SPOTI DOKTA: Ligi imeanza na majeraha ya Kigimbi hayakosi

HIVI sasa Ligi mbalimbali duniani zimeanza kutimua vumbi katika viwanja vya soka ikiwamo hapa nyumbani Ligi Kuu Bara iliyoanza wiki iliyopita.

Vile vile kule nchini Uingereza mwishoni mwa wiki iliyopita ligi kuu ya EPL nayo imeanza kutimua vumbi katika viwanja mbalimbali ikijumuisha timu zilizopanda daraja ikiwamo Leicester City.

Kawaida tumezoea kuona majeraha mbalimbali ambayo huwa hayakosi kutokana na eneo la miguu kutumika wakati wa kucheza soka.

Kuanza kwa ligi hizi ndio pia mwanzo wachezaji kukumbana na majeraha mbalimbali ikiwamo misuli ya paja, goti, kifundo cha mguu na kubanwa au kukamaa kwa misuli.

Ukiacha majeraha hayo ambayo ndio mara kwa mara huwa yanawapata wachezaji lakini pia kuna majeraha ya eneo la nyuma ya ugoko ambayo ndio hujulikana kama kigimbi.

Katika ligi ya NBC ya moja ya wachezaji ambao unaweza kuona vyema eneo kwa mtitio wa misuli ya kigimbi ni kutoka kwa mchezaji wa Yanga Stephan Aziz Kii na wakati kule EPL ni kwa mchezaji wa Man City Jack Grelish.

Kitabibu ni kigimbi ni mkumbatiano wa misuli mikubwa miwili katika eneo la nyuma ya ugoko, hujulikana kitabibu kama gastrocnemius and Soleus.

Kwakuwa misuli hii inatokea pamoja katika goti na kutengeneza muishilio wa misuli wa kamba ngumu ujulikanao kama Achilles Tendon ambayo ukishika kwa nyuma ya kifundo unaweza kuhisi.

Kwakuwa eneo hili ni sehemu ya mguu ambao wachezaji wanautumia sana hivyo ni vigumu kigimbi kukosa majeraha hasa ligi hizi zinapoanza kwa kupaniana.

TAARIFA ZA JUMLA ZA KIGIMBI

Kitabibu kigimbi cha mguu hujulikana kama calf muscles, sehemu ina misuli mikubwa miwili huku msuli mmoja wapo ambao ndio mkubwa zaidi ndio huonekana zaidi kama kiazi.

Misuli hii huwa na miishilio ya nyuzi ngumu iliyopo nyuma ya mguu iliyoanzia kujipachika katika mfupa wa paja katika ungio la goti, kisha hujikita na kujichimbia katika mfupa wa kisigino.

Misuli hii kwa pamoja ina umuhimu kwa mwanasoka kuweza kucheza na kujongea mielekeo tofauti uwanjani, kigimbi huwa na kazi ya kuwezesha kupiga hatua kwenda mbele, kukunja goti, kuvuta misuli ya paja kwenda nyuma.

Mambo haya yote ni muhimu kufanyika kwa mwanasoka ili kuweza kucheza mchezo huo na kuleta burudani kwa mtazamaji.

Kutokana na kigimbi kilivyo huwafanya kazi kwa mara nyingi sana na mara kwa mara.

Ukimtazama vizuri mchezaji kama Stephane Aziz Ki au Jack Grealish ni mchezaji waliojengeka, unaweza kuona umbile la kigimbi lilivyo.  Misuli hii huwa na shughuli nyingi wakati wa kucheza soka ndio ligi zikianza kutimua vumbi huwa majeraha hayakosekani.

Kujaa kwa kigimbi na kutitia  nikuonyesha dhahiri misuli ya eneo hili inatumika sana na mwili na hivyo hakuna mrundikano wa mafuta katika eneo hilo kwani mara kwa mara yanatumika.

JERAHA LA KIGIMBI LIPO HIVI

Kigimbi kinaweza kupata majeraha kama vile kukakamaa au kubana, kuvutika sana na kuchanika. Mara nyingi majeraha ya kiazi cha mguu huanzia madogo madogo, ya kati na mpaka makubwa.

