Moshi. Ama kweli penye nia pana njia, hii ni baada ya raia wa Nigeria, Mike Nwankoko kupigania haki yake kwa siku 3,842 sawa na miaka 10 na miezi sita, akiwa katika magereza ya Tanzania na hatimaye ameachiwa huru na mahakama.
Februari 12, 2021, Jaji Mohamed Gwae wa Mahakama Kuu Moshi alimuhukumu Nwankoko kifungo cha maisha jela kwa kusafirisha dawa za kulevya na kumwachia huru mpenzi wake Mtanzania, Mastura Makongoro waliyekuwa wameshitakiwa naye.
Upande wa mashitaka katika shauri hilo ulikuwa unadai Februari 12, 2014 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), washitakiwa walipatikana wakisafirisha gramu 5,126 za dawa za kulevya aina ya Heroin kwenda Freetown, Sierra Leone.
Hata hivyo, wakati Nwankoko akikata rufaa kupinga kutiwa kwake hatiani na adhabu ya kifungo cha maisha jela, Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) kupitia Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS) Kilimanjaro, nayo ilikata rufaa kupinga kuachiwa kwa Mastura.
Katika hukumu yake, Jaji Gwae alisema anamwachia huru mshitakiwa wa kwanza, Mastura kwa kuwa dawa hizo zilikuwa zimehifadhiwa ndani ya begi asingeweza kuwa na ufahamu kuwa kulikuwa na kitu cha ziada.
Hata hivyo, Agosti 7,2024, Mahakama ya Rufani Tanzania ilitoa amri kwa NPS kutoa tangazo katika vyombo vya habari la kutafutwa kwa Mastura ili ahudhurie mahakamani kusikiliza rufaa hiyo, baada ya kutopatikana ili apokee hati ya wito.
Hukumu ya kumwachia huru Nwankoko ilitolewa Agosti 20, 2024 na jopo la majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Dk Marry Levira, Zephrine Galeba na Mustafa Ismail, baada ya kukubaliana na sababu za rufaa alizokuwa ameziwasilisha.
Katika usikilizwaji wa rufaa hiyo, upande wa Jamhuri ukitetewa na wakili mwandamizi wa Serikali, Rose Sulle akisaidiana na wakili wa Serikali, Isack Mangunu uliunga mkono kikamilifu rufaa ya raia huyo wa Nigeria ili aachiwe.
Historia ya kukamatwa kwake
Katika hukumu yao, jopo la majaji hao watatu lilichambua historia ya mashitaka hayo na kueleza kuwa Nwankoko na Mastura aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo cha Bandari Tanzania, walikuwa ni mtu na mpenzi wake.
Februari 12, 2014, Mastura alikuwa anasafiri kwenda Sierra Leone kupitia KIA ili kuwahi ndege hiyo, Februari 10, Nwankoko akaamua kumsindikiza mpenzi wake na walipanda basi la Dar Express kutoka Dar es Salaam hadi Kilimanjaro.
Waliposhuka njia panda ya KIA, walichukuliwa na dereva taksi aitwaye Rajabu Kwayu aliyekuwa shahidi wa saba wa Jamhuri na akawapeleka hadi nyumba ya kulala wageni wakisubiri siku ya kusafiri ambayo ilikuwa ni Februari 12, 2014.
Siku hiyo saa 6:45 usiku, Mastura akampigia simu Rajabu dereva taksi ili amfuate mahali alipokuwa amelala na kumuwahisha KIA, walikwenda pamoja na Nwankoko hadi uwanja wa ndege na akamuacha Mastura na kurudi na taksi ile hadi hotelini.
Hata hivyo, wakati Mastura akiendelea na itifaki katika uwanja wa KIA kwa ajili ya kusafiri, shahidi wa nane, WP 3052 Janeth ambaye ni Polisi, alimuona Mastura kama mtu mwenye msongo wa mawazo, hivyo akamtilia shaka abiria huyo.
Ili kuondokana na hisia hiyo, WP Janeth alikwenda katika mashine ya ukaguzi wa mizigo (HBS) na kukagua begi la Mastura lakini hakuna kitu kilichoonekana, akamwamuru Mastura atoe vitu vyote lakini begi likawa na uzito wa mashaka.
Uamuzi ulifikiwa wa kulifumua begi hilo ndipo zikagundulika bahasha nne zikiwa zimefichwa na hapo Mastura alianza kububujikwa machozi, na ndani ya bahasha hizo ndio kulikuwa na dawa hizo zilizokuwa na thamani ya Sh400 milioni.
Mastura alivyomtupia mpira Nwankoko
Katika maelezo yake kwa Polisi, alisema awali alikuwa na mabegi yake mwenyewe kabla ya kusafiri kwenda Kilimanjaro ambayo alitoka nayo nyumbani Ilala Jijini Dar es Salaam, na kwenda kwa Nwankoko aliyekuwa amefikia hotelini eneo la Sinza.
Baada ya kufika hotelini, Nwankoko alimshauri ili kuwa na mizigo michache, alimpa begi kubwa na aliondoa vitu vyote vilivyokuwa katika mabegi aliyokuwa nayo na kuviweka katika begi hilo na Nwankoko ndiye aliyemwandalia safari.
