Uzuri wa Serikali yetu ni kwamba hakuna swali linalokosa majibu. Kunaweza kukosekana ufumbuzi wa matatizo yetu ya miaka mingi, lakini majibu ya malalamiko yote yapo. Kwa mfano majibu ya tatizo la kukosekana kwa kituo cha afya lililodumu kwa miaka thelathini ni “Mchakato umeshakamilika na mkandarasi ameshatafutwa, tunasubiri mwaka wa fedha ili tuidhinishe mradi”.
Lakini cha ajabu fedha za mradi zinaweza kuidhinishwa na bado shida ikaendelea. Kwa tatizo linaloendelea kwa miaka thelathini, nina wasiwasi fedha zinaweza kutolewa zaidi ya mara mbili. Nikaingiwa na shaka zaidi hivi karibuni nilipomsikia mkuu mmoja aliyepokea taarifa kwamba fedha za mradi hazijulikani zilipo, akaonya kwamba kama hajaletewa taarifa inayoeleweka atafunga safari kuelekea eneo husika na kuchukua hatua kali.
Hata siku moja mradi hautakiwi kuwa na dosari kwenye eneo lolote. Hiyo ndiyo sababu ya fedha za mradi kupitia hatua za uhakika kabla ya kufikia ukamilisho wake. Ni lazima kuwepo na bajeti ya mradi inayopangwa na kuidhinishwa na wadau au mamlaka husika. Mara zote mamlaka hufanya hayo baada ya kujiridhisha na viwango na muda ulioombwa na mkandarasi. Baada ya bajeti kupitishwa, fedha zinakuwa tayari kwa ajili ya matumizi.
Fedha hizi ni lazima ziwekwe kwenye akaunti maalumu ya mradi inayotumika kulipia gharama zake kulingana na mpango wa bajeti. Hakutegemewi kutokea upungufu wa vifaa wala mishahara ya wafanyakazi. Ndiyo maana kuna nyongeza ya fedha ya dharura juu ya bajeti ya mradi. Ikiwa mradi umepangwa kutekelezwa kwa hatua, fedha zinaweza kutolewa kulingana na kukamilika kwa kila hatua. Hii ni kuhakikisha kuwa mradi haupatwi na kwikwi.
Tatizo linaanza pale baadhi ya makandarasi wanapoingia “chocho” kwenye malighafi zisizo rasmi (kama za wizi au ubora duni) wakilenga kutumia kiasi kidogo zaidi cha fedha walizoidhinishiwa. Na wakati mwingine wasimamizi na wadau wengine wa mradi huweza kujiingiza kwenye kamati za manunuzi wapate kupiga hodi kwenye maduka ya “wajomba” ili nao wapate chochote kitu.
Tabia hii imekuwa mwiba mchungu kwa maendeleo yetu. Hakuna mdau yeyote kuanzia juu mpaka chini asiyejua umuhimu wa usimamizi na uwazi wa fedha katika kuhakikisha mradi unakamilika kwa ufanisi na ndani ya bajeti, lakini baadhi yao wanapofikiria mafao ya binafsi wanapagawa. Ndipo mshika dau anapofikiri kupata kiasi kikubwa kuliko atakachomlipa mkandarasi, na mkandarasi anapofikiria kununua malighafi duni.
Haituingii akilini tunapoambiwa “Sh20 milioni za ujenzi hazijulikani zilipo” wakati aliyezipokea anajulikana. Aliyesaini kupokea fungu ni mtu mwenye dhamana kwenye jambo hilo.
Makabidhiano yalifanyika ofisini, siyo chini ya nguzo wala kwa kupitia simu kama wafanyavyo wakopeshaji wa fasta fasta mitandaoni. Hapa ndipo hasira za wanyonge zinapowaka kwa kudhani “wote ni walewale”: Mbuzi wa Bwana Heri amekula shamba la Bwana Heri…
Tena kwa mfumo uliopo, kila hatua inakuwa bayana kwenye maandishi. Hata kwa akili zetu ndogo tunaweza kutambua kuwa mfadhili alibaki na vielelezo baada ya kukabidhi fedha hizo. Ni lazima kuna maandishi pamoja na saini katika kila hatua ya makabidhiano. Hivyo yeyote aliyehusika na fungu la mradi iwapo alilikabidhi salama, hana haja ya kutafuna maneno ila kuonesha vielelezo.
Vilevile haina haja ya Mkuu wa Wilaya kuchoma mafuta kwenda kuzitafuta fedha hizo kwa tochi.
Iwapo mradi unachelewa au umesimama, taratibu za kimamlaka zinapaswa kutumika, kwani ni za haraka na uhakika. Kama kuna mtu aliyetoroka nazo basi ngazi za kiserikali zitumike kumsaka, kumkamata, kumhoji na hata kumchukulia hatua hata kama bado hajazila. Haina haja ya kiongozi wa makao makuu kuacha kazi na kutumia gharama nyingine wakati Serikali ipo kila mtaa.
Kwa vyovyote mtendaji asiye mwadilifu atakapolenga kujipatia faida haramu, atazunguka huku na huko kutafuta bei za mteremko. Leo atakwenda China na kesho Dubai, hivyo kukiuka mkataba wa pande zote mbili. Ndiyo maana nikasema akikamatwa aadhibiwe kwa kuchelewesha hatua za mradi. Izingatiwe kuwa ni muhimu kwa mteja na mkandarasi kuelewa vizuri masharti ya mkataba kabla ya kuanza kazi ili kuepuka migogoro ya baadaye.
Wakati mhujumu huyo akihangaika, hakumbuki kwamba anatumia fedha za mradi. Atakaposhtuka atagundua kuwa ameshapiga robo nzima ya fedha hizo. Akili ya kijinga itamshauri anunue bidhaa huko Dubai na kuja kuziuza nyumbani. Faida atakayopata azibe pengo alilosababisha, na ya ziada aiingize kwenye mzunguko wake. Hajui kwamba “jino la bandia halizibi pengo orijino”.
Ataanza kupiga simu kwa ndugu zake wafanyabiashara kuwauliza ni bidhaa gani inayokwenda “moto chini” huko mtaani. Hata mimi ningeulizwa swali hilo ningejibu haraka “laptop na simu” nikiwaza kufunguliwa dunia ya biashara na kupata faida. Lakini kumbe soko la hapa nyumbani haliko kivile; kiwanda kinamkopesha muuzaji wa jumla anayemkopesha muuzaji rejareja anayemkopesha mlaji. Malipo huwa “dusuro-dusuro”, tena wakati mwingine huwa maneno badala ya fedha.
Humu ndimo fedha za miradi yetu zinamotumbukia. Sasa ili kuondoa dhana ya Shamba la Bwana Heri kwa wananchi, tuanze na Serikali kuwaadabisha wadau wanaozungusha fedha za miradi yetu.