TMA: Wanaoishi mikoa hii wajiandae na hali mbaya ya hewa

Dar es Salaam. Wananchi wanaoishi katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Lindi, Mtwara, Pemba na Unguja wametakiwa kuchukua tahadhari kutokana na uwepo wa hali mbaya ya hewa kwa siku tano.

Taarifa ya uwepo wa hali mbaya ya hewa kwa siku tano, imetolewa jana Jumanne Agosti 20, 2024 na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

“Angalizo la upepo mkali unaofikia kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofikia mita mbili limetolewa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara na  ikijumuisha visiwa vya Mafia, Unguja na Pemba,” imeeleza taarifa hiyo.

Athari zinazotarajiwa kutokana na hali hiyo mbaya ni kuathirika kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi, uvuvi na usafirishaji baharini.

Pia, leo Jumatano, Agosti 21, 2024 TMA imetoa angalizo la upepo mkali wa kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofikia mita mbili.

Baadhi ya maeneo ya ukanda wote wa Pwani ya bahari ya Hindi mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara na  ikijumuisha visiwa vya Mafia, Unguja na Pemba kiwango cha athari kilichotabiriwa ni wastani.

“Agosti 22, angalizo la mawimbi makubwa yanayofikia mita mbili limetolewa kwa baadhi ya maeneo ya ukanda wote wa Pwani ya bahari ya Hindi ikiwamo mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara, ikijumuisha visiwa vya Mafia, Unguja na Pemba kiwango cha athari kinachoweza kutokea ni wastani,’’ imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Hata hivyo, hakuna hali mbaya iliyotabiriwa kwa siku ya Agosti 23 na 24, 2024.

Related Posts