Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema Serikali imeyapokea mapendekezo na maoni yaliyotolewa juu ya ujenzi wa daraja kutoka Tanzania bara (Dar es Salaam) kwenda visiwani Zanzibar.
Mbali na hilo amesema matumizi ya pesa ya China (Yuan) na shilingi ya Tanzania katika shughuli za biashara na uwekezaji na nchi ya China, vilevile Serikali imechukua kwenda kuyafanyia kazi kwa kuyachakata.
Mapendekezo hayo yametolewa na Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi wakati akizungumza kwenye Jukwaa la mashirikiano ya maendeleo kati ya China na Tanzania ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya diplomasia ya mataifa hayo mawili.
Katika kongamano hilo lililofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam leo Alhamisi Agosti 22, 2024, Profesa Moshi amesema China ni rafiki wa kwanza wa Tanzania katika nyanja mbalimbali, hivyo ameomba wawekezaji na Serikali ya nchi hiyo kujenga daraja huku akipendekeza liitwe Daraja la Karume/Nyerere.
Aidha, Profesa Moshi ameomba kuibadilisha reli kati ya Tanzania na Zambia (Tazara) kuwa reli ya kisasa kama zilivyo za China kwa ajili ya kuendana na dunia ya sasa.
“Katika matumizi ya pesa nashauri tutumie Yuan na Shilingi kwa sababu dola ni gharama kubwa, tukitumia pesa za ndani basi tutapunguza hasara na athari mbaya za dola kwenye ulipaji wa deni, mfumuko wa bei na gharama ya maisha,” amesema.
Aidha, msomi huyo amesema itakuza matumizi ya sarafu za ndani katika miamala ya kibiashara kama njia ya maendeleo ya kiuchumi.
Sambamba na hilo, Profesa Moshi ameomba uwekezaji katika kilimo cha kisasa ili kuongeza tija, kwa nia ya kuongeza kasi ya kupunguza umaskini, na kukuza uchumi shirikishi zaidi.
Vilevile, amehamasisha matumizi ya vyanzo mbadala vya nishati, yaani jua na upepo, kwa nia ya kupunguza utegemezi wa maji. Pia, kwa upande mwingine ameipongeza nchi ya China kwa kukitangaza Kiswahili.
Katika kuyajibu hayo alipoulizwa na Mwananchi wakati akizungumza na waandishi wa habari nje ya kongamano hilo, Profesa Mkumbo amesema Serikali imeyapokea yote hayo.
“Ni hoja, mawazo na maoni mazuri, tumezipokea tunajua wasomi wamefanyia utafiti mfano kwenye kilimo, daraja na uwekezaji, mimi kama waziri wa mipango na anayesimamia dira ya Taifa tumepokea,” amesema.
Sambamba na hilo, amesema uboreshwaji wa reli ya Tazara inayoziunganisha nchi za Tanzania na Zambia huku akisema hadi sasa tayari wameshakubaliana na China kushirikiana namna ya kuifufua reli hiyo.
“Waziri wetu wa uchukuzi ataenda kusaini mkataba na kampuni ya China katika safari ijayo ambapo China imealika nchi 52 za Afrika watasaini kwa ajili ya kuimarisha reli ya Tazara.”
Akieleza zaidi, Profesa Mkumbo amesema China kwa sasa inaongoza katika uwekezaji na Tanzania ikiyapiku mataifa ya magharibi na nchi yetu itazidi kuiga China kwakuwa walishawekeza kwenye elimu na uchumi wa viwanda kisha wakaaga umasikini.
“Lazima tuwatoe watu kwenye uchuuzi kwenda kwenye uzalishaji wa viwanda na Serikali inazidi kuweka mkazo kwenye maeneo hayo,” amesema Profesa Mkumbo.
Imeandikwa na Mariam Mbwana, Sute Kamwelwe na Victoria Michael