BAADA ya Yanga kusota kwa msimu mmoja kwenye eneo la ushambuliaji ni kama tumaini jipya limerudi ndani ya viunga vya Jangwani.
Msimu wa 2022/23 Yanga ilimuuza mshambuliaji wake raia wa DR Congo, Fiston Mayele kwenda Pyramids FC ya Misri ambako amemaliza msimu na mabao 17 na asisti tano, akishika nafasi ya pili nyuma ya mfungaji bora, Wessam Abou Ali wa Al Ahly aliyefunga mabao 18 na asisti nne.
Mayele alisajiliwa Yanga msimu wa 2021 akiitumikia kwa misimu miwili na tangu atambulishwe Jangwani na alikuwa straika tegemeo akiwaacha washambuliaji wengine Heritier Makambo na Yacouba Sogne aliyekuwa majeraha.
Msimu wake wa kwanza aliwezesha Yanga kuchukua ubingwa wa ligi kwa kufunga mabao 16 akiibuka mfungaji namba mbili nyuma ya George Mpole aliyefunga mabao 17.
Hakuishia hapo, msimu uliofuata akashinda tuzo ya Kiatu cha Dhahabu cha mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akiweka nyavuni mabao 17 akiwa sawa na aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Simba, Said Ntibazonkiza ‘Saido’.
Baada ya kuondoka kwa Mayele, matumaini ya mashabiki wengi yalikuwa kwa Kennedy Musonda na Clement Mzize ambaye alipandishwa kutoka timu ya vijana.
Matarajio hayakwenda kama ilivyotarajiwa badala yake baadhi ya mashabiki wa timu hiyo wakaanza kumisi yale mabao ya ‘mzee wa kutetema’.
Na tangu Mayele aondoke Yanga timu hiyo imekuwa ikisuasua katika eneo la mshambuliaji Namba 9.
Kutokana na kutokuwa na mshambuliaji tegemeo, viongozi wa Yanga wakaingia tena sokoni kusajili washambuliaji wapya ili kuwapa ushindani Mzize na Musonda.
Ndani ya msimu mmoja timu hiyo ilisajili Hafiz Konkoni akitokea Bechem United ya Ghana na dirisha dogo la msimu uliopita ikamuongeza Joseph Guede akitokea Tuzlaspor ya nchini Uturuki.
Lakini kama ilivyokuwa kwa Konkoni, hamna aliyeonekana kukidhi matakwa ya kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi ambaye mara nyingi anapenda kuwatumia viungo watatu Stephane Aziz KI, Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua.
Konkoni alifunga bao moja huku Guede aliyeingia dirisha dogo akiweka nyavuni mabao sita Ligi Kuu na kuiwezesha Yanga kutinga robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kushinda mechi yao ya Kundi D kwa mabao 4-0 dhidi ya CR Belouzdad ya Algeria.
Hata hivyo, baada ya washambuliaji kusuasua kocha wa Yanga, Gamondi alikuwa akiwatumia zaidi viungo watatu ambao licha ya kuanzisha mashambulizi wamekuwa wakitupia mabao nyavuni jambo lililomfanya Aziz KI kushinda tuzo ya Kiatu cha Dhahabu ya mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara 2023-24 akifunga mabao 21, mbele ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam aliyefunga 19.
Mshambuliaji huyo alisajiliwa Yanga akitokea Azam FC ambako alidumu kwa msimu minne tangu ajiunge nayo mwaka 2020 kutoka Highlanders ya Zimbabwe.
Hata hivyo, ndani ya misimu hiyo amefunga mabao 34 tu kwenye ligi wastani wa mabao 8 kwa kila msimu ambao amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara yanayomuweka nje ya uwanja.
Ingawa bado ni mapema kuongelea kiwango cha mshambuliaji mpya wa Yanga, Dube, lakini kuna dalili za kuwa mrithi wa Mayele aliyejizoelea ufalme wake pale Jangwani.
Yanga ilicheza mechi nne za kirafiki kimataifa dhidi ya Augsburg inayoshiriki Ligi ya Ujerumani ambayo Wananchi walilala 2-1, kisha ikashinda 1-0 dhidi ya TS Galaxy ya Afrika Kusini, Dube akiweka bao la ushindi, halafu Wananchi wakaichakaza Kaizer Chiefs mabao 4-0 na kutwaa Kombe la Toyota la michuano ya kirafiki, Dube akifunga tena kabla ya kuilaza Red Arrows ya Zambia 2-1 kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi.
Katika mechi za Ngao ya Jamii za ufunguzi wa msimu mpya wa 2024-25, Yanga ilicheza mechi ya nusu fainali ikiifunga Simba 1-0 kwa bao la Maxi Nzengeli na kwenda fainali ambako Yanga iliichakaza Azam kwa mabao 4-1, huku Dube akiwatungua waajiri wake wa zamani katika ushindi huo, likiwa ni bao lake la tatu katika mechi sita tangu atue Jangwani.
Kisha Yanga ikacheza mechi ya awali ya kuwania kufuzu kuingia hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa ikaichakaza Vital’O ya Burundi mabao 4-0 huku Dube akifunga bao lake la nne katika mechi 7 za kuwatumikia Wananchi.
Kama atakuwa na muendelezo wa kufunga basi anaweza kuwa mbadala kwa Mayele kwenye eneo la ushambuliaji ambalo msimu uliopita likisuasua.
Tayari Dube ameonyesha makali katika mechi hizo chache alizocheza akiwa na jezi za njano na kijani, lakini bado Jean Baleke ambaye hajapata muda mwingi wa kuonekana uwanjani tangu aliposajiliwa na timu ya Wananchi baada ya kuwa amewatumikia watani wao, Simba.
Baleke, katika mechi yake ya kwanza tu dhidi ya Augsburg aliweka chuma na kukumbushia makali yake aliyoonyesha wakati akiwa na Wekundu wa Msimbazi.
Kwa kuwa msimu ndio kwanza umeanza, Baleke anaweza kupindua meza kwa Dube kutokana na namna atakavyopambana uwanjani, mapambano ambayo hakika yatakuwa na manufaa kwa klabu yao.
Alikopita: The Highlanders, SuperSports Utd, Black Leopards, Azam FC