa na riba au adhabu ndani ya muda wa malipo ulioanishwa.
Hata hivyo, imesema kama kutakuwa na ukiukwaji wa makubaliano hayo wa namna yoyote katika ulipaji katika awamu hizo basi malipo hayo yatakuwa na riba na benki hizo zitakuwa huru kuchukua hatua zozote.
Hatua hizo ni pamoja na kupiga mnada mali zilizowekwa kama dhamana kufikia deni hilo au kuomba utekelezaji wa makubaliano hayo kwa namna ileile kama amri ya mahakama.
Awali, State Oil ilifungua kesi hiyo dhidi ya EBT, kama wakala wa EBK, kufuatia mgogoro wa malipo ya mkopo wa Dola za 18,640,000 Marekani ambazo EBK inaidai State Oil.
Makubaliano hayo ni ushindi kwa benki hizo na hii inakuwa ni kesi ya pili kwa benki hizo kushinda miongoni mwa kesi kadhaa zilizofunguliwa na kampuni mbalimbali zikipinga kulipa mikopo kutoka katika benki hizo.
Mwaka 2018, State Oil ilichukua mkopo wa Dola 18.64 milioni za Marekani kutoka kwa mkopeshaji wa nje, kampuni ya Lamar Commodity Trading DMMC of Dubai kwa udhamini wa Equity Bank Kenya.
Ili kupata udhamini huo, State Oil pia iliweka dhamana zake kwa Equity Bank Kenya, chini ya usimamizi wa Equity Tanzania.
Hata hivyo, State Oil ama ilishindwa au ilipuuza kulipa mkopo huo kwa Kampuni ya Lamar hivyo mdhamini wake Equity Bank Kenya ikalazimika kuulipa, na yenyewe ndio ikabaki inaidai kampuni hiyo.
Baada ya muda iliopewa kulipa deni hilo kuisha bila kulipa Equity Bank Tanzania ilipoidai State Oil kwa niaba ya Equity Bank Kenya kama wakala wake aliyepewa dhamana hiyo, ndipo State Oil ilipokimbilia mahakamani.
Katika kesi hiyo kampuni hiyo iliiomba Mahakama iiamuru Equity Bank Tanzania iirejeshee hati za mali ilizokuwa imeziweka dhamana, kwa ajili ya kupata udhamini kutoka kwa Equity Bank Kenya, huku ikidai kuwa haidaiwi na benki hizo.
Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo miongoni mwa mashahidi hao walikuwa ni pamoja na mwakilishi wa Kampuni ya Lamar iliyotoa mkopo huo ambayo ilieleza kuwa State Oil ilishindwa kulipa mkopo wake na badala yake mdhamini wake, Equity Bank Kenya ndo akaulipa.
Hata hivyo, mahakama hiyo katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Stephen Magoiga Oktoba Mosi, 2021, alikubaliana na madai ya State Oil, kuwa ilikuwa imeshalipa deni lake lote, hivyo benki hizo hazikuwa na madai dhidi yake.
Hiyo jaji Magoiga aliamuru hati za mali zote zilizokuwa zimewekwa dhamana na State Oil, zinashikiliwa zirejeshwe kwa kampuni hiyo, uamuzi ambao benki hizo hazikukubaliana nao ndipo zikakata rufaa Mahakama ya Rufani.