Wadau waonyesha njia kukabili matukio ya unyanyasaji katika jamii

Dar es Salaam. Wakati matukio ya kikatili ikiwemo ulawiti, vipigo yakiendelea kuripotiwa nchini Tanzania, wanaharakati wanasheria na waandishi wa habari wamesema lazima Taifa liungane katika kuripoti na kupaza sauti wa matukio ya namna hiyo.

Baada ya kupaza sauti, wameshauri sheria kufuata mkondo wake ili wale wote wanaohusika na vitendo hivyo wawajibishwe kwa mujibu wa sheria ili kukomesha aina hiyo ya matukio ambayo ina athari kimwili hata kisaikolojia.

Wadau hao wameyasema hayo leo Jumatano Agosti 21, 2024 katika mjadala wa Mwananchi Space uliofanyika katika mtandao wa X (zamani Twitter) wenye mada inayohoji: Je, Wanahabari na Wanaharakati wanafanya vya kutosha kukomesha ukatili na unyanyasaji katika jamii?

Mhariri wa Jarida la Familia wa Mwananchi, Elizabeth Edward akichokoza mada hiyo amesema takwimu za hali ya uhalifu zilizotolewa na Jeshi la Polisi kwa mwaka 2023 kulikuwa na waathirika 37,448 kutoka 30,566 mwaka 2022 ikiwa kuna ongezeko la idadi ya watu waliokutana na ukatili.

“Ulawiti umezagaa si kwa vijana wala watoto wa jinsia zote, kwa mwaka 2023 kuna wanaume 2,231 walikutana na ulawiti huku wanawake wakiwa 257. Kwenye vipigo kuna wanaume 118 na wanawake 323.

“Shambulio la aibu 309 kwa wanaume na wanawake 1075 ambapo kwa takwimu hizo inaonesha kuna hali mbaya kwenye jamii,” amesema Elizabeth

Amesema waandishi wa habari wanapaswa kuongeza jitihada katika kuripoti matukio hayo.

Amesema sio kwamba miaka ya nyuma kulikuwa hakuna aina hiyo ya matukio bali kwa sasa uelewa na elimu kwa jamii inasaidia kuyaripoti.

Hivyo amesema waandishi na wanaharakati wanafanya kinachotakiwa lakini bado nguvu inahitajika kutokana na uwepo wa matukio hayo.

Amesema lazima hatua zichukuliwe kuhakikisha sintofahamu inayoendelea nchini ya matendo ya kikatili inakomeshwa.

Changamoto utekelezaji wa sheria

Akichangia mada hiyo, Ofisa Programu Mwandamizi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Getrude Dyabene amesema changamoto iliyopo kama nchi ni utekelezaji wa miongozo na sheria zilizopo na wakati mwingine maagizo ndiyo yanayotawala.

Amesema katika kukomesha ukatili lazima ifuatwe sheria na miongozo iliyopo ambayo kwa namna moja au nyingine haifuatwi. Amesema Chanzo kinaweza kuwa ni kutokujua au hakuna mtu wa kukumbusha kuzitekeleza sheria zilizopo.

“Mfano mtu amefanya kosa lazima afikishwe kwenye vyombo vya haki ili kuchukuliwa hatua lakini unakuta kama vile utawala wa sheria haupo na inaonekana kama haifanyi kazi, ipo kwa baadhi ya makundi ya watu na ukiangalia Katiba inasema hakuna aliye juu ya sheria.”

“Ukienda ngazi ya chini unakuta mambo mengi yanafanyika bila kufuata sheria kwa sababu hawajui au hakuna mtu anayewawajibisha wao kusimamia sheria,” amedai.

Amesema kwa upande wao LHRC wanakutana na kesi za namna hiyo na mara nyingi wakipeleka mapendekezo yao serikalini huwa wanaomba sheria zitekelezwe.

Mmoja ya mchangiaji wa mjadala, Yassin Hassan amesema kwa upande wake amepoteza imani na vyombo vya habari baada ya kuacha kuripoti habari zinazogusa jamii moja kwa moja kama matukio ya utekaji ubakaji na ukatili.

Amesema wanahabari wanahofu inayoathiri utendaji wao na wamekubali kuwa chawa wa Serikali.

Kwa upande wake, Gwangwai amesema tasnia ya uandishi inadidimia kwani hakuna habari za uchunguzi za matukio ya utekaji yanayoripotiwa mara kwa mara.

Amesema hata wananchi wamepoteza imani kwa waandishi wakiwaona hawafanyi kazi yao ipasavyo. Amesema hata maudhui ya kila siku ya vyombo vya habari mengi hayaigusi jamii moja kwa moja. 

