Wadau walia masharti elimu kwa mpigakura, Serikali yajibu

Dar es Salaam. Wingi na ugumu wa masharti kwa asasi za kiraia kuomba kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vimeibua hofu kwa wadau, wakisema kuna nia ya siri ya Serikali kuwadhibiti wasiifanye kazi hiyo.

Wadau hao kutoka asasi za kiraia, wamekwenda mbali zaidi na kufananisha wingi na ugumu wa masharti yaliyowekwa na ule msemo wa ‘akufukuzaye hakwambii toka.’

Serikali inaweka mazingira hayo, ilhali Tanzania ina historia ya idadi ndogo ya wananchi wanaojitokeza kupiga kura katika chaguzi kadhaa za hivi karibuni.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, watu milioni 14.8 hawakujitokeza kupiga kura, sawa na asilimia 49.8 ya wapiga kura wote, kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo kwa sasa ni Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Hali kama hiyo ilijitokeza pia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ambapo kati ya wananchi milioni 25.5 waliojiandikisha asilimia 33 hawakujitokeza kupiga kura.

Wakati wadau wakiwa na shaka hiyo, Mwananchi lilipomtafuta Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa simu yake iliita bila majibu.

Hali ilikuwa hivyo, hata alipotafutwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Adolf Ndunguru, lakini Mkuu wa Mawasiliano Serikalini wa Wizara hiyo, Nteghenjwa Hosseah alipoulizwa kupitia mtandao wa WhatsApp, alisema hawajaweka masharti.

“Kwanza hatujaweka masharti. Tumeweka aina ya nyaraka ambazo taasisi inapaswa kuwasilisha wakati wa maombi. Nyaraka zilizowekwa ni nyaraka za kawaida na ambazo taasisi yoyote inakuwa nazo wakati wowote,” amesema.

Katika tangazo lililotolewa na Tamisemi wiki iliyopita, taasisi itakayoomba kutoa elimu ya umma inatakiwa kuambatanisha nyaraka ambazo ni cheti cha usajili, katiba yake, anuani ya makazi na namba za simu.

Pia taarifa ya rasilimali watu na vitendea kazi, vibali vya kazi na ukaazi endapo taasisi ina wafanyakazi wasio Watanzania na barua ya kutoka kwa msajili kuthibitisha uhai wa taasisi.

Nyaraka zingine ni za majina, wasifu, namba za simu na uthibitisho wa uraia wa viongozi wa juu wa taasisi, taarifa ya fedha ya miaka mitatu ikionyesha vyanzo vya fedha, na taarifa ya utendaji kazi na taarifa ya wadau au washirika wa karibu.

Akizungumzia hilo, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa amesema wingi wa masharti hayo unaweka ugumu kwa taasisi kuifanya kazi hiyo.

Ametaja baadhi ya masharti kama kuwasilisha cheti cha taasisi kadhalika barua ya msajili wa taasisi, akisema lilipaswa kuwepo sharti moja.

“Cheti kinathibitisha uwepo wa taasisi tena wanakutaka uwasilishe na barua ya msajili ya nini,” ameeleza.

Hata hivyo, sharti linalotaka kuwasilisha barua ya msajili, limefafanuliwa katika tangazo hilo kuwa, linalenga kuthibitisha uhai wa taasisi.

Sharti lingine alilolitaja kuwa gumu ni uthibitisho wa uraia wa viongozi wa taasisi, akisema si jukumu la mwenye taasisi kuthibitisha hilo.

Amesema uthibitisho wa uraia wa raia yeyote hufanywa na Idara ya Uhamiaji, hivyo ni jambo linaloweka ugumu pia.

“Masharti yanakuwa mengi na yanaweza kufanya asasi za kiraia zisiende kuomba. Wangejaribu kuweka utaratibu kama unaotumika na tume ambao masharti yake yanakuwa nafuu,” amesema.

Hata hivyo, ameeleza taasisi nyingi hazina taarifa ya fedha za miaka mitatu na kwamba sharti hilo linawanyima haki hiyo wale waliosajiliwa hivi karibuni.

Ameeleza kilichofanywa mwaka huu kinafanana na kile cha mwaka 2020 na kusababisha asasi nyingi za kiraia zishindwe kutekeleza wajibu huo.

Amependekeza kupunguzwa masharti yabaki matano na hasa yake ya msingi kama rasilimali watu, cheti, anuani ya makazi, vibali vya kazi kwa waajiriwa wasio raia na taarifa ya utendaji.

Mkurugenzi wa Youth Partnership Countrywide, Israel Ilunde aliyafananisha masharti hayo na kile alichoeleza, sawa na mtu anayekualika kwenye harusi yake lakini anakutaka uchangie kiwango kilicho nje ya uwezo wako.

“Ukiona mtu anakualika kuchangia harusi anaweka kiwango kikubwa, ujue huyo mtu ana watu wake au anakufukuza hataki wewe masikini achangie harusi yake,” amesema.

Masharti hayo, amesema ni mengi na yanaashiria ama nchi imerudi katika enzi za kutoaminiana au ina shaka na wadau wake.

“Nafikiri tunatakiwa tuaminiane, waweke masharti ya kawaida. Likiwa limetokea janga linalohitaji ushiriki wa pamoja wasingeweka masharti mengi kama hayo,” amesisitiza.

Ameishi Serikali ipunguze masharti hayo ili kutoa mwanya kwa wadau wengi kushiriki kutoa elimu ya mpiga kura.

“Serikali iwaamini wananchi ili tushirikiane kuwahamasisha wananchi washiriki kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa,” amesema.

Related Posts