Mafuriko yachelewesha kufungua shule Kenya

Nairobi, Kenya/AFP.  Kenya imesema leo Jumatatu kuwa imeahirisha kufunguliwa kwa shule kwa wiki moja kutokana na “mvua kubwa inayoendelea” ambayo imesababisha mafuriko katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Awali shule zilipangwa kufunguliwa leo Jumatatu Aprili 29, 2024 baada ya likizo za katikati ya muhula, lakini mvua kubwa za Masika zimeathiri miundombinu mingi ya elimu na kusababisha wizara ya elimu kuchelewesha kuanza masomo kwa juma moja.

“Athari mbaya za mvua katika baadhi ya shule ni kubwa sana na hivyo halitakuwa jambo la busara kuhatarisha maisha ya wanafunzi na wafanyikazi bila kuhakikisha usalama wa kutosha,” amesema Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu amesema.

“Kulingana na tathmini hiyo, Wizara ya Elimu imeazimia kuahirisha kufunguliwa kwa shule zote za msingi na sekondari kwa wiki moja, hadi Jumatatu, Mei 6, 2024,” almesema katika taarifa yake.

Watu 76 wamepoteza maisha nchini Kenya tangu Machi, huku mvua kubwa kuliko kawaida ikinyesha Afrika Mashariki, ikichangiwa na mufumo wa hali ya hewa wa El Nino.

Mafuriko makubwa yamesababisha barabara na kujaa maji, kukatika na kusababisha zaidi ya watu 130,000 kuyahama makazi yao katika kaya 24,000; wengi wao katika mji mkuu wa Nairobi, kulingana na takwimu za Serikali zilizotolewa Jumamosi.

Shule 64 za umma jijini Nairobi, karibu theluthi moja ya idadi yote, zimeathiriwa pakubwa na mafuriko, Belio Kipsang, katibu mkuu wa elimu, alisema Ijumaa.

Mashariki mwa Kenya, mashua iliyokuwa imebeba “idadi kubwa ya watu” ilizama Jumapili katika kaunti ya Tana River iliyofurika, Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya limesema na kuongeza kuwa wengine 23 wameokolewa.

Kanda za video zilizosambazwa mtandaoni na kutangazwa kwenye runinga zilionyesha mashua iliyojaa watu ikizama, watu wakipiga kelele huku wananchi wengine pembeni wakitazama kwa hofu.

Mvua hizo pia zimesababisha uharibifu katika nchi jirani ya Tanzania, ambapo takriban watu 155 wamepoteza maisha katika mafuriko na maporomoko ya ardhi.

Nchini Burundi,  takriban watu 96,000 wameyakimbia makazi yao kutokana na miezi kadhaa ya mvua zinazoendelea kunyesha, Umoja wa Mataifa na Serikali zilisema mwezi huu.

Uganda pia imekumbwa na dhoruba kali ambayo imesababisha kingo za mito kupasuka, huku vifo viwili vikithibitishwa na mamia ya wanakijiji kuyahama makazi yao.

Mwishoni mwa mwaka jana, zaidi ya watu 300 walikufa kutokana na mvua na mafuriko nchini Kenya, Somalia na Ethiopia, wakati eneo hilo lilipokuwa likijaribu kujikwamua kutokana na ukame mbaya zaidi katika miongo minne iliyoacha mamilioni ya watu wakiwa na njaa.

El Nino ni mfumo wa hali ya hewa unaotokea kiasili unaohusishwa na ongezeko la joto duniani kote, na kusababisha ukame katika baadhi ya maeneo ya dunia na mvua kubwa kwingineko.

Related Posts