Mashujaa Queens yahamia Dar | Mwanaspoti

WAKATI msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), ukisubiriwa kwa hamu kuanza, Amani Queens (kwa sasa Mashujaa) imetangaza kuhamia Dar es Salaam kuwa makao makuu badala ya Lindi ilipokuwa awali.

Msimu uliopita Amani ilimaliza katika nafasi ya sita katika msimamo wa WPL ikishinda mechi saba, sare mbili na kupoteza mechi tisa.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa timu hiyo, Morice Katumbo alisema rasmi watahamishia makazi yao Dar es Salaam na kutoka Lindi.

Katumbo alisema kulinagana na ratiba ya ligi hiyo kuanza Septemba, wanatarajia kuanza kambi mwanzoni mwa mwezi ujao.

“Msimu uliopita hatukuanza vizuri kutokana na changamoto za kifedha lakini msimu huu tumeanza maandalizi mapema na kambi yetu inaweza kuwa Masaki au Mbezi Beach kulingana na kikao cha mwisho cha viongozi kitakavyoamua,” alisema Katumbo na kuongeza

“Pia tumefanya marekebisho ya wachezaji hususani maeneo mawili ya ulinzi na ushambuliaji kutokana na msimu uliopita hatukuwa vizuri katika maeneo hayo.”

Katika mechi 18 za WPL msimu uliopita, Amani ilifunga mabao 22 na kuruhusu 35 ikiwa ni miongoni mwa timu tatu zilizoruhusu mabao mengi msimu uliopita.

Related Posts