Lengo la safari hiyo ilikuwa ni kwenda kumsalimia dada yake Nwankoko anayeishi Freetown kwa kuwa alikuwa amejifungua na ilikuwa waondoke pamoja naye, lakini ghafla alibadili ratiba na kumkatia tiketi yeye tu ya kusafiri kwenda huko.
Mastura anamwita Nwankoko KIA
Kutokana na maelezo hayo, Polisi katika uwanja wa KIA walimruhusu Mastura ampigie simu Nwankoko arudi uwanjani amweleze kuna tatizo limetokea, Nwankoko baada ya kupokea simu ya mpenzi wake, alimwita dereva taksi ili ampeleke tena KIA.
Baada ya kufika KIA, wote wawili yaani Nwankoko na dereva taxi walikamatwa na Polisi na baada ya Polisi kujiridhisha dereva taksi hana uhusiano wowote na dawa za kulevya zilizokuwa zimekamatwa, walimwachia huru arudi nyumbani.
Kwa upande wake, Nwankoko alijitetea kuwa hakuwahi kumwandalia safari Mastura kwenda Freetown kwa kuwa hana ndugu yoyote huko na kwamba, hakumpa mpenzi wake huyo begi lolote Februari 10, 2014 kama Mastura alivyodai.
Alieleza kuwa begi hilo ni mali ya Mastura kwa kuwa ndiye aliyekuja nalo na akasema kuhusika kwake na masuala ya Mastura ni kumsindikiza tu kwenda KIA, lakini hayo ya safari ya Afrika Magharibi hayajui.
Wote wawili walifunguliwa mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya na Februari 12,2021, Jaji Gwae alimtia hatiani Nwankoko na kumuhukumu kifungo cha maisha jela na kumwachia huru Mastura kwa kukosekana kwa ushahidi.
DPP alivyounga mkono rufaa
Nwankoko aliyekuwa akitetewa na wakili Majura Magafu hakuridhishwa na hukumu hiyo na akakata rufaa Mahakama ya Rufani, ilipokuja kusikilizwa Agosti 7,2024, wakili mwandamizi wa Serikali, Sulle aliunga mkono rufaa ya Nwankoko.
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, wakili Sulle alisema msimamo wa Jamhuri ni kuwa wanaunga mkono rufaa ya Nwankoko kwamba mashtaka dhidi yake hayakuthibitishwa na Jamhuri, hivyo hukumu dhidi yake inastahili kubatilishwa.
Yaani kwa mujibu wa majaji hao, wakili huyo wala hakusubiri wakili Magafu awasilishe sababu za rufaa za mteja wake, bali alitoa sababu sita za kwa nini upande wa Jamhuri unaunga mkono rufaa ya raia huyo wa Nigeria.
Moja ni kuwa kwa kuzingatia begi na vilivyokuwamo ndani, hakuna ushahidi unaomuunganisha Nwankoko na dawa za kulevya na pili cheti cha utaifishaji begi lililokutwa na dawa za kulevya lilikuwa kwenye umiliki wa Mastura pekee.
Sababu ya tatu ni kuwa kitendo cha Nwankoko kupigiwa simu na kurudi KIA baada ya Mastura kumwambia amepata matatizo sio tabia ya mtu mwenye hatia na nne Mastura alisema anaenda kwa wifi yake, lakini ilionyesha anafikia hotelini.
Katika sababu ya tano, wakili alisema mahakama ilihamisha mzigo wa kuthibitisha hana kwa mrufani kinyume cha sheria na sita Nwankoko alitiwa hatiani kwa kuegemea ushahidi wa Mastura aliyekuwa mshirika, bila ushahidi wake kuungwa mkono.
Kwa upande wake, wakili Magafu aliunga mkono hoja zote za Jamhuri lakini akatilia mkazo kuwa kulikuwa hakuna shahidi hata mmoja wa Jamhuri, ambao ulimuunganisha Nwankoko na dawa hizo za kulevya au begi.
Wakili Magafu alikosoa uamuzi wa Mahakama Kuu kwa sababu uliegemea ushahidi ambao haukupimwa kikamilifu, kazi ambayo ilikuwa ni ya mahakama na kama ingefanya hivyo, isingemtia Nwankoko hatiani na kumfunga kifungo cha maisha.
Jopo la majaji watatu katika hukumu yao baada ya kusikiliza hoja za mawakili wa pande hizo mbili, walisema hawakuweza kufanyia kazi kikamilifu hoja za wakili Sulle, kwa sababu kuna rufaa dhidi ya Mastura.
Walisema kujadili hoja mojamoja kwa mapana yake, ingeweza kuwa ni kishawishi cha kutafsiri vibaya hukumu yao na kumaanisha kile ambacho hawakukimaanisha, lakini wameridhika kuwa rufaa ya Nwankoko ina mashiko na kesi haikuthibitishwa.
Kwa msingi huo, majaji hao baada ya kuchambua hoja mbalimbali na kurejea misimamo ya mashauri yanayofanana na shauri hilo, wamebatilisha hukumu na adhabu aliyopewa Nwankoko na kuagiza aachiliwe mara moja kutoka gerezani.