Majaliwa: Suluhu Sports Academy itasaidia vijana kuonyesha vipaji

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Ujenzi wa Suluhu Sports Akademi utasaidia kujenga mfumo wa kuwaandaa vijana kucheza michezo mbalimbali.

Majaliwa ameyasema hayo Zanzibar leo, Agosti 22,2024 kwenye hafla ya kuweka Jiwe la Msingi kwenye kitu hicho kinachojengwa Mkunguni- Kizimkazi Zanzibar huku mgeni rasmi akiwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Majaliwa amesema changamoto hiyo ni ya muda mrefu lakini Rais kuamua kujenga kiwanja hicho itasaidia vijana wenye umri mbalimbali kuonesha vipaji vyao na kuja kulitumikia taifa baadaye.

“Tunatambua tulikotoka tulianza kwa kusuasua kwenye mitaala yetu ya elimu awali tulikuwa na michezo baadaye mtu mmoja akaja akaondoa michezo kwenye mitaala kwa kipindi cha miaka 15 bila mtaala kusema michezo kiwango chetu kilishuka,” amesema.

Amesema amekuwa akisimamia michezo kwenye shule na imekuwa ikifanyika ikiwemo Umishumta huku akitumia fursa hiyo kuwapongeza walioanzisha vituo vya michezo.

Kwa upande wake, Waziri wa Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Maulid Mwita amesema wanatarajia mwaka 2027 Zanzibar itakuwa miongoni mwa waandaaji wa michuano ya Kombe la Mataifa ya  Afrika (Afcon).

“Kabla ya hapo Februari mwakani tunatarajia kuandaa mashindani ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani maarufu kama (Chan), kwa maana ya upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.

“Nikuambie uwanja wetu wa Amaan umekubalika kutumika kitu kilichobakia ni kimoja kubadilisha nyasi kutoka zile za bandia na kuweka nyasi asili na Rais wa Zanzibar amekubali kubadili ili mashindano yafanyike,” amesema.

Amesema wataendelea kufanya kazi usiku na mchana kwa kuhakikisha wanajenga miundombinu ili vijana wapate sehemu za kuonyesha vipaji vyao.

“Kwa kuzingatia hilo kule mjini tumeweka utaratibu wa vijana kushiriki michezo kwenye viwanja bure lakini kukamilika kwa Suluhu Academy litakuwa jambo jema na vijana kuchukuliwa na timu mbalimbali,” amesema.

Related Posts