Jinsi wanasiasa watakavyofanikisha uchaguzi wa Serikali za mitaa

Dodoma. Uchaguzi wa Serikali za mitaa uliopangwa kufanyika Novemba 27, 2024 nchini unatoa fursa muhimu kwa viongozi wa vyama vya siasa kuhakikisha mchakato unafanyika kwa amani na utulivu. 
Kwa kuhakikisha uchaguzi huu unakuwa wa haki na uwazi, viongozi wa vyama vya siasa wana jukumu la kuongoza na kudhibiti mchakato huu kwa njia yenye kujali masilahi ya wananchi na maendeleo ya nchi. 
Mbinu na hatua zinazoweza kutumiwa na viongozi wa vyama vya siasa, ili kufanikisha uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa amani na utulivu ni ushirikiano na mawasiliano ya wazi.
Viongozi wa vyama vya siasa wanapaswa kuanzisha na kudumisha ushirikiano mzuri na wadau wote wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), mashirika ya kiraia, na wawakilishi wa Serikali. 
Mawasiliano ya wazi na ya mara kwa mara yatasaidia kupunguza kutokuelewana na migogoro inayoweza kutokea. 
Kila chama kinapaswa kushirikiana na wadau wengine kutoa maoni na mapendekezo juu ya taratibu za uchaguzi na kuhakikisha kuwa haki za wagombea zinaheshimiwa.
Pia, katika kufanikisha uchaguzi kwa amani kunahitaji elimu na mafunzo kwa wanachama wa vyama vya siasa na wagombea. 
Viongozi wanapaswa kutoa mafunzo kuhusu sheria na kanuni za uchaguzi, taratibu za kampeni, na haki na wajibu wa wagombea. 
Hii itasaidia kupunguza migogoro na kutokuelewana wakati wa kampeni na uchaguzi wenyewe. 
Kwa mfano, wagombea wanatakiwa kufahamu taratibu za kuwasilisha malalamiko na kupinga matokeo kwa njia ya kisheria, badala ya kutumia vurugu.
Pia, viongozi wa vyama vya siasa wanapaswa kuchukua hatua madhubuti kudhibiti vurugu na mapigano yanayoweza kutokea wakati wa kampeni na siku ya uchaguzi. 
Hii inajumuisha kuzuia vikundi vya vijana au wanachama wa chama wenye maelekeo ya vurugu, pamoja na kutoa mwongozo wa kisheria na kimaadili kwa wanachama wao. 
Viongozi wanapaswa kuhakikisha maelekezo ya kisheria na kanuni yanatekelezwa kwa ukamilifu na kwamba, hakuna atakayekubaliwa kufanya vitendo vya vurugu.
Pia, viongozi wanapaswa kutoa mfano wa utawala wa haki na uwazi katika shughuli zote za uchaguzi.
Kwa kufanya hivyo, wataonyesha kuwa wanatenda kwa haki na wanajali matokeo ya uchaguzi kwa usawa.
 
Usalama wa umma

Usalama wa umma ni muhimu katika kuhakikisha uchaguzi wa amani. 
Viongozi wa vyama vya siasa wanatakiwa kushirikiana na vyombo vya usalama kuhakikisha kuwa kuna usalama wa kutosha katika maeneo yote ya uchaguzi. 
Kwa kuwa kampeni ni sehemu muhimu ya uchaguzi, viongozi wa vyama vya siasa wanapaswa kuhakikisha kampeni zinaendeshwa kwa mujibu wa sheria na kanuni. 
Maelezo na miongozo kuhusu taratibu za kampeni inatakiwa kutolewa kwa wanachama wa vyama na wagombea, kampeni zifanyike kwa amani, za kujenga na zisizo na lugha ya chuki. 
Pia, viongozi wa vyama vya siasa wanapaswa kushirikiana na mashirika ya kiraia na watendaji wa uchaguzi kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unakubalika na unafanyika kwa uwazi. 
Mashirika ya kiraia yanaweza kutoa maoni na mapendekezo ambayo yataboresha taratibu za uchaguzi na kuhakikisha kuwa haki za wananchi zinaheshimiwa. 
Ni muhimu viongozi wa vyama kuunga mkono juhudi za mashirika haya na kuhakikisha kuwa inakuwa sehemu muhimu ya mchakato wa uchaguzi.
Pia, viongozi wa vyama vya siasa wanapaswa kuhakikisha uamuzi wowote kuhusu uchaguzi unachukuliwa kwa uwazi. 
Matokeo ya uchaguzi yanatakiwa kutangazwa kwa uwazi na kwa wakati, ili kuzuia uvumi na migogoro. Kwa uwazi katika maamuzi, viongozi wataongeza uaminifu wa umma katika mchakato wa uchaguzi.

