Asilimia 31 ya watoto Mara wanabeba mimba

Tarime. Asilimia 31 ya watoto wenye umri kati ya miaka 15 – 19 katika Mkoa wa Mara wanapata mimba za utotoni, jambo linaloelezwa kuwa na madhara katika ustawi wa watoto na jamii nzima mkoani humo.

Hayo yamebainishwa leo Agosti 22, 2024 mjini Tarime na Mratibu wa Huduma za Afya na Uzazi na Mtoto Mkoa wa Mara, Leah Daniel kwenye mafunzo kwa waandishi wa habari yaliyoandaliwa na Shirika la Utu wa Mtoto (CDF) kwa lengo la kuwapa uelewa kuhusu suala zima la afya ya vijana na huduma binafsi (Selfcare) kwa vijana.

Leah amesema kwa mujibu wa takwimu za ripoti ya Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Maralia (THDS) za mwaka 2022, asilimia 31 ya watoto wenye umri huo hupata mimba mkoani humo na kwamba ipo haja kuhakikisha mimba na ndoa za utotoni zinakomeshwa kwani zina madhara makubwa kwa watoto na jamii kwa ujumla.

“Hii namba ni kubwa, ni muhimu kuchukua hatua za dharura na kuanzisha mikakati madhubuti ili kuhakikisha kuwa vijana wanapata elimu na huduma wanazohitaji ili kupunguza kiwango hiki na kuboresha maisha yao na sote tunalo jukumu katika hili,” amesema.

Amesema jamii inapaswa kutambua kuwa ulinzi wa mtoto ni jukumu la kila mmoja na kwamba watoto wanapaswa kupewa ulinzi wa kutosha, kuhakikisha wanakuwa salama kiakili, kisaikolojia, kimwili na kijamiii ili kujenga jamii bora ya baadaye.

Amesema mbali na mapambano dhidi ya ukatili kwa watoto, Serikali pia imeweka mikakati kadhaa kuhakikisha watoto na vijana wanakuwa salama ambapo mikakati hiyo ni pamoja na upatikanaji wa huduma rafiki ya afya ya uzazi kwa vijana.

“Huduma hii inapaswa kupatikana katika vituo vyote vinavyotoa huduma ya kliniki lakini kwa sasa ni vituo 24 pekee ndivyo vinatoa huduma hizi kati ya vituo 380 mkoani kwetu na hii ni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ufinyu wa bajeti. Jitihada zinaendelea kuhakikisha huduma zinapatikana kwa wingi na karibu ili vijana wawe na elimu ya kutosha kuhusu masuala ya afya ya uzazi,’’ amesema.

Amefafanua kuwa huduma rafiki ya uzazi kwa vijana inahusu elimu mbalimbali ikiwemo namna ya kuepuka maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, mimba za utotoni, hedhi salama na mambo mengine ambayo yanalenga kuwaweka walengwa salama kiafya, kiakili, kisaikolojia na kimwili.

Awali akizungumza katika mafunzo hayo, Ofisa Miradi kutoka CDF, Anold Massawe amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa kuandika habari zinazowahusu vijana hasa katika masuala ya uzazi na mapambano dhidi ya Ukimwi.

“Zipo huduma nyingi kwa vijana hasa zinazohusu afya ya uzazi pamoja na masuala ya namna ya kujikinga na maambukizi ya Ukimwi zinazotolewa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, hivyo ni vema waandishi mkatumia taaluma yenu kuwaeleza vijana kuhusu huduma hizi ili wanufaike nazo,” amesema.

Ameongeza kuwa shirika lake hivi sasa linatekeleza mradi ujulikanao kama Youth  Care kwa vijana wenye umri kati ya miaka 10 – 25 katika kata tisa wilayani Tarime, lengo likiwa ni kuhakikisha walengwa hao wanafaidika na sera bora na mazingira ya kijamii ili kuimarisha mfumo wa afya kwa ujumla.

Baadhi ya wakazi wa Tarime wamesema mimba za utotoni ni tatizo linalosababisha madhara mengi ikiwa ni pamoja na kuathiri maendeleo ya kielimu na kiuchumi ya vijana, pamoja na hatari za kiafya kwa watoto.

Joseph Ghati amesema takwimu hizo zinaonyesha kuwa Mkoa wa Mara una kiwango cha juu cha mimba za utotoni, jambo linalohitaji hatua za haraka na mikakati madhubuti ili kukabiliana nalo.

“Hawa watoto wanapewa mimba na sisi wanajamii, hivyo kabla hatujasema Serikali imeshindwa kuwapa ulinzi watoto, tuanze kujisema sisi, kila mmoja ajiulize amechukua hatua gani kumlinda mtoto, aidha wa kwake mwenyewe au wa jirani yake,” amesema Ghati.

Related Posts