Jumapili ya Desemba 22, mwaka huu, Sudan Kusini inatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu wa kwanza tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake mwaka 2011.
Uchaguzi huu ulipaswa kufanyika mapema mwaka 2015, lakini kutokana na jaribio la mapinduzi na machafuko yaliyofuata, uchaguzi huo uliahirishwa.
Hadi mwaka 2015, Katiba ya mpito ya mwaka 2011 ya nchi hiyo ilihitaji uchaguzi kufanyika kabla ya Julai 9, 2015, siku ambayo kipindi cha kwanza cha urais baada ya uhuru kilikuwa kinamalizika.
Bunge la nchi hiyo lilipiga kura Aprili 2015 kurekebisha katiba ya mpito ili kuongeza muda wa urais na bunge hadi Julai 9, 2018.
Baadaye, uchaguzi huo uliahirishwa tena hadi mwaka 2021 kufuatia makubaliano ya amani ya kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe. Mwaka 2022, serikali ya mpito na upinzani walikubaliana kuusogeza hadi mwishoni mwa mwaka 2024.
Hivi karibuni Rais Kiir alifanya mazungumzo na viongozi wa kisiasa nchini humo kujadili uchaguzi ambao umecheleweshwa kwa muda mrefu.
Nchi hiyo changa zaidi duniani bado haijashiriki mchakato wa uchaguzi wa kidemokrasia, ikiwa ni takribani miaka 13 tangu kile kinachoitwa uhuru wake uliopiganiwa kwa bidii kutoka kwa Sudan, hali ambayo imekuwa ikiwakatisha tamaa watu wake na jumuiya ya kimataifa.
Katika taarifa ambayo imechapishwa katika ukurasa wa Facebook wa ofisi hiyo ya Rais inaeleza, “Rais pamoja na viongozi wa vyama vikuu vya kisiasa, wameazimia kutafuta ushauri wa kitaalamu kutoka taasisi za uchaguzi kuhusu uwezekano wa kufanya uchaguzi ujao.”
Mkutano huo ulitathmini hali ya kuyumba kwa utekelezaji wa makubaliano ya amani ya mwaka 2018 ili kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano kati ya vikosi vinavyomtii Kiir na mpinzani wake mkuu ambaye sasa ni Naibu Rais, Riek Machar.
Waziri mwenye dhamana na masuala ya Baraza la Mawaziri la taifa hilo, Martin Elia Lomuro alisema mapitio hayo “yalilenga kutoa ratiba halisi kwa viongozi wa kisiasa kukubaliana kuhusu uchaguzi”.
Lengo la makubaliano ya amani ya Sudan Kusini Mkataba wa 2018 ulifungua njia kwa serikali ya mgawanyo wa madaraka na uliweka ramani ya muda wa mpito wa kisiasa na hatimaye kuandaliwa uchaguzi.
Historia ya uhuru Sudan Kusini
Sudan Kusini ni nchi changa zaidi duniani iliyopata uhuru wake rasmi kutoka Sudan Julai 9, 2011 baada ya miongo kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Vita hivi vilikuwa kati ya Serikali ya Sudan iliyoongozwa na Waarabu wa Kaskazini dhidi ya wapiganaji wa Sudan Kusini ambao wengi wao ni Waafrika weusi.
Uhuru huu ulipatikana baada ya kura ya maoni ya mwaka 2011 ambapo wananchi wengi wa Sudan Kusini waliunga mkono kujitenga na Sudan.
Baada ya kupata uhuru, Salva Kiir alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa Sudan Kusini na Riek Machar akawa Makamu wa Rais.
Hata hivyo, nchi hiyo imekumbwa na changamoto nyingi za kisiasa na kiusalama tangu wakati huo, ikiwamo vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza mwishoni mwa mwaka 2013.
Vita hivi vilitokana na mzozo wa madaraka kati ya Rais Salva Kiir na Makamu wake, Riek Machar ambao ulisababisha mgawanyiko mkubwa wa kikabila kati ya Dinka na Nuer, makabila mawili makubwa nchini humo.
Rais wa Sudan Kusini huchaguliwa kwa mfumo wa duru mbili, ambapo iwapo hakuna mgombea anayepata zaidi ya nusu ya kura halali zilizopigwa, duru ya pili hufanyika ndani ya siku 60 kati ya wagombea wawili waliopata kura nyingi zaidi. Ili kustahili kugombea urais, mgombea lazima awe raia wa Sudan Kusini kwa kuzaliwa, awe na umri wa miaka 40 au zaidi, awe na akili timamu na asiwe na rekodi ya makosa ya jinai yanayohusiana na udanganyifu au utovu wa maadili.
