Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, ameipongeza Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Jafo ametoa pongezi hizo leo jijini Dar es Salaam wakati akipokea taarifa ya Mradi wa Uboreshaji wa Tabia za Usafi kwenye shule 30 na vituo vya afya 15 katika Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.
Mradi huo ambao umegharimu zaidi ya Sh. bilioni 4 umefadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) kwa kushirikiana na Shirika la WaterAid.
Amesema mradi huo unatekeleza lengo la tatu na la sita ili kuhakikisha maisha ya watu wenye afya njema na ustawi wa watu wote wa rika na upatikanaji wa maji salama, usafi wa mazingira na usafi kama hitaji la msingi zaidi la afya na ustawi wa binadamu yamefanikiwa.
“WaterAid kupitia mradi huu mmetusadia kutekeleza malengo haya kwa kuhakikisha mnaifikia jamii ya pembezoni inayokosa huduma ya maji inapatikana na suala la afya bora, mmekuwa mkichochea kwasababu bila maji wananchi hawawezi kuwa na afya njema,”amesema Jafo.
Aidha, amesema kuboreshwa kwa huduma za maji, usafi wa mazingira katika Wilaya ya Kisarawe kutasaidia ukuaji wa uchumi na kupunguza magonjwa yatokananyo na kukosekana kwa huduma ya maji,” amesema Jafo na kuongeza kuwa;
“Serikali inatumia fedha nyingi kutibu magonjwa yanayosababishwa na maji, hivyo kupatikana kwa maji safi kunapunguza tatizo hilo na watu kukua kiuchumi na kuikinga jamii na magonjwa yatokanayo na hali duni ya usafi.”
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti, alisema wilaya yake bado inahitaji vifaa zaidi vya WASH kwa kuwa ina jumla ya shule 120.
Nayr Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la WaterAid, Ana Mzinga, amesema kwa ufadhili wa Shirika la JICA, waliweza kubuni mradi wa kufundisha namna bora ya matumizi ya maji katika vituo vya afya 15 na shule 30 katika Wilaya ya Kisarawe.
Amesema mradi huo wameufanya katika kipindi cha miaka mitatu wamepata ushirikiano kutoka serikali na wadau wa maendeleo ambao wamesaidi kufanikisha utafiti huo.
“Tafiti hii imeonyesha kuwa kutapokuwa na maji usafi wa mazingira na namna endelevu za kufundisha njia bora ya kutumia vyoo na maji katika kunawa kuna uwezekano wa kupunguza magonjwa ambayo yanaambukiza kutokana na uchafu,”amesema.
Aidha, Mzinga amesema katika utafiti huo waligundua utumiaji wa maji hasa baaada ya kutoka chooni ulikuwa upo chini kutokana na uelewa na ukosefu wa miundombinu ya kuwawezesha kunawa mikono kwa wanafunzi wanapotumia vyoo.