Baada ya miezi 10 ya vita, maafisa kutoka Marekani na wