Dar es Salaam. Bohari ya Dawa (MSD) imetaja mikakati kuhakikisha wenye magonjwa sugu ya figo wanaohitaji huduma ya kuchujwa damu kupitia mashine maalumu ‘dialysis’ wanapata huduma hiyo kwa gharama nafuu.
Wenye kuhitaji huduma hiyo, hulazimika kulipia kati ya Sh180,000 mpaka Sh150,000 kwa mzunguko mmoja ambao huchukua takribani saa nne, huku mgonjwa akihitaji kupewa tiba hiyo mara mbili mpaka tatu kwa wiki.
Ili kufanikisha hilo, MSD imejikita katika ununuzi wa mashine na vitendanishi moja kwa moja kwa wazalishaji ili kuvipata kwa gharama nafuu, wakizingatia ubora.
Hayo yamesemwa leo Agosti 21,2024 na Meneja wa Kanda ya MSD Dar es Salaam, Betia Kaema wakati akipokea tuzo ya shukurani kutoka Hospitali ya Temeke kwa kutambua maboresho ya huduma ikiwemo ya kusafisha damu, kwa wagonjwa wa figo na upatikanaji wa dawa muhimu uliofikia asilimia 98.
Betia amesema kwa sasa wanajikita kuona namna gani wanaweza kupata mashine na vitendanishi kwa gharama nafuu, ili waweze kushusha bei zaidi na hospitalini gharama ziendelee kushuka.
“Huduma ya dialysis ni ghali, tunachokifanya sasa MSD ni kutafuta wazalishaji ambao tutaendelea kupata mashine hizi kwa bei rahisi.”
“Upatikanaji wa mashine ni kitu kimoja lakini uwezo wa wagonjwa kumudu gharama ni kitu kingine, tunaendelea kupata washitiri wengine kwa sababu na sisi tunaenda moja kwa moja kwa wazalishaji ili kupata bei ambayo itakua nafuu kwetu na watumiaji. “Tupo katika hatua kuhakikisha tunaongeza wigo wa uzalishaji, lakini wakati huohuo tukizingatia ubora, kwa kuwa hata ukiwa na bei ndogo lakini usipozingatia ubora hutatoa huduma inayohitajika, tunapambana kuhakikisha tunapata wazalishaji ambao bei zao zitakuwa zinaendelea kuwa chini lakini vifaa vyenye ubora.”
Aidha Betia amesema mpaka sasa katika Kanda ya Dar es Salaam, hospitali tano za rufaa za mkoa tayari zinatoa huduma hiyo kati ya tano zilizopo.
Amezitaja hospitali hizo kuwa ni Mwanangamala, Amana, Temeke, Tumbi na Hospitali ya Rufaa ya Morogoro.
Ameongeza kuwa huduma ya kusafisha figo ni moja ya kipaumbele chao, “Kwa miaka miwili nyuma tumekuwa tukihudumia hospitali tano na sasa tumeiwezesha Hospitali hii ya Temeke. Lengo letu ni kuhakikisha wateja wetu wote wanaweza kutoa huduma hii kwa bei za chini ili kuwawezesha Watanzania kupata huduma hii kwa bei wanazoweza kuzimudu.”
Akikabidhi tuzo hiyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Dk Joseph Kimaro amesema wanaishukuru MSD kuendelea kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana kwa wakati, hasa mashine 10 za kusafisha damu (dialysis).
Amesema mashine hizo zina uwezo wa kutoa huduma kwa wagonjwa 30 kwa siku na sasa wanahudumia wagonjwa 18 pekee.
“Mashine tumeshazifunga na tumeanza huduma kuanzia mwezi wa sita mwaka huu. Kwa sasa tuna wagonjwa 18 wanapata huduma hapa kwa bei nafuu ya Sh150,000 kwa wale wanaolipa papo kwa papo,” amesema Dk Kimaro.
Dk Kimaro ameongeza kuwa, pamoja na huduma ya kusafisha figo pia imeiwezesha huduma ya upatikanaji dawa muhimu kufikia asilimia 98 na kupunguza malalamiko kwa wagonjwa wanaopata huduma hospitalini hapo.