Mgombea pia lazima apate saini za wapigakura 10,000 kutoka angalau majimbo saba, huku kila jimbo likiwa na angalau wapigakura 200.
Usimamizi na matokeo tarajiwa
Uchaguzi huu utasimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa ya Sudan Kusini kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kitaifa na kimataifa. Changamoto kubwa inatarajiwa kuwa kuhakikisha usalama katika maeneo yenye machafuko ya mara kwa mara.
Matokeo ya uchaguzi huu yanatarajiwa kuleta sura mpya katika uongozi wa Sudan Kusini, lakini pia kuna hofu ya machafuko endapo matokeo yatapingwa. Hata hivyo, makubaliano ya amani na usimamizi wa haki unatarajiwa kuchangia uchaguzi wa amani na wa haki.
Hali ya siasa Sudan Kusini
Sudan Kusini imeendelea kukumbwa na changamoto za kisiasa na kiusalama, ikiwamo migogoro ya kikabila na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya zaidi ya watu 400,000.
Serikali ya mpito ya mgawanyo wa madaraka, iliyoongozwa na Rais Salva Kiir na Makamu wa Rais, Riek Machar imekuwa ikijaribu kurejesha amani na utulivu nchini humo.
Hata hivyo, utekelezaji wa makubaliano ya amani ya mwaka 2018 umekuwa wa mwendo wa taratibu sana, huku mambo muhimu kama kutungwa kwa katiba ya kitaifa na kuunganishwa kwa vikosi hasimu vya kijeshi bado hayajakamilika.
Sudan Kusini pia inakumbwa na changamoto za kiuchumi, licha ya kuwa na utajiri wa mafuta. Uchumi wa nchi hiyo umeathirika kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe, ufisadi na majanga ya asili kama mafuriko.
Shirika la kimataifa la Save the Children lilionya mwezi uliopita kuwa sehemu nyingi za nchi hiyo ziko hatarini kukumbwa na baa la njaa kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua za msimu.
Hatima ya Sudan Kusini kisiasa
Uchaguzi huu unatarajiwa kuwa jaribio kubwa na muhimu kwa hatima ya Sudan Kusini kisiasa.
Iwapo uchaguzi huo utaendeshwa kwa haki, uwazi na kwa amani, kuna uwezekano mkubwa wa kufungua ukurasa mpya wa matumaini kwa taifa hilo.
Uchaguzi wa kidemokrasia ni fursa muhimu kwa Sudan Kusini kuonyesha uwezo wake wa kujenga taasisi thabiti za kisiasa na kuleta utulivu wa kudumu baada ya miaka mingi ya mzozo na mgawanyiko.
Hata hivyo, kufanikisha uchaguzi huo kutategemea kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa makubaliano ya amani ya mwaka 2018, ambayo yalikuwa msingi wa kuleta utulivu nchini humo baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha maafa makubwa. Utekelezaji wa makubaliano haya unajumuisha kuunda katiba ya kudumu na kuunganisha vikosi vya kijeshi vilivyokuwa hasimu. Bila hatua hizi muhimu kutekelezwa kikamilifu, uchaguzi huo unaweza kukabiliwa na changamoto kubwa ambazo zitavuruga mchakato mzima.
Hali ya kisiasa na kiusalama nchini humo pia itakuwa na athari kubwa katika kufanikisha uchaguzi huu. Matatizo ya kikabila, ambayo yamekuwa yakichochea ghasia za mara kwa mara, ni changamoto inayohitaji kushughulikiwa kwa umakini.
Viongozi wa kisiasa wanapaswa kujenga uaminifu na ushirikiano kati ya makabila tofauti ili kuhakikisha kuwa uchaguzi hauchochei tena mgawanyiko bali unaleta umoja na mshikamano wa kitaifa.
Sudan Kusini ina nafasi ya kipekee ya kuimarisha demokrasia yake na kuleta utulivu wa kudumu ikiwa viongozi wake wataonesha nia ya dhati ya kushirikiana kwa pamoja na kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa uwazi, haki na usawa.
Hii itahitaji msaada kutoka kwa jumuiya ya kimataifa na taasisi za uchaguzi ili kutoa ushauri na msaada wa kiufundi kuhakikisha mchakato mzima unafanyika kwa ufanisi.
Pamoja na hayo, changamoto zinazokabili nchi hiyo, kama vile kukosekana kwa katiba ya kudumu, migogoro ya kikabila na hali ya usalama, zitalazimika kuzingatiwa kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha mustakabali mzuri wa Sudan Kusini.