Dar es Salaam. Wakati asilimia 44 ya wakulima milioni 860 duniani kote wakiathiriwa na sumu inayohusiana na viuatilifu, wadau wameanzisha mikakati mipya ya kukabiliana na hatari hizo.
Takwimu za kutisha za mwaka 2020, zilizoripotiwa na Kituo cha Taifa cha Habari za Bioteknolojia (NCBI) nchini Marekani, zilionyesha utumiaji duni wa zana za kujikinga kama sababu kuu inayochangia sumu ya viuatilifu.
Utafiti wa NCBI umefichua zaidi wakulima katika Asia ya Kusini, Kusini-Mashariki mwa Asia na Afrika Mashariki ndio walioathiriwa zaidi na matumizi ya viuatilifu.
Katika kukabiliana na suala hilo kubwa, mavazi mapya ya kujikinga yametengenezwa Afrika Mashariki ili kuwalinda wakulima kutokana na madhara ya viuatilifu.
Hayo yamesemwa jana Jumanne Agosti 20, 2024, Ofisa Mtendaji MKuu wa Bodi ya Kudhibiti Wadudu Waharibifu Kenya (PCPB), Fredrick Muchiri, wakati wa uzinduzi wa zana hizo za kujikinga zilizoundwa kwa ajili ya nchi za eneo hilo.
Amesema upatikanaji wa mavazi hayo ni matokeo ya ushirikiano kati ya PCPB na Kituo cha Kimataifa cha PPE (ICPPE) katika Chuo Kikuu cha Maryland Eastern Shore, BASF, na Syngenta Kenya.
Muchiri amesisitiza uamuzi wa kutengeneza mavazi hayo ya kujikinga ulichochewa na hitaji la kulinda afya za wakulima wanapotumia dawa za kuulia wadudu shambani.
Kabla ya kuzinduliwa, nguo hizo zilijaribiwa na wakulima 110 kutoka sehemu mbalimbali za Kenya, ambao walitoa maoni kuhusu utumiaji wa raha, uimara, rangi, na vipengele vingine vya usanifu.
“Matumizi ya viuatilifu lazima yafanywe kwa uzingatiaji madhubuti wa hatua za usalama, ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya Vifaa vya Kujikinga (PPE).
“Kama chombo cha udhibiti wa bidhaa za kudhibiti wadudu nchini, tunabaki kujitolea kuhakikisha kuwa PPE inayotumiwa hapa inaendana na viwango vinavyofaa, inapatikana kwa bei nafuu, na inapatikana kwa urahisi katika masoko yetu,” amesema Muchiri.
Amesisitiza umuhimu wa PPE kwa kilimo endelevu, akibainisha matumizi ya mavazi hayo ya kinga huwasaidia wakulima kupata mavuno bora bila kuathiri afya zao. Nguo za kinga zilizoidhinishwa na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO) zimetengenezwa kwa nyenzo za nguo zinazoweza kupumua, na kutumika tena.
Mkuu wa Kikanda wa Suluhu za Kilimo katika BASF Afrika Mashariki, Gift Mbaya amesema kuwekeza katika mavazi hayo ya kinga ni zaidi ya kulinda afya za wakulima; pia inalinda jamii pana.
“Kwa kuwekeza katika mavazi ya kujikinga, sio tu kwamba tunalinda afya na usalama wa wakulima wetu, lakini pia na jamii tunamofanyia kazi. Tumejitolea kuhakikisha mustakabali endelevu na wa kuwajibika kwa ulimwengu unaotuzunguka,” amesema Mbaya.
Mratibu wa mpango wa ICPPE, Anugrah Shaw, amekiri baadhi ya watumiaji wanasitasita kuvaa nguo za kujikinga kutokana na wasiwasi kuhusu joto na usumbufu. Hata hivyo, bidhaa hiyo mpya inalenga kushughulikia masuala hayo kwa kusawazisha ulinzi na faraja.
Mkuu wa Eneo la Biashara Afrika Mashariki na Kusini, Given Mudenda, ameeleza mpango huo umelenga katika kuhakikisha usalama wa wakulima na wafanyakazi wengine wa mashambani.
“Tunafanya juhudi kubwa za uwakala na tunajivunia kuhusishwa na uzinduzi wa mavazi ya kwanza ya ulinzi ya kibinafsi yaliyoidhinishwa na Kenya.
“Vazi hili la kiubunifu la kinga huongeza ulinzi wa mazao na kukuza utamaduni wa usalama miongoni mwa wakulima na waendeshaji nchini kote na pengine kwingineko. Kila mkulima anastahili kupata zana bora za kinga, na kuwawezesha kufanya kazi endelevu,” amesema Mudenda.