Aidha, David amesema waandishi wamekuwa machawa wakati jambo likiwa limevuka mipaka na kufika kwenye vyombo vya kimataifa, ndipo vyombo vya ndani vinaanza kutangaza.

Mwandishi wa habari za jinsia Zanzibar, Najat Omary amesema kila mmoja ana haki ya kuhoji na kukemea matukio ya kikatili ambayo yameendelea kutikisa nchi.

Amesema katika masuala ya kijamii matukio hayo yanapaswa kuzungumzwa na watu wote wanaotaka kitu kitendeke kwa haki na usawa na si kunyoosheana vidole nani afanye, akisema ndio chanzo cha mpasuko.

Amesema sauti za wengi zinasikilizwa sana kuliko sauti ya mwandishi na hicho ndicho kilicholeta mageuzi kiutendaji. “Kila mmoja ana wajibu wa kuzungumza iwe linamuhusu au halimuhusu.”

Suala hilo lichukuliwe kama la kila mtu na si waandishi pekee. Aidha, Najat ameishukuru jamii kwa kuelimika ambayo inasaidia waandishi wa habari kutoa taarifa na inawapa mahali pa kuanzia katika habari hizo ikiwa ni tofauti na zamani.

“Kwa sasa wananchi wako tayari kusema fulani amebakwa, amebakwa na nani na wapi, ambapo inaleta urahisi hivyo jamii inaelewa vita hii ni ya mtu mmoja mmoja,” amesema.

Mwandishi na mwanaharakati wa kutetea haki za watoto, Devotha Tweve amesema jukumu la kutokomeza ukatili ni jukumu la kila mmoja hajilishi kuwa ni mwanahabari au mwanaharakati licha ya kupelekewa lawama nyingi kwa wanahabari.

“Tusifichefiche wala kumung’unya maneno kuna kauminywaji tumeambiwa uhuru una mipaka kuzungumza sio shida bali unachokizungumza baadaye kitaleta matokeo gani ndiyo kuna shida hapo,” amesema Tweve.

Amesema sasa hivi habari za uchunguzi zimekuwa ni shida kwa sababu wenyewe pia wanaogopa ndiyo maana baadhi ya wanahabari wamekuwa machawa hiyo yote sababu ya woga wa madhara ya baadye.

“Sio huku nyuma watu walikuwa wakifanya habari za uchunguzi kwa kugusa mamlaka na tumeona madhara waliokuwa wanayapata ndiyo maana vyombo vya habari vinaogopa,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Programu The Launchpad Tanzania, Angela Karashani amesema kwa miaka iliyopita kuanzia 2022 kuna hatua kubwa imepigwa katika kukomesha ukatili, lakini kuna vizingiti ambavyo jamii bado haijapokea kwenye jambo gani lifanyike na lipi lisifanyike.

“Kizingiti kimojawapo ni sheria zipo lakini hazifuatwi kwa hiyo unaenda sehemu unaelimisha watu kwamba kuna sheria hii inamlinda mtoto wako, hii inamlinda ndugu yako lakini wanauliza sheria hii nikienda mamlaka husika itafuata mkondo wake na sitajiingiza katika unyanyasaji wa wanawake?” amesema Angela.

Amesema kwa baadhi ya harakati zinazofanywa kupitia madawati ya jinsia na watoto wanaharakati wamekuwa wakielimisha jinsi ya kupokea waathirika, kuwasikiliza na kuwaelimisha ili na wao wasijikute wamewafanyia ukatili kwa namna moja ama nyingine.

Katika kuhakikisha wanaharakati wanafanikiwa kupiga hatua wanatakiwa kufika kwenye jamii na kuwaeleza namna ya kufanya, kwani sheria ipo kinachotakiwa ni kufuatwa.

“Sheria inaonekana kama kisu butu kwani kila kitu kinakuwa mezani akiwepo shahidi, lakini mtuhumiwa anatembea akiwa huru.”

‘Taasisi ya kwanza ni familia’

Mshauri wa masuala ya afya na jinsia Dk Katanta Simwanza amesema taasisi ya kwanza ni familia kukomesha vitendo vya ukatili kwani vitendo hivyo vinaanzia katika ngazi ya familia. Pili amesema shule na nyumba za ibada zinapaswa kuwapa elimu watoto dhidi ya matendo ya kikatili.

Vilevile ameshauri kwamba jukumu la kukomesha vitendo hivyo ni la watu wote wala si la kundi au mtu mmoja mmoja, hivyo jamii inapaswa kusimama imara.

Related Posts