Kondoa. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, ametoa wito kwa wananchi wa wilaya za Kondoa na Chemba, mkoani Dodoma, kuwekeza kwa dhati katika elimu ya watoto wao.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika mkoa wa Dodoma, Jumatano, Agosti 21, 2024, Dk Mpango alisisitiza umuhimu wa elimu kama msingi wa maendeleo endelevu kwa watoto na taifa kwa ujumla.
Katika ziara hiyo, Dk Mpango amesema kuwa watoto wenye elimu bora wana nafasi kubwa zaidi ya kufanikiwa katika maisha yao ya kitaaluma na kijamii.
“Elimu inatoa maarifa na uwezo wa kufikiria kwa kina, ambayo ni muhimu kwa mafanikio ya baadaye ya watoto wetu,” alieleza.
Aliendelea kwa kusema kuwa hata kama nchi inapata maendeleo katika nyanja mbalimbali kama vile uwepo wa umeme na miundombinu ya kisasa kama treni ya SGR, bila kuwa na watoto wenye elimu, mafanikio hayo hayataweza kudumu na kuwa na manufaa kwa jamii nzima.
Katika hotuba yake kwenye Shule ya Wanafunzi Wenye Mahitaji Maalum ya Iboni iliyopo Kondoa mjini, Dk Mpango aliwasihi wazazi wa Kondoa kutambua na kutumia fursa ya shule hiyo kwa kuwapeleka watoto wao wenye mahitaji maalum kujiunga na kupata elimu.
“Msifiche watoto wenu wenye mahitaji maalum ndani ya nyumba. Ninaambiwa watoto wenye mahitaji maalum waliopo hapa ni 30 tu, wakati kwenye mkoa mzima kuna zaidi ya watoto 200 wenye mahitaji hayo,” alieleza kwa msisitizo.
Aliongeza kuwa kuwapeleka watoto wenye mahitaji maalum shuleni si tu kuwapa fursa ya elimu, bali pia ni kuwajengea msingi wa kujitegemea na kuchangia katika jamii wakiwa na uwezo na maarifa yanayohitajika.
“Elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum ni suala la haki na ni wajibu wetu kama wazazi kuhakikisha wanapata haki hiyo,” alisema.
Akiwa kwenye mkutano wa hadhara wilayani Chemba, Dk Mpango alirudia tena wito wake kwa wazazi kuwekeza katika elimu ya watoto wao.
Alifafanua kuwa wazazi wanaowekeza kwenye elimu ya watoto wao wanajenga msingi wa ustawi wa kiuchumi wa familia yao kwa vizazi vijavyo.
“Watoto wenye elimu ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla,” alieleza Dk Mpango, akiongeza kuwa elimu bora inachangia katika kujenga taifa lenye ustawi na maendeleo endelevu.
Kwa mujibu wa Dk Mpango, elimu ina nafasi muhimu katika kujenga maadili na tabia njema kwa watoto.
Alisema, “Kumekuwa na mmonyoko wa maadili katika jamii yetu, ambapo mambo ambayo huko nyuma yalikuwa hayawezi kutamkwa sasa yamekuwa yakifanyika hadharani. Hivyo, elimu ni njia mojawapo ya kuwarejesha watoto wetu kwenye maadili mema na misingi ya utu.”
Aliwataka wazazi kuwapa watoto wao elimu ya dini pia, akisisitiza kuwa elimu hiyo ni muhimu katika kujenga msingi wa maadili mema, nidhamu, na heshima kwa wengine.
“Elimu ya dini ni nyenzo muhimu kwa watoto wetu, kwani inawasaidia kukuza tabia njema, kuwajengea hofu ya Mungu, na kuwafanya wawe raia wema na wenye kufuata misingi ya haki,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alieleza kuwa wilaya ya Kondoa ina vivutio vya kipekee vya utalii, ikiwa ni pamoja na Hifadhi ya Mkungunero ambayo ina wanyama wote isipokuwa faru, pamoja na michoro ya Koro ambayo ni kivutio kingine muhimu kwa watalii.
Alisema kuwa Serikali imepeleka zaidi ya Sh77.9 bilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa huo, huku zaidi ya Sh4 bilioni zikiwa zimeelekezwa katika Wilaya ya Kondoa.
“Fedha hizi zimetekeleza miradi mingi ya maendeleo ambayo imeleta mabadiliko chanya katika maisha ya wananchi wetu,” alieleza Senyamule.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Fatma Nyangasa, ameelezea maendeleo yanayoendelea katika wilaya yake, akisisitiza juhudi kubwa zinazofanywa ili kuhakikisha kwamba wilaya hiyo inazidi maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Amesema kwamba Wilaya ya Kondoa imepiga hatua kubwa katika nyanja mbalimbali, ikiwemo sekta za elimu, afya, miundombinu, na kilimo.
Nyangasa pia ameelezea juhudi za wilaya yake katika kuboresha sekta ya elimu, akisisitiza umuhimu wa elimu bora kwa watoto wote.
Katika sekta ya afya, Nyangasa alielezea jinsi wilaya yake imeweka kipaumbele katika kuboresha huduma za afya, hususan katika vituo vya afya vya vijijini.
Aliainisha kuwa vifaa vya matibabu vimeongezwa, na juhudi zinaendelea kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya unakuwa wa haraka na bora zaidi kwa wananchi wote wa Kondoa.
Nyangasa amesema Wilaya ya Kondoa inaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wote, na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi katika kila hatua ya maendeleo.