Mukwala afichua siri Simba | Mwanaspoti

MSHAMBULIAJI mpya wa Simba, Mganda Steven Mukwala hajawapa furaha Wanamsimbazi, lakini mwenyewe amekiri sasa anauona ukubwa na thamani ya kikosi hicho baada ya kuanza kukitumikia tangu ajiunge msimu huu akitokea Asante Kotoko ya Ghana.

Mukwala alisema tangu atue nchini amekutana na presha kubwa kuanzia katika benchi la ufundi hadi kwa mashabiki, jambo ambalo ni tofauti na baadhi ya klabu alizochezea ingawa anaendelea kuzoea mazingira.

“Kila mmoja anaweza kuongea kadri anavyoweza kwa sababu huwezi kuzuia hilo. Natambua bado nina deni kubwa la kufanya ndani ya timu hii ili kufikia malengo, hivyo siwezi kusikiliza maneno ya watu kutokana na kutofanya vizuri,” alisema Mukwala.

Nyota huyo aliongeza, jambo kubwa linalompa matumaini makubwa ya kufanya vizuri msimu huu ni kutokana na imani kubwa ya kucheza anayoendelea kupewa na benchi lao la ufundi la timu hiyo, chini ya kocha mkuu wa kikosi hicho, Fadlu Davids.

“Mashabiki siku zote wanapenda mambo mazuri na siwezi kuwaahidi jambo lolote zaidi ya kuomba ushirikiano wao, suala la kutofunga natambua linawaumiza wengi, ila nalichukulia kama changamoto ambayo inanifanya nipambane zaidi ya sasa,” alisema.

Katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu ambao Simba ilishinda kwa mabao 3-0, dhidi ya Tabora United Agosti 18, kocha wa timu hiyo Fadlu Davids alisema, sio suala la siku moja kuwaunganisha wachezaji ila kuna maendelezo mazuri kikosini kwake.

Mukwala ametua huku akikumbukwa zaidi msimu uliopita ambapo alifunga mabao 14 akiwa na Asante Kotoko nyuma ya kinara mshambuliaji wa Berekum Chelsea, Stephen Amankonah aliyefunga mabao 16.

Pia aliibuka mchezaji bora wa Ligi ya Ghana Desemba mwaka jana akiwa na kikosi hicho cha Asante Kotoko aliyojiunga nayo Agosti 2022 akitokea Klabu ya URA ya kwao Uganda na katika msimu wake wa kwanza alifunga mabao 11 na kutoa asisti tano.

Akiwa URA, Mukwala alicheza kwa misimu mitatu kuanzia mwaka 2020 ambapo msimu wa kwanza 2019/2020 aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Uganda akifunga mabao 13 na msimu wa 2020/2021, akafunga 14 kisha 2021/2022 akatupia tena kambani mabao 13.  Mukwala anakumbana na presha hasa baada ya uhamisho wa mshambuliaji mpya raia wa Cameroon, Leonel Ateba ambaye bado hajaanza kucheza tangu ajiunge na kikosi hicho msimu huu kufuatia kuachana na USM Alger ya Algeria.

Ateba alijiunga na USM Alger Januari mwaka huu akitokea Dynamo Douala ya Cameroon.

Related Posts