Morogoro. Mratibu wa Elimu, Kata ya Tomondo aliyetambuliwa kwa jina la Mwenge Mnune, amefariki dunia baada ya kuungua kwa moto shambani kwake , wakati akijaribu kuuzima moto huo alioukuta ukiteketeza mazao kwenye shamba hilo.
Tukio hilo linadaiwa kutokea Agosti 21, 2024 katika kitongoji cha Banzayage kilichopo katika kata ya Kiroka, mkoani Morogoro ambapo Mnuna na mkewe walikwenda kutembelea shamba lao na kukuta moto ukiteketeza mazao.
Akizungumzia tukio hilo, mwenyekiti wa kitongoji Banzayage, Abdallah Shabani amesema Mnune alianza kupambana kuuzima moto huo, hata hivyo moto ulimzidi nguvu na kumuunguza mwili wake.
“Baada ya kuona moto unateketeza mazao yake, aliweka pikipiki yake n’gambo ya shamba na kuanza kuuzima, hata hivyo moto ulizidi kuwaka, hivyo ulimshinda nguvu na alipojaribu kukimbia, alianguka na kushindwa kutoka na baadaye moto kushika mwilini mwake,” amesema Shabani.
Amesema alipokea taarifa za tukio hilo saa 2:15 usiku, hata hivyo wananchi walianza kumtafuta tangu saa 8 baada ya moto kuzimika wenyewe na ilipofika alfajili ya leo Agosti 22, 2024, mwili wa mratibu huyo ulikutwa ndani ya shamba hilo ukiwa umeteketea kwa moto.
Mwenyekiti huyo amesema moto huo uliosababisha kifo cha mratibu huyo, pia, umeteketeza mazao yaliyokuwemo kwenye shamba hilo ambayo ni miembe, minazi na migomba, hata hivyo hadi sasa haijajulikana nani aliyewasha moto huo.
Amesema tayari Jeshi la Polisi na viongozi wengine wa kata wamefika eneo la tukio kwa ajili ya kuchukua mwili na kwenda kuuhifadhi katika chumba cha kuhifadhia maiti, hospitali ya rufaa Mkoa wa Morogoro huku taratibu zingine zikiendelea.
“Hili shamba liko mbali na makazi ya watu na huyu mratibu amekuwa akija kukagua mazao yake, yeye mwenyewe anaishi Bigwa Manispaa ya Morogoro na anafanya kazi kata ya Tomondo,” amesema Shabani.
Mmoja wa watu waliofanya kazi na marehemu ni diwani wa zamani wa kata ya Kiloka, Robert Selasela ambaye amesema kabla ya kuwa mratibu wa elimu kata ya Tomondo, Mnune alikuwa mwalimu mkuu shule ya msingi Bamba iliyopo kata ya Kiroka na alifika shuleni hapo miaka ya 1990.
Selasela amesema baadaye Mnune alihama na kwenda kata ya Tomondo kama mratibu wa elimu wa kata hiyo hata hivyo akiwa Kiroka aliweza kufanya shughuli za kilimo na ufugaji na aliweza kuwa na mashamba yenye mazao tofauti.
Amesema Mnune alikuwa mwalimu mahili wa somo la hisabati na pia alikuwa mpenzi wa michezo hivyo aliweza kupata umaarufu kupitia vipaji vyake hivyo.
Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema bado hajapata taarifa za tukio hilo.
“Mwandishi kiukweli bado sijapata taarifa lakini nafikiri watu wa Zimamoto na Uokoaji wanaweza wakawa na taarifa, hebu watafute wakati nami nafuatilia kwa karibu, nitakapopata taarifa nitakujulisha,” amesema Kamanda Mkama.
Mwananchi limemtafuta Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Daniel Myalla ambaye naye amesema taarifa za tukio hilo bado hazijafika ofisini kwake, hata hivyo ameahidi kuzifuatilia.