Kamati ya bunge yaimwagia sifa wizara ya maji kwa ubunifu wa hatifungani ya tanga UWASA

Kamati ya Kudumu ya Bunge Maji na Mazingira ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe Jackson Kiswaga Mbunge wa Jimbo la Kalenga Leo 22.08.2024 Dodoma katika kikao chake imetoa pongezi kwa Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa H. Aweso (Mb) na Mejeniment ya Wizara ya Maji kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (TANGA UWASA) kwa kufanikisha ubunifu na uuzaji wa Hatifungani ya Kijani ya TANGA UWASA.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa TANGA UWASA, Mhandisi Geofrey Hilly amefafanua kuwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (TANGA UWASA) katika kuendelea kuboresha huduma zake kwa jamii imeendelea kubuni na kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo utekelezaji wa mradi wa kuboresha miundombinu ya maji Tanga kupitia uuzaji wa Hatifungani, ambao umetoa fursa kwa jamii kushiriki katika uwekezaji kupitia ununuzi wa hisa (bonds) hivyo kufanikisha upatikanaji wa fedha zitakazotumika katika utekelezaji wa mradi huo.

Aidha, Mradi huu unathamani ya Shilingi za Kitanzania Bilioni 53.12 na utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mapema mwaka huu ambapo unalenga kutekeleza yafuatayo;
Moja, Kuboresha miundombinu katika kituo cha kuzalisha na kusambaza Maji cha Mowe, pili, kuboresha Miundombinu ya mabomba ya kusambazia Maji katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Tanga, Mji wa Muheza, Pangani na Mkinga, Tatu, Kufunga Mita za Malipo ya kabla (Smart Prepaid Water meters) kwa wateja 10,000 na Nne, kuendeleza jitihada za utunzaji wa vyanzo vya maji., alisema Mhandisi. Hilly.

Mapema mwezi Februari, 2024 Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdor Mpango alizundua rasmi Dirisha la uuzaji wa Hatifungani ya Kijani ya TANGA UWASA, ambapo makusanyo ya mauzo hayo yalizidi lengo kwa asilimia 103 ambapo TANGA UWASA ilifanikiwa kukusanya Shilingi za Kitanzania Bilioni 54.72 ambapo lengo halisia lilikuwa ni kukusanya Shilingi Bilioni 53.12.

Related Posts