WATOTO wa marehemu Zacharia Hans Poppe, wanakusudia kuwasilisha mahakamani maombi mengine ya ama kuziunganisha kampuni tatu zinazomilikiwa na baba yao mzazi ili ziweze kuwa sehemu ya wadaiwa katika kesi ya mirathi au wachukue hatua zingine katika mahakama nyingine.
Watoto hao, Angel na Abel ambao ni wasimamizi wa mirathi, katika kesi ya mirathi ya Zacharia HansPoppe namba 177/2022, iliyopo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia(IJC) Temeke, wanakusudia kufanya hivyo, baada ya maombi yao ya awali kugonga mwamba mahakamani hapo.
Kupitia wakili wao, Emmanuel Msengezi na Regina Helman walidai watawasilisha maombi mengine mahakamani hapo ya kuziunganisha kampuni hizo tatu ambazo ni Z.H. P Ltd, HansPoppe Hotels Ltd na Z.H.Poppe Limited ili ziwe sehemu wadaawa katika shauri hilo.
Alidai lengo la kufanya hivyo ni kumpa Mamlaka Jaji Glady’s Nancy Barthy anayesikiliza shauri hilo, aweze kutoa amri ambazo walikuwa wameziomba ili Wakurugenzi wa kampuni hizo wapeleke mahakamani taarifa za fedha pamoja na mikataba mbalimbali ya pango na mambo mengine yanayohusu kampuni hizo.
Wakili Msengezi ametoa maelezo hayo jana, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi katika maombi madogo ya awali yaliyowasilishwa mahakamani hapo na watoto hao wa Zacharia Hans Poppe kupitia mawakili hao.
Katika maombi hayo, wakili Msengezi aliomba mahakama itoa amri ya kwa Wakurugenzi Watendaji wa Kampuni ya Z. H. Poppe Limited, Z.H. P Ltd na HansPoppe Hotels Ltd, ambao ni; Caeser Hans Poppe na mwanae Adam Caeser HansPoppe, wawasilishe nyaraka mbalimbali za mikopo waliyochukua kwenye taasisi za fedha kupitia kampuni hizo mpaka sasa, taarifa ya fedha ikiwemo faida ya mwaka kwa kampuni hizo, mikataba ya kusafirisha mafuta nje ya nchi pamoja na mikataba ya upangishaji wa hoteli ya Zacharia Hans Poppe iliyopo Iringa.
Caeser ni mdogo wake, Zacharia Hans Poppe aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba na Adamu ni mtoto wa Caeser ambao kwa pamoja ni Wakurugenzi katika kampuni ya Z. H. Poppe Ltd inayomilikiwa Zacharia kwa asilimia 90 ya hisa zote.
Hata hivyo, mahakama hiyo baada ya kupitia maombi hayo ilisema kuwa itakuwa ni vigumu kutoa amri hizo kwa kuwa kampuni hizo sio sehemu ya kesi ya mirathi iliyopo mbele yake.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Barthy alisema hawezi kutoa uamuzi dhidi ya kampuni ambayo haipo na haijaunganishwa kama sehemu ya wadaawa mahakamani hapo.
“Itakuwa ni vigumu kutoa amri hizo na uamuzi dhidi ya kampuni ambayo haipo katika shauri hili na wala haijaunganishwa kama sehemu ya wadaawa(walalamikiwa) katika shauri hili la mirathi” alisema jaji Barthy na kuongeza;
“Lakini ikiwa Angel na Abel wana Interest(maslahi )wanaweza kuchukua hatua zingine ikiwemo kuziunganisha kampuni hizo katika kesi hii au kwenda katika jukwaa lingine.”
Kuhusu ombi la kuongeza au kupungeza orodha ya idadi ya mali za marehemu, jaji Barthy alisema amri hiyo haijaondolea wala kulifuta na bali ipo palepale kwa ajili ya utekelezwaji.
Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, wakili Msengezi aliieleza mahakama hiyo kuwa wanakusudia kuwasilisha maombi yao ya kuziunganisha kampuni hizo tatu.
