Dk Jafo asisitiza usafi kuepusha magonjwa

Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amesema huduma bora za maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi (WASH) katika Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani zitaimarisha ukuaji wa uchumi kutokana na kupungua kwa mzigo wa magonjwa yanayotokana na maji.

Dk Jafo ametoa kauli hiyo leo Agosti 21, 2024 jijini Dar es Salaam alipokuwa akieleza ufanisi wa programu ya tabia za usafi katika shule na vituo vya afya inayotekelezwa wilayani Kisarawe kwa miaka mitatu.

Programu hiyo iliyoanza kutekelezwa mwaka 2021 hadi 2024, imefadhiliwa na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (Jica) pamoja na ufadhili kutoka WaterAid, kwa  zaidi ya pauni 2.28 (zaidi ya Sh8 bilioni), ukilenga kuboresha tabia za usafi na miundombinu katika shule 30 na vituo vya afya 15 wilayani humo.

Dk Jafo amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) hususan lengo namba tatu linalolenga kuhakikisha maisha yenye afya na ustawi kwa wote katika kila umri, na lengo namba sita linalolenga kuhakikisha upatikanaji wa maji safi, usafi wa mazingira na usafi binafsi.

“Upatikanaji wa maji safi na huduma bora za usafi hupunguza uwezekano wa kupata magonjwa yanayotokana na maji kama vile kuhara.”

“Hii ina maana kupungua kwa gharama za matibabu na kuhakikisha kunakuwa na jamii yenye afya bora,” amesema Jafo ambaye pia ni Mbunge wa Kisarawe.

Waziri Jafo amesisitiza umuhimu wa viongozi, walimu, wanafunzi na jamii kwa ujumla kuhakikisha uendelevu wa miundombinu ya WASH iliyojengwa ili kudumisha usafi.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti amesema wilaya hiyo bado inahitaji huduma zaidi za WASH kwani ina jumla ya shule 120.

“Tunazo shule 100 zinazohitaji huduma hizo. Hii itaokoa watoto dhidi ya magonjwa yanayotokana na maji, hivyo kuboresha ufaulu wao kitaaluma,” amesema Magoti.

Anna Mzinga, Mkurugenzi mkazi wa WaterAid Tanzania amesema kuwa ujenzi wa vyoo vya umma, vituo vya kunawa mikono na miundombinu ya maji na hifadhi umebadilisha kwa kiasi kikubwa mazingira ndani ya vituo vya afya na shule vilivyochaguliwa wilayani Kisarawe.

“Mikakati ya kubadili tabia ilitumika na kuingizwa ili kuwawezesha jamii pamoja na vifurushi vya usafi mahususi kwa shule na vituo vya afya ili kuimarisha tabia za usafi za maisha,” amesema.

Amesema mradi huo umezaa matunda kwa kuboresha tabia ya kunawa mikono miongoni mwa walengwa, kuunda ushahidi wa kina wa tabia za usafi wa mikono,  kuunda vifurushi viwili vya usafi vyenye mwongozo wa hatua kwa hatua juu ya jinsi ya kufanya vipindi vya usafi katika shule na vituo vya afya.

Related Posts