Kuanzia Rais Joe Biden, mwenye sauti yenye nishati ya hali ya juu, mpaka Seneta Bernie Sanders, kila kitu kinasherehesha Kongamano la Kitaifa la chama cha Democratic (DNC), kwa ajili ya uteuzi wa mgombea urais.
Agosti 19 – 24, 2024, zimekuwa siku nne zenye kubadili upepo wa kisiasa za Marekani kwa sehemu kubwa. Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris, amefanikiwa kukusanya sauti zenye nguvu, ambazo zinampigia debe kuwa Rais wa 47 wa taifa hilo.
“Wamarekani, nawapenda, lakini ngoja niwaulize, mpo tayari kuchagua kwa ajili ya uhuru? Mpo tayari kuchagua kwa ajili ya demokrasia na Marekani? Ngoja niwaulize, mpo tayari kumchagua Kamala Harris na Tim Walz?” alihoji Biden, akishangiliwa.
Hadhira iliyochangamka, wengi wakiwa na vipeperushi vilivyoandikwa “Tunakupenda Joe” na wachache wakipepea vilivyo na maandishi “Asante Joe”, Rais Biden, alitumia dakika 50, kueleza ni kwa nini Kamala anatosha kuchaguliwa kuwa Rais, katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Novemba 5, 2024.
Turufu kuu ya Biden katika hotuba yake ni mafanikio ambayo ametamba kuyapata kupitia Serikali anayoiongoza; ushindi dhidi ya janga la Covid-19, ambalo lilikuwa linaipigisha magoti Marekani kipindi anaingia madarakani, ukuaji wa uchumi, kudhibiti mfumuko wa bei.
“Ni kwa sababu yenu Wamarekani, tumeweza kuifanya nchi ipige hatua kubwa kupata kutokea. Na ninaposema sisi, namaanisha mimi na Kamala Harris. Covid-19 haitusumbui tena, tumetengeneza ajira 62 milioni, mfumuko wa bei umeshuka na utazidi kushuka,” alizungumza Biden kwa msisitizo.
Mara kwa mara, Biden alilazimika kukatisha hotuba, kupisha shangwe za hadhira, iliyokuwa ikiimba “Tunakupenda Joe”, na alipofulululiza anataja mafanikio ya Serikali anayoiongoza, sauti zilipazwa “Asante Joe”, naye akajibu: “Mumshukuru Kamala pia.”
Kimsingi, Biden alitaka sifa za mafanikio ya Serikali anayoiongoza, ziende pia kwa Kamala, kwa sababu walifanya kazi kama mapacha.
Akasisitiza, alipomteua Kamala kuwa mgombea mwenza wake kuelekea Uchaguzi wa Rais wa Marekani mwaka 2020, ulikuwa uamuzi bora zaidi ambao amewahi kuufanya maishani.
“Tunahitaji uchumi wenye manufaa kwetu sote, siyo kwa mabilionea peke yao,” alisema Sanders akimnadi Kamala. Hotuba ya Sanders aliegemea kwenye hali ambayo taifa la Marekani lilikuwa miaka mitatu na nusu iliyopita, kipindi Biden na Kamala wanakula kiapo kuongoza dola.
“Tulikuwa kwenye mchanganyiko wa mfumo mbovu wa utoaji huduma za afya, kuwahi kutokea ndani ya miaka 100 iliyopita. Tulikuwa kwenye anguko kubwa zaidi la kiuchumi tangu mdororo mkuu wa kiuchumi (mwaka 1929-1939). Wamarekani 3,000 walipoteza maisha kila siku.
“Hospitali zetu zilizidiwa na wagonjwa wa Covid-19. Biashara zilifungwa kila kona ya nchi, ajira ziliyeyuka, shule zilifungwa, watu waliondolewa kwenye nyumba kwa kushindwa kulipa kodi. Wanafunzi Marekani walishinda njaa,” alisema Sanders, Seneta wa Vermont, akitaka watu wakumbuke siyo tu mahali Wamarekani wametolewa na Biden pamoja na Kamala, bali pia wasisahau aliyewaingiza kwenye hali hiyo ni Donald Trump.
Awali, Biden alikuwa awanie urais wa Marekani kwa muhula wa pili. Hata hivyo, Julai 21, 2024, alitoa taarifa ya kujitoa kwenye mbio hizo. Hiyo ilikuwa baada ya kufanya vibaya katika mdahalo dhidi ya Trump, Juni 28, 2024. Democrats wengi walipiga mayowe kutaka Biden akae kando, kupisha mgombea mwingine, wengine walimtetea. Chama cha Democratic, kiliingia kwenye mgawanyiko.
Biden alipotangaza kujitoa, moja kwa moja alimpendekeza Kamala kuwa mgombea urais. Akataka hadi rasilimali zote za kampeni zake, zitumiwe na Kamala kwa sababu walikuwa wakigombea pamoja. Yeye (Biden) urais, Kamala makamu wa rais.
Upepo wa kisiasa ulibadilika haraka. Mwanzoni, kura za maoni zilionesha Kamala asingekuwa tishio dhidi ya Trump. Kuna Democrats waliopaza sauti kutaka Seneta wa zamani wa New York, Hillary Clinton, ndiye angepewa nafasi, maana aligombea urais na Trump mwaka 2016, na alikuwa mwenye nguvu.
