SIMBA imecheza mechi tatu tu za mashindano msimu huu ambazo mbili ni za Ngao ya Jamii ilizokutana na Yanga na Coastal Union na moja ya Ligi dhidi ya Tabora United.
Katika mechi hizo tatu, imeibuka na ushindi mara mbili ambazo ni dhidi ya Coastal kwa bao 1-0 na dhidi ya Tabora United kwa mabao 3-0 na ilipoteza mbele ya Yanga kwa bao 1-0.
Kabla ya hapo ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya APR katika mechi ya kilele cha Tamasha la Simba Day.
Hata hivyo, baada ya hizo mechi, kuna mashabiki wa Simba wamesikika wakiwabeza baadhi ya wachezaji ambao wamesajiliwa hivi karibuni hasa wa kigeni wakidai uwezo wao ni mdogo na hawawezi kuipa mafanikio Simba.
Katika hili nadhani mashabiki wa Simba wanatumia vibaya wajibu wao wa kukosoa wachezaji wao kwa vile hadi sasa timu yao haijafanya vibaya hadi kufikia hatua waanze kuwaona wachezaji hao hawana mchango kwa timu.
Timu yao inajengwa upya na wachezaji wengi ni wapya pamoja na kocha wao na ukiangalia muda ambao wamekaa pamoja haujafika hata miezi miwili hivyo katika hali ya kawaida timu haiwezi kuwa na ubora huo wanaoutaka na hata wachezaji wote hawawezi kuwa na ubora wa hali ya juu.
Wapo wachezaji ambao wanaposajiliwa kwenye timu huwa wanahitaji kupata muda wa kuweza kuzoea na kumudu mazingira mapya hivyo kipindi hicho cha mpito hawawezi kuwa katika kiwango kile ambacho mashabiki wanakihitaji.
Ninachokiona ni, watu wengi wa Simba wameingia katika mtego wa Yanga ambayo timu yao tayari ina ubora na wanawaaminisha kuwa Simba inapaswa kuwa levo yao na wachezaji ilionao hawana uwezo wa kuwafikia.
Presha hii inawapanda kichwani na kuwafanya washindwe kuridhika na kile wanachokipata hivyo matokeo yake wanahamishia kuwabebesha lawama wachezaji wao kuwa hawachezi vizuri.
Hakuna timu inayojengwa ndani ya mwezi mmoja au miwili hivyo mashabiki wa Simba wanapaswa kulizingatia hilo na kuwaunga mkono wachezaji wao vinginevyo watajitoa kwenye mstari.