Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliyoketi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeelezwa jinsi aliyekuwa Ofisa Usalama wa Taifa, Zaburi Kitalamo (50) alivyoingia makubaliano na mganga wa kienyeji ya kumuua mke wake, Atusege Kitalamo, baada ya kubaini anamroga hadi anaishiwa nguvu za kiume.
Mganga huyo ambaye hakutajwa jina lake aliwaagiza vijana wawili kwenda kufanya mauaji ya Atusege ikiwa ni kutimiza suluhisho la mwisho la matibabu ya Kitalamo, aliyekuwa mgonjwa kwa wakati ule.
Kitalamo au kwa jina lingine Peter Alex Kitalamo, ambaye ni mkazi wa Uzunguni Wilaya ya Urambo, mkoani Tabora anadaiwa kumuua mke wake aitwaye Atusege Kitalamo kwa kumchinja na kisha mwili wake kuutupa mtoni.
Ofisa huyo wa Usalama, anadaiwa kutenda kosa hilo, akishirikiana na wenzake wawili kwa imani za kishirikina.
Mbali na Katalamo, washtakiwa wengine ni mfanyabiashara, Roger Salumu (25), maarufu Mayala na mkazi wa Utewe Wilaya ya Urambo.
Mwingine ni Furaha Ngamba (47), mganga wa jadi na mkazi wa Uyogo, Wilaya ya Urambo.
Ushahidi huo umetolewa leo Jumatano, Agosti 21, 2024 na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Mbagala, Debora William mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Abdallah Ally Mkama aliyeongezewa Mamlaka ya ziada kusikiliza kesi hiyo ya mauaji.
Akiongozwa kutoa ushahidi na wakili wa Serikali Mwandamizi, Deborah Mushi, shahidi huyo amesoma maelezo ya ungamo aliyoyatoa Kitalamo mbele ya mlinzi wa amani ambaye aliyatoa kwa Hakimu William.
William ambaye ni shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka alidai kuwa mshtakiwa aliishi na mke wake kwenye ndoa tangu mwaka 2012.
Amedai kwa kipindi hicho kulikuwa na matukio mengi ya kichawi yanampata akaona anayefanya hivyo ni mke wake marehemu Atusege yaliyodumu ndani ya miaka tisa ya ndoa.
“Kitalamo alidia alikuwa akiumwa magonjwa mbalimbali kutaka kupooza mwili, kupungua nguvu za kiume na ngozi kutoka mwilini mwake, lakini kwa kipindi hicho alikuwa akimuuliza mke wake kuwa yeye ni mchawi na alikuwa akikataa,” amedai shahidi huyo. wakati akisoma maelezo ya ungamo ya mshtakiwa huyo na kuongeza.
“Kitalamo baada ya kumuuliza sana mke wake kwa muda mrefu, kuna siku Atusege alimueleza bibi yake mzaa baba ni mchawi sana, ikabidi aende kwa mganga wa kienyeji, lakini matokeo yake alikuwa anapona anaumwa tena,” amedai shahidi huyo.
Ameendelea kudaiwa kuwa marehemu alikuwa ana mpango wa kumuua, alishawahi kumuweke sumu kwenye soda akatapika, wakakubaliana na mganga kwamba matibabu yake yatakuwa Sh2 milioni na akarudi kukaa nyumbani kwao wilayani Urambo.
Hakimu huyo, ameendelea kusoma maelezo hayo kwamba Desemba 12, 2020 Kitalamo alipigiwa simu na mganga kwamba anatakiwa kuongeza fedha Sh3 milioni ili ziwe jumla Sh5 milioni.
Ilidaiwa mshtakiwa alimtumia mganga huyo Sh500,000 na kumuahidi kwamba akimaliza matatizo aliyoyapata ya msiba ya mke wake atamalizia fedha zilizobaki, baada ya mazishi mganga alimpigia simu akatuma Sh2.5 milioni kwa njia ya wakala.
“Suluhisho la mganga la mwisho aliwachukua vijana wawili kutoka Wilaya ya Urambo kwenda kufanya mauaji hayo, baada ya kutekelezwa mganga alimpigia simu tena akimtaka aongeze fedha zitimie Sh12 milioni kwa sababu kazi ilikuwa ngumu,”alidai William
Iliendelea kudaiwa kuwa mganga huyo alimueleza kuwa watu hao walikwenda nyumbani kwake wakiwa na bastola na wamemueleza kuwa asipotekeleza hilo watamfuata nyumbani kwake wamdhuru na yeye akamueleza kuwa hana fedha kwa wakati huo.
Shahidi huyo aliendelea kusoma kuwa, mganga alimueleza ana gari mbili ataziweka rehani akishapata fedha hizo atamrudishia, baada ya muda kidogo alipigiwa simu na mganga akashangaa anakamatwa.
“Kitalamo aliitwa katika kituo chake cha kazi Oysterbay, Makao Makuu ya Usalama wa Taifa ndipo akakamatwa,” amedai William
Aliendelea kudai kipindi anachukua maelezo ya ungamo, mshtakiwa huyo alikuwa Mahakama ya Mwanzo Magomeni na pia aliweza kumtambua mshtakiwa licha ya kwamba amekonda sana.
“Naweza kumtambua mshtakiwa Peter Kitalamo kwa sababu nilimchukua maelezo mimi kwa ukaribu, hapa mahakamani naweza kumtambua licha ya kwamba amekonda sana alikuwa mtu kweli siku alikuwa amevaa suti yake nyeusi ya Usalama wa Taifa,” alidai shahidi.
Katika kesi ya msingi, wakili Mushi alidai washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo, Desemba 12, 2020 katika eneo la Kinzudi Wilaya ya Ubungo, ambapo walimuua Atusege Alex Kitalamo.
Inadaiwa siku hiyo, usiku washtakiwa Shabani na Ng’amba walivamia nyumba ya Atusege na kumpeleka kwenye mto uliopo karibu nyumba hiyo na kisha kumchinja hadi kufa, baada ya kuelekezwa na Zaburi (mume wa marehemu) juu ya imani za kishirikina.
Kesi bado inaendelea na usikilizwaji kwa shahidi wa nne kutoa ushahidi wake…