“Kamala atavunja dari ya kioo na kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Marekani,” alisema Hillary, akimpigia chapuo Kamala, kwenye hotuba yake ndani ya DNC, iliyosimamisha watu kumpigia makofi (standing ovation). Hillary, alikumbusha mwanzo wa harakati za mwanamke Marekani kuwania urais na kusisitiza kuwa Kamala atatimiza ndoto.
Kuanzia Shirley Chisholm, aliyejitosa kuwania urais Marekani kupitia Democratic mwaka 1972, akiweka rekodi ya mwanamke wa kwanza kuthubutu, kisha Geraldine Ferraro, aliyeteuliwa na Democrats kuwa mgombea mwenza mwaka 1984, akichangia tiketi na Walter Mondale, halafu yeye mwenyewe (Hillary), mwaka 2016, matumaini yote ni kwa Kamala.
“Tunayo nafasi ya kuchagua, kwenda mbele au kurudi nyuma. Kuungana pamoja kama watu wa taifa moja au kugawanyika baina sisi na wao. Kamala ana uhusika wa kutupeleka mbele na kutuunganisha kuwa kitu kimoja. Donald Trump ana rekodi yake ya kuwa mtu wa kwanza kugombea urais akiwa na hatia ya makosa 34 ya uhalifu mkubwa,” alisema Hillary.
Mgombea huyo wa urais kupitia Democratic mwaka 2016, ni mke wa Rais wa 42 wa Marekani, Bill Clinton. Hillary pia alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani mwaka 2009 – 2013.
Kila sauti yenye nguvu ndani ya Democratic, imezungumza kuhusu umuhimu na ulazima wa kumchagua Kamala kuwa mgombea urais dhidi ya Trump. Rais wa 42 wa Marekani, Bill Clinton, aliyetumikia taifa hilo Januari 1993 mpaka Januari 2001, naye amemuunga mkono Kamala.
Bill, pamoja na kupongeza hotuba ya Hillary (mkewe), aliyoisifia kwamba ilikuwa bora, alisema: “Mwaka 2024 kuna chaguo la kufanya, Kamala Harris kwa ajili ya watu na mtu mwingine ambaye amethibitisha kuwa yeye huamini katika ‘mimi, mimi mwenyewe, mimi’.
Kamala Harris atafanya kazi kutatua matatizo yetu, atawezesha kufikia fursa zetu, kupunguza hofu zetu, na kila Mmarekani, vyovyote atakavyopiga kura, atakuwa na nafasi ya kufukuzia ndoto zake.”
Akimchambua Trump, Bill alisema mwanasiasa huyo tajiri ambaye ni Rais wa 45 wa Marekani, bado anaendelea kugawa watu, anazidi kulalamika, anatengeneza fujo, wakati Kamala ana maono, uzoefu, haiba, utashi na furaha ya kuhakikisha mambo yanatokea.
Ukimwacha Trump, Rais mstaafu wa Marekani kutokea chama cha Republican, aliye hai, ni George Bush. Hata hivyo, Bush hakutokea kwenye Kongamano la Kitaifa la Republican (RNC) Julai 15 – 18, 2024, kumuunga mkono Trump. Zaidi, hotuba za kumpigia chapuo Trump, nyingi zilitolewa na wahamasishaji (motivational speakers), vilevile wanasiasa wasio na uzani mkubwa.
DNC, Kamala amemvutia kila mwanasiasa mwenye nguvu kutoka Democratic. Marais wastaafu walio hai kutokea Democratic ni Bill na Barack Obama, ambao wote wametoa hotuba za kumuunga mkono Kamala. Vilevile Biden aliye madarakani, ambaye atastaafu Januari 20, 2025.
“Uchaguzi huu tunayo nafasi ya kumchagua mtu ambaye ametumia maisha yake yote, kujaribu kumpa kila mtu fursa ambayo yeye amepewa na Marekani. Mtu ambaye anakuona, anakusikia, atakayeamka kila siku kukupigania, Rais ajaye wa Marekani, Kamala Harris,” alisema Barack akishangiliwa.
Barack, Rais wa 44 wa Marekani, alitambulishwa jukwaani na mkewe, Michelle Obama, ambaye katika hotuba yake alisema: “Kamala, yupo zaidi ya tayari kwa ajili ya wakati huu. Ni mmoja wa watu wenye sifa za juu kabisa kugombea urais, ni mmoja wa watu adhimu kabisa.”
Jukwaa la DNC 2024, limepambwa na wanasiasa pamoja na watu mashuhuri mbalimbali, mmoja wa waliokuwa kivutio kikubwa ni mume wa Kamala, Douglas Emhoff, aliyesema: “Kamala anapenda kuona watu wapo vizuri, anachukia kuona watu wakishangilia wenzao kufeli. Tamaa yake ni kusaidia watu. Huruma yake ndiyo uimara wake.”
Hali ikiwa hivyo, jarida la Forbes limetoa mkusanyiko wa kura za maoni kati ya Julai 15 – 18, 2024, RNC ilipoketi Fiserv Forum, Milwaukee, na Agosti 19 – 22, DNC, ilipokutana United Centre, Chicago, na kuonesha kwamba Kamala yupo mbele ya Trump kwa asilimia tatu mpaka nne. Hii ni kuonesha kuwa kiwango cha Kamala kukubalika ni kikubwa na chenye kasi.