Misuli hii inaweza kupata tatizo la ghafla kutokana na mchoko uliopitiliza na kushindwa kupata lishe ya damu yenye hewa ya oksijeni. Hali hii husababisha misuli hii kubanwa, kukakamaa, kujikunja pasipo hiari na kumsababishia mchezaji maumivu makali.

Ingawa mara nyingi majeraha ya hapa huwa nikutokana na nyuzi zilizo kama bunda katika msuli kuvutika kupita kiwango chake.

Kupata michubuko, au jeraha bapa, jeraha la kuchanika msuli, na kukwanyuka kwa nyuzi ngumu zilizojipachika katika mfupa wa kisigino ni mojawapo ya majeraha ya kigimbi cha mguu.

Mara nyingine tunayaita majeraha ya hapa kama kujivuta kupita kiasi au kukwanyuka kwa nyuzi ngumu za miishilio ya misuli ya kigimbi.

Nyuzi hii ndio mwishilio wa msuli wa kiazi cha mguu pale unaposhika juu ya kisigino upande wa nyuma unaweza kushika ilipojishikiza katika kisigino.

Kwa mwanasoka jeraha linaweza kutokea wakati kufanya matendo kama vile mijongeo mbalimbali kama vile kukimbia, kutembea, kuruka, kupiga mpira na hata kuchezewa faulu.

Majeraha haya yanatokea pia wakati wa kubadili mwelekeo ghafla, unaposerereka na anapoteleza na mguu hivyo misuli kuvutika kupita kiasi.

Mwanasoka huanza kuhisi maumivu makali sana katika kigimbi, kuwa na michubuko, rangi ya sehemu ya jeraha kuwa nyekundu, kuvimba na maumivu.

Baada ya hali hii mtu anashindwa kuutumia mguu uliojeruhiwa kutokana na maumivu na kupoteza ufanisi wake.

Jeraha la kigimbi daraja la kwanza hutokea baada ya msuli kujivuta na kusababisha vijeraha vidogo vya ndani kwa ndani katika nyuzi nyuzi ndogo ndani ya msuli, huweza kupona kwa wiki 2-4.

Daraja la pili huwa na mchaniko mdogo wa juu juu katika msuli. Huchukua wiki 4-8 kupona endapo matibabu yakifuatwa kwa usahihi.

Jareha daraja la tatu huwa ni kuchanika kabisa kwa msuli na kugawanyika pande mbili. Kupona kabisa huchukua miezi 3-4. Huku mara nyingine upasuaji unaweza kufanyika ili kukarabati jeraha.

Majeraha haya ni moja ya majeraha yanayotokea mara kwa mara kwa wanasoka, lakini pamoja na kupona yanaweza kujirudia tena pale unaporudi mchezoni haraka.

Mchezaji atakayepata jeraha la kigimbi atahitajika kushikamana ushauri na matibabu na kumaliza programu maalum ya matibabu na mazoezi tiba ya viungo katika vituo maalum vya matibabu.

Kama mchezaji atahisi maumivu katika kigimbi asilazimishwe kushiriki mchezo wala mazoezi, kucheza na maumivu ni kuendelea kuongeza ukubwa wa jeraha.

Mchezaji arudi uwanjani endapo tu hakuna maumivu, uvimbe, pana utulivu wakati wakuutumia mguu huo na misuli haikakamai, na anaweza kuchuchumaa na kunyoosha goti bila tatizo lolote.

Usingaji wa misuli hiyo, unyooshaji kwa kutumia mazoezi mepesi na kuupa utulivu mguu kwa vifaa tiba ni muhimu ili kuponesha haraka jeraha hilo.

Mchezaji apate mapumziko kwa masaa 6-8 kwa siku, aepuke na matukio yote yanayoweza kumkosesha mapumziko.

Muhimu kupasha moto misuli kabla na baada ya mechi au mazoezi, vile vile kufanya mazoezi ya viungo katika kigimbi ili kulainisha misuli ya hiyo hatimaye kujikinga na majeraha ya kigimbi yasiyolazima.

Related Posts