Mkanwa amrithi Josiah Biashara Utd

KLABU ya Biashara United ya Mara imeingia makubaliano ya msimu mmoja na Henry Mkanwa kuwa kocha mkuu wa timu hiyo kwa msimu ujao wa Ligi ya Championship, huku akiwa na kibarua cha kuipandisha daraja kwenda Ligi Kuu baada ya kukwama msiimu uliopita.

Kocha huyo wa zamani wa Tabora United, Usalama FC na Polisi Mara anachukua mikoba ya Amani Josiah na wasaidizi wake, Edna Lema na Ivo Maunda waliomaliza mikataba yao, huku Josiah akitimkia Geita Gold na Edna Lema akitua Yanga Princess.

Mbali na Mkanwa, Biashara United imeimarisha benchi lake la ufundi ambapo Mkanwa atasaidiwa na Mussa Said, huku kocha wa viungo (fitness coach) akiwa ni Masoud Ally na daktari wa timu ni Revina Renatus.

Klabu hiyo iliyokuwa imefungiwa kufanya usajili na Shhirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) imeondolewa marufuku hiyo Agosti 15, mwaka huu baada ya kukamilisha masharti kwa kumlipa mchezaji aliyekuwa anaidai Tayo Odongo raia wa Uganda.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mjumbe wa Kamati tendaji ya klabu hiyo, Agustine Mgendi alisema usajili wao ulikuwa umekamilika na kilichokuwa kinasubiriwa ni kuondolewa marufuku hiyo ili kuwaingiza wachezaji wappya kwenye mfumo.

“Kocha mkuu tayari yupo msaidizi wake yupo njiani anakuja kila kitu kiko sawa, Kocha Mkuu ni Henry Mkanwa alikuwa Tabora United msimu uliopita na msaidizi wake ni Mussa Said na tumewapa mkataba wa msimu mmoja tukiwa na lengo la kuipandisha timu.

“Timu iko kambini inaendelea na mazoezi tunaendelea na ujenzi wa timu kila kitu kipo kinaendelea, tunaendelea kuiandaa timu yetu kwa kucheza mechi za kirafiki wiki iliyopita tulikuwa Rorya tukacheza na kombaini ya hapo tukashinda 3-2 Jumamosi tutakuwa Serengeti,” alisema Mgendi

Related Posts