Mbivu, mbichi dhamana ya Kombo wa Chadema leo

Tanga. Mahakama ya Wilaya ya Tanga leo Alhamisi, Agosti 22, 2024 inatarajiwa kutoa uamuzi wa zuio la dhamana ya mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Tanga, Kombo Mbwana.

Kombo ambaye awali aliripotiwa kupotea kabla ya Jeshi la Polisi Tanga, kutangaza kumshikilia siku 29 baadaye, anakabiliwa na kesi ya jinai mahakamani hapo akidaiwa kutumia vifaa vya mawasiliano ikiwemo kadi ya simu ya mkononi isiyosajiliwa na bila kutoa taarifa.

Ingawa mashtaka yanayomkabili yanadhaminika kwa mujibu wa sheria, lakini amekuwa mahabusu kwa siku 37 sasa tangu alipopandishwa kizimbani kutoakana na hatua ya Jeshi la Polisi Tanga kupitia kiapo cha Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Tanga (RCO) kuomba asipewe dhamana.

Maombi hayo ya zuio la dhamana yake yalisikilizwa pande zote  Agosti 12, 2024 na Hakimu Mkazi Mfawidhi, anayesikiliza kesi hiyo, Moses Maroa, ambaye alipanga kutoa uamuzi wake leo.

Uamuzi huo ndio utakaoamua hatima ya uhuru wake kwamba ama utamfanya arejee uraiani au kuendelea kusota mahabusu.

Kombo alipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Julai 16, 2024, na kusomewa mashtaka hayo, ambayo hata hivyo aliyakana.

Mahakama ilisema dhamana yake ilikuwa wazi kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh2 milioni kila mmoja, wenye barua ya mtendaji wa mtaa wanakokaa pamoja na vitambulisho vya Taifa (Nida).

Hata hivyo, alipelekwa mahabusu kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana baada ya kukosa wadhamini kwa kuwa ndugu zake hawakuwa na taarifa wakati anapandishwa kizimbani.

Julai 30, 2024 siku ambayo kesi hiyo ilitajwa, mawakili na ndugu zake walifika mahakamani hapo wakiwa wamejiandaa kukamilisha masharti hayo ya dhamana wakitarajia kuondoka naye.

Hata hivyo, dhamana yake iliyeyuka baada ya RCO Tanga kuwasilisha mahakamani kiapo cha cha kuzuia dhamana hiyo kwa maelezo bado wanaendelea na upelelezi na kwamba wanatarajia kuwaongeza washtakiwa wengine katika kesi hiyo, ambao wako katika maneo mbalimbali nchini

Mawakili wa mshtakiwa huyo waliokuwepo siku hiyo, Deogratius Mahinyila na Michael Rugina walipinga kuwepo kwa kiapo hicho kuwa kiko kinyume na utaratibu wa kisheria na kwamba RCO hana mamlaka hayo ya kuzuia dhamana, tena Mahakama ikiwa imeshatoa uamuzi wa masharti ya dhamana.

Hata hivyo, Hakimu Maroa aliamua kutengua amri ya masharti ya dhamana na akapanga kusikiliza maombi hayo ya polisi ya zuio la dhamana Agosti 22.

Pia Hakimu Maroa aliutaka upande wa utetezi kuwasilisha kiapo kinzani kujibu kiapo hicho cha RCO kabla ya leo, yaani tarehe iliyopangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa zuio hilo.

Siku hiyo maombi hayo yaliposikilizwa upande wa mashtaka ulidai RCO anataka mshtakiwa asipewe dhamana kwa kuwa anaweza kuingilia upelelezi ambao bado unaendelea.

Mawakili wa Kombo walipinga hoja hiyo wakidai dhamana ni haki ya mshtakiwa na mashtaka yanayomkabili yanadhaminika.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote ndipo Hakimu Maroa akapanga kutoa uamuzi leo Alhamisi.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 19759 ya mwaka 2024, Kombo anakabiliwa na mashtaka matatu chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta.

Katika shtaka la kwanza anadaiwa kushindwa kutoa taarifa za kutosha za akaunti ya kadi yake ya simu, kinyume na kifungu cha 126 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta.

Anadaiwa Julai 9, 2024 katika mtaa wa Hassan Ngwilizi wilayani na mkoani Tanga, alikutwa akimiliki laini (kadi ya simu) ya Tigo yenye namba (ICCID) 8925502042093621824, iliyosajiliwa kwa jina la Shukru Kahawa na kushindwa kutoa maelezo ya kutosha kuhusu umiliki wa laini hiyo.

Pia anadaiwa kushindwa kusajili laini ya simu ambayo awali ilikuwa inamilikiwa na mtu mwingine, na kushindwa kuripoti kuhusu mabadiliko ya laini ya simu.

Kombo alitoweka tangu Juni 15, 2024, baada ya kuchukuliwa na watu  wasiojulikana nyumbani kwake kijiji cha Kwamsala, wilayani Handeni, mkoani Tanga na kupelekwa mahali ambako hata ndugu zake hawakupafahamu.

Julai 14, 2024, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Zakaria Bernard alipotangaza kuwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma hizo, ndipo Julai 16 akapandiahwa kizimbani.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa mbalimbali

Related Posts