Mwenyekiti Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake ya CCM, (UWT) Taifa, Mary Chatanda alipendekeza wasimamizi wa uchaguzi wawe wenye sifa zinazostahili na zinazoelezewa vyema, kigezo cha historia ya uadilifu na uzoefu katika masuala ya uchaguzi kiwepo. 
“Hii itasaidia kuhakikisha kuwa msimamizi wa uchaguzi ni mtu mwadilifu na mwenye uzoefu wa kutosha katika kusimamia uchaguzi,” alisema Chatanda wakati wa uzinduzi wa kanuni za uchaguzi huo hivi karibuni.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alipendekeza kuongeza muda wa kampeni hadi angalau siku 14, tofauti na siku saba za sasa. 
Pia, alipendekeza uandikishaji wa wapigakura ufanyike mara moja, ili kupunguza matumizi ya fedha za umma. 
Mnyika alitaka kusiwe na ulazima wa msimamizi wa uchaguzi kuwa mtumishi wa umma, badala yake watu watume maombi na vyama viwe na fursa ya kuweka pingamizi.

Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Shaweji Mketo, alipendekeza kuondolewa kwa ulazima wa mawakala wa uchaguzi kuapishwa na hakimu, badala yake waapishwe na wasimamizi wa uchaguzi, jambo ambalo litapunguza vikwazo na urahisishaji wa taratibu.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), John Mongella aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi na kuwachagua viongozi wanaowafaa.
“Rais Samia Suluhu Hassan ameanzisha falsafa ya R4, ambayo ni msingi wa kudumisha amani, utulivu na kuchochea maendeleo ya nchi yetu. Tunapaswa kuhakikisha kuwa demokrasia inakua na maendeleo ya nchi yanaendelea kwa kasi,” alisema Mongella.
Falsafa ya R4 za Rais Samia ni maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga taifa.
Mongella alisema CCM kama chama kilichoanzisha demokrasia nchini, kimejizatiti kuhakikisha kuwa uchaguzi wa Serikali za mitaa unakuwa wa haki na usalama. 
“Iwapo kutatokea mtikisiko au kutokuwa na uwazi katika demokrasia, maendeleo ya nchi yetu yatakumbwa na changamoto. CCM itahakikisha kuwa haki na uhuru vinatamalaki katika uchaguzi huu,” alisema Mongella.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UDP, Saum Rashid, alisema ni muhimu vyama vya siasa kuhakikisha wagombea wao wanazingatia ratiba ya uchaguzi. 
Rashid alitoa wito kwa viongozi kutoa mwongozo kwa wanachama, ili kuepuka ucheleweshaji wa maandalizi na mchakato wa uchaguzi. 
“Ni muhimu kwa viongozi wa vyama vya siasa kutoa mwongozo kwa wanachama wetu wanaotarajia kugombea. Hii itasaidia kuepuka matatizo ya ucheleweshaji wa rufani na manung’uniko yasiyo ya lazima,” alisema Rashid.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema uchaguzi uliopita ulikumbwa na matatizo mengi na wagombea waliondolewa bila haki. 
Alionya kuwa uchaguzi wa mwaka huu unahitaji kuboresha hali hii, kwa kuhakikisha matakwa ya wananchi yanaheshimiwa na kura zinahesabiwa kwa usahihi. 
“Tunatarajia kuwa masuala ya kuenguliwa na kutopewa fursa yasiwepo. Tunataka matakwa ya wananchi yaheshimiwe na kura zihesabiwe kama zilivyopigwa,” alisema Profesa Lipumba.

Related Posts