Vita vya Ukraine vyatawala kampeni za majimbo Ujerumani – DW – 22.08.2024

Sera ya kigeni ya Ujerumani inatawala katika kampeni za uchaguzi ujao kwenye majimbo ya Saxony, Thuringia, na Brandenburg, ambapo umepangwa kufanyika mwezi Septemba, ingawa ni jukumu la serikali ya shirikisho.

Sababu inayowafanya wanasiasa wa majimbo kuchukua msimamo wa ghafla kwenye masuala ya sera ya kigeni, ni kuongezeka kwa mashaka miongoni mwa wakaazi, hasa wa mashariki mwa Ujerumani, kuhusu msimamo wa serikali ya shirikisho ya vyama vya Social Democratic, SPD, Kijani cha watetezi wa mazingira, pamoja na kile cha Waliberali, Free Democratic, FDP, kuhusu Ukraine.

Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari, mwaka 2022, Ujerumani imekuwa ikiiunga mkono Ukraine kwa takribani euro bilioni 23, kwa silaha, malipo ya moja kwa moja ya pesa taslimu, na misaada ya kiutu. Ni Marekani pekee ndiyo imeipatia Ukraine msaada zaidi.

Taasisi ya utafiti wa maoni ya umma ya Forsa hivi karibuni iligundua kuwa asilimia 34 ya watu waliohojiwa wa mashariki mwa Ujerumani wanaamini kuwa Ujerumani inazidisha kutoa msaada wake kwa Ukraine.

Soma pia:Scholz kuizuru Moldova na kujadili athari za vita vya Urusi nchini Ukraine

André Brodocz, mwanasayansi wa siasa katika Chuo Kikuu cha Erfurt, anasema masuala ya kisiasa ya shirikisho yanatumika kuchochea hisia katika kampeni za uchaguzi.

Katika mahojiano yake na shirika la umma la utangazaji, MDR, Brodocz, amesema hata kama hakuna kinachoweza kufanywa kuhusu suala hilo katika ngazi ya jimbo, bado ni muhimu kwa vyama kupata wapiga kura kwenye uchaguzi. Anasema masuala ya kihisia zaidi kama vile vita na amani, bila shaka yanatoa fursa nzuri katika hili.

Msimamo wa vyama vya siasa katika ajenda 

Huku vyama vya Christian Democratic Union, CDU na Christian Social Union, CSU katika ngazi ya shirikisho kwa kiasi kikubwa vinaunga mkono hatua za serikali nchini Ukraine, vyama viwili ambavyo vimepata nguvu hivi karibuni eneo la mashariki, vinapinga kupelekwa silaha, na vinaunga mkono mazungumzo na Urusi.

Ujerumani | CDU | Friedrich Merz
Friedrich Merz Mwenyekiti wa CDU akionesha kadi ya kupigia kura wakati wa mkutano wa chama.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Chama Mbadala kwa Ujerumani, AfD chenye kufuata siasa kali za mrengo wa kulia, na muungano wa BSW unaoongozwa na Sahra Wagenknecht, chama cha kizalendo kinachofuata sera za kiuchumi zinazoegemea siasa kali za mrengo wa kushoto na kinachopinga uhamiaji, na mipango ya sera ya kigeni inayoiunga mkono Urusi.

Chama cha Sahra Wagenknecht kilichoanzishwa mapema mwaka huu, kimepata asilimia 20 katika utafiti wa maoni ya wapiga kura jimboni Thuringia, na hivyo kinaweza kuwa na sauti muhimu serikalini baada ya uchaguzi.

Soma pia:Wapinzani Ujerumani wataka Waukraine wasiofanya kazi warudi kwao

Katika mahojiano yake na kituo cha redio cha Ujerumani, Deutschlandfunk mwezi Julai, Wagenknecht alisema uchaguzi wa mashariki pia ni kura ya maoni juu ya vita na amani. Kulinga na Wagenknecht, wapiga kura wake wanamtarajia ahakikishe kwamba hatari ya vita nchini Ujerumani haionegezeki.

Msimamo wa Wagenknecht katika vita vya ukraine kwa kiasi kikubwa unawiana na ule wa chama cha AfD, ambacho kinaongoza katika utafiti wa maoni ya wapiga kura Thuringia na Saxony, kikiwa na zaidi ya asilimia 30.

Akizungumzia vikwazo dhidi ya Urusi, mwenyekiti mwenza wa AfD, Tino Chrupalla amesema kuwa vikwazo vya uchumi dhidi ya Urusi lazima viondolewe, akidai kuwa vinautatiza uchumi wa Ujerumani, kwani wananchi wanalipa bei kubwa ya nishati, mfumuko wa bei umeongezeka na yote hayo ni matokeo ya vikwazo.

CDU: Punguzeni msaada wa kijeshi Kyiv

Waziri Mkuu wa Saxony, Michael Kretschmer wa chama cha CDU ametoa wito wa kupunguzwa kwa msaada wa silaha nchini Ukraine, kwa kuzingatia upungufu wa bajeti ya shirikisho na kuhimiza hatua za kidiplomasia katika mzozo wa Ukraine. Waziri Mkuu wa jimbo la Brandenburg, ametoa maoni sawa na hayo.

Katika kukabiliana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, sasa kuna mipango ya kuweka makombora mapya ya masafa ya kati ya Marekani nchini Ujerumani ifikapo mwaka 2026. Mjadala huu umeongezeka hivi karibuni.

Hilo lilitangazwa kwa mara ya kwanza wakati wa mkutano wa kilele wa Jumuia ya Kujihami ya NATO nchini Marekani katikati ya Mwezi Julai, na mapema mwezi Agosti, chama cha Kansela Olaf Scholz cha SPD kilikubali.

Ujerumani: Hatutaiacha Ukraine kwenye vita peke yake

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Thuringia Georg Maier amesema hana pingamizi kuhusu kuwekwa silaha za jeshi la Marekani, lakini maslahi ya usalama wa taifa ni kipaumbele kwanza, na wasiwasi wake ni jinsi suala hilo lililvyofanyika na kuwasilishwa.

Soma pia:Urusi, Ukraine mambo yazidi kuwa mabaya

Sahra Wagenknecht anasema kwamba chama chake cha BSW kitazingatia tu kujiunga na serikali ya jimbo lolote ikiwa washirika wake watakataa wazi mipango ya kuweka silaha mpya za Marekani kwenye kituo nchini Ujerumani.

Hata hivyo, akizungumza na DW, msemaji wa sera ya kigeni ya chama cha CDU, Roderich Kiesewetter amesema kwa maoni yake uamuzi huo wa kuweka makomboar utakuwa naathari ndogo sana kwenye uchaguzi.

Kwa hakika hayo sio maoni ya wanasiasa kutoka vyama tawala vya SPD, Kijani na FDP, pamoja na kile cha wahafidhina cha CDU, ambao wanafanya kampeni mahariki mwa Ujerumani.

Ukweli ni kwamba vyama kama hivyo, vinavyopendelea kuendelea kuunga mkono msaada kwa Ukraine na silaha mpya za MArekani nchini Ujerumani, vinazidi kuwa peke yake.

 

 

Related Posts