Arusha. Sakata la kijana Peter Charles (21) Mkazi wa kata ya Daraja Mbili jijini Arusha aliyedai kupigwa hadi kuvunjwa mguu na askari wa Jeshi la Polisi, amedai kupokea vitisho vya kukatishiwa uhai wake.
Peter alidai amevunjwa mguu ndani ya chumba cha mahojiano kilichopo ndani ya kituo cha kati cha Polisi Jijini Arusha Juni 6, 2024 akilazimishwa kukubali kosa la kucheza kamari baada ya kukamatwa na askari watatu akiwa nyumbani kwao usiku.
Hata hivyo Jeshi la Polisi mkoani humo limemtaka kutoa taarifa kuhusu vitisho hivyo ili zifanyiwe kazi.
Akizungumza na Mwananchi leo Agosti 21,2024, Peter amesema kuwa baada ya kutoa taarifa kwa waandishi wa habari, amekuwa akipokea vitisho vingi kutoka kwa watu asiowafahamu.
“Nimekuwa nikipigiwa simu na watu wanaokataa kujitambulisha ikiwemo siku moja nikiwa nimekaa nyumbani kwetu nikapigiwa simu na mtu akisema kuwa nisionekane tena kituoni kwenda kutoa ushirikiano juu ya mashtaka niliyoyatoa, la sivyo itakuwa ni mwisho wangu duniani.”
“Zaidi ya hiyo, nilipigiwa simu siku nyingine na mtu mwingine akisema kuwa nisiendelee kutoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya tukio hilo kama nayapenda maisha yangu,”amesema Peter.
Amesema kuwa baada ya kupokea vitisho hivyo amekuwa na hofu kubwa ya maisha yake na kuliomba Jeshi la Polisi kuharakisha upelelezi wa kesi yake ili watuhumiwa waweze kuchukuliwa hatua za kisheria kwa hatma ya watu wengine.
“Mimi sijakata tamaa hata wakiniua lakini sitarudi nyuma kikubwa mimi sina hatma tena duniani baada ya kuvunjwa mguu, lakini nitaendelea kufuatilia kesi hii ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria kwa hatma ya watu wengine ambao wanaweza kuwafanyia hivi endapo likiachwa juu juu,”amesema Peter.
Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo amesema kuwa upelelezi wa suala hilo unaendelea ukikamilika utafikishwa kwenye vyombo vya sheria ili lichukuliwe hatua zaidi.
“Narudia tena kama nilivyosema awali, hakuna mtu yuko juu ya sheria hivyo naombeni mtuache tuendelee na uchunguzi na ikibainika kuna kosa limetendeka basi mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu shtaka lake kwa wakati huo,” amesema Masejo.
Hata hivyo Kamanda Masejo amesema kuwa askari huyo bado anaendelea na majukumu yake ya kila siku ya kulitumikia Jeshi la Polisi kama kawaida.
“Unavyoniuliza kama bado yuko kazini unataka nijibu nini hapo, kwani mtu akituhumiwa ndio ametenda kosa? Subirini akibainika ana kosa Jeshi la Polisi litachukua hatua zake,” amesema Masejo.
Masejo ametumia nafasi hiyo, kumtaka kijana Peter kutoa taarifa kwa jeshi hilo kama amepokea vitisho kutoka kwa mtu yoyote na suala hilo litafanyiwa kazi.
Endelea kufuatilia Mwananchi.