‘Mheshimiwa jaji, baada ya uamuzi wako, tunakusudia kuwasilisha maombi ya kuziunganisha kampuni zote tatu zilizokuwa zinamilikiwa na marehemu Zacharia Hans Poppe ili ziweze kuwa sehemu ya wadaawa katika shauri hili ili jaji uwe na mamlaka na kampuni hizi kwa zitakuwa zimeunganishwa kama wadaawa na hivyo utaweza kutoa amri ambazo tulikuwa tumeziomba za wao kuleta taarifa za fedha, mikabata mbalimbali ya mapango (upangishaji) na mambo mengine” alidai wakili Msengezi na kuongeza
‘Na kwa kuwa milango haijafungwa kwa Abel na Angel kwa kuchukua hatua zaidi ama kwenye shauri hili la mirathi au kwenye mahakama nyingineyo, wakiweza kuzipeleka kampuni hizi pekee bila kuhusisha na kesi hii ya mirathi wanaweza kwa sababu wana mamlaka hayo na kama wasimamizi wa mirathi ya Zacharia Hans Poppe, wanaweza kuipeleka kampuni makamani kumlazimisha mkuregenzi aliyopo alete vitu hivyo mahakamani,” aliodai wakili Msengezi.
Baada ya upande wa waleta maombi kutoa maelezo hayo, wakili wa Peter Kibatala akisaidiana na Glory Ulomi ambao wanawatetea wadaawa katika shauri hilo ambao ni Caeser na mwanae Adam Caeser, waliondoa maombi yao waliyokuwa wamewasilisha mahakamani hapo Julai 23, 2024 ya kuweka pingamizi kuwa mahakama hiyo isitoa amri kwa kampuni hizo kwa sababu hazijawekwa kuwa ni moja ya wadaawa katika shauri hilo.
“Mheshimiwa jaji, tunaomba kuondoa maombi yetu tuliyowasilisha mahakama hapa, kwani tumeona uamuzi uliyoutoa umeenda moja kwa moja kutoa amri kwa kile tulichokuwa tunaomba kwamba, mahakama yako isitoa amri yoyote dhidi ya kampuni kwa sio sehemu yah ii esi na wala haijaunganishwa kwenye kesi hii ili iweze kusikilizwa,” alidai Kibatala.
Jaji Barthy, baada ya kusikiliza hoja za pande zote alikubaliana na waleta maombi na wajibu maombi na kuahirisha kesi hadi Septemba 12, 2024 kwa ajili ya amri nyingine.
Kesi hiyo ya mirathi ya marehemu Hansppoe, namba 177 ya mwaka 2022 imefunguliwa katika mahakama hiyo na wasimamizi wa mirathi, wakiomba wakurugenzi wa kampuni hizo zinazomilikiwa na Zacharia Hans Poppe wawasilishe orodha ya mali zilizopo katika kampuni hizo.
Waombaji hao waliwasilisha maombi, wakiomba kusomewa orodha ya mali iliyokusanywa na kutoa taarifa ya hesabu ya fedha tangu baba yao alipofariki hadi sasa.
Vile vile wanaiomba Mahakama hiyo ielekeze wakurugenzi hao waeleze hali ya mali za marehemu Zacharia zilizopo katika kampuni zake ikiwemo taarifa ya mapato na matumizi.
Zacharia HansPoppe alifariki dunia Septemba 10, 2021 katika Hospitali ya Aga Khan alikokuwa akipatiwa matibabu na mazishi yake yalifanyika Septemba 15, 2021 mkoani Iringa.
Hans Poppe alikuwa mwanachama kindakindaki wa klabu ya wekundu wa Msimbazi na atakumbukwa na wanachama kwa kuleta mafanikio makubwa ndani ya klabu ya Simba, kwa uhamasishaji aliofanya baada ya kuteuliwa pia kuwa mwenyekiti wa kundi la marafiki wa Simba ‘ Friend of Simba’ ambapo kundi hilo lilijizolea umaarufu mkubwa ndani ya klabu hiyo.