Aliyekuwa winga wa Simba, Aubin Kramo amejiunga na klabu ya Olimpique Zouia inayoshiriki Ligi Kuu Libya kwa mkataba wa mwaka mmoja, Mwanaspoti limethibitisha.
Usajili huo wa Kramo, umefanya kuwa mchezaji wa pili kutoka Simba kujiunga na klabu za Ligi Kuu Libya baada ya awali mshambuliaji Mcameroon Willy Onana kujiunga na Al Hilal SC ya nchini humo katika dirisha hili la uhamisho.
Kramo alisainiwa na Simba msimu mmoja uliopita akitokea Asec Mimosas lakini hakuwahi kuichezea timu hiyo mechi yoyote ya mashindano rasmi kutokana na kuandamwa na majeraha msimu mzima.
Akizungumza na Mwanaspoti, Licha ya kutoweka wazi dili hilo kukamilika, Kramo amesema lolote linaweza kutokea katika dirisha hili la usajili.
“Taarifa hizo bado hazijawa rasmi hivyo tusubiri kuona itakuwaje kwani lolote linaweza kutokea na nitakujuza,” alisema Kramo.
Hata hivyo pamoja na kutokuthibitishwa Mwanaspoti lina picha zikionesha mchezaji huyo akisaini mkataba na klabu hiyo.
Picha kwa hisani ya @mickyjr