Polisi watumia mabomu ya machozi kutuliza wananchi wanaoandamana Simiyu

Simiyu. Jeshi la Polisi mkoani Simiyu limelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya baadhi ya wananchi katika mji mdogo wa Lamadi Wilaya ya Busega, baada ya kufunga barabara kuu ya Mwanza-Simiyu na Mara kwa kile walichodai matukio ya watoto kupotea yameongezeka.

Wananchi hao walioanza kuandamana saa tatu asubuhi leo Agosti 21, 2024 hadi katika kituo cha Polisi cha Lamadi hadi muda huu (saa 8 mchana) bado wapo eneo hilo wakiwa na mawe, ambapo wanashambulia magari yanayopita barabarani huku wakidai wamechoshwa na matukio hayo.

Wanadai kwa kufanya hivyo wanaishinikiza Serikali na Jeshi la Polisi mkoani Simiyu kuchukua hatua ili kukomesha vitendo hivyo.

Tayari Kamati ya ulinzi na usalama mkoani humo ikiongozwa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Simon Simalenga imefika eneo hilo na kuimarisha usalama kwa kuwatawanya wananchi hao.

Mwananchi ilipomtafuta Simalenga amesema taarifa kamili itatolewa baadaye baada ya kuwatuliza wananchi hao.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi.

Related Posts