Wawili watoa ushahidi kesi ya ‘waliotumwa na afande’

Dodoma. Mashahidi wawili wa upande wa mashtaka wamekamilisha kutoa ushahidi katika kesi ya ubakaji kwa kikundi na ulawiti kwa binti mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) MT.140105 Clinton Damas, askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Lord Lema na Nickson Jackson.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Agosti 21, 2024 baada ya kesi kuahirishwa, wakili wa washtakiwa, Godfrey Wasonga amesema mtaalamu wa uchunguzi wa mambo ya sayansi ya simu na vifaa vingine vya kielektroniki kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi, aliyemtaja kuwa ni shahidi wa kwanza amekamilisha ushahidi wake leo aliouanza jana Agosti 20. Amesema wao walipata nafasi ya kumuhoji kwa niaba ya washtakiwa.

“Tulikuwa na shahidi mwingine ambaye ni daktari wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambaye alitoa ushahidi na amemaliza kwa maana ya kuulizwa maswali. Shauri hili limeahirishwa hadi kesho (Agosti 22) saa nne asubuhi kwa ajili ya kuendelea kusikiliza mashahidi wengine,” amesema.

Amesema shahidi wa kwanza alimaliza kutoa ushahidi saa tisa alasiri na kuanza wa pili ambaye ni daktari aliyemfanyia vipimo binti huyo, ambaye alimaliza ushahidi saa 12.00 jioni.

Washtakiwa wanatetewa na mawakili wanne katika kesi hiyo inayosikilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Zabibu Mpangule.

Wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kubaka kwa kikundi na kumlawiti binti huyo ambaye katika hati ya mashtaka anatajwa kwa jina la XY. Kesi hiyo inasikilizwa faragha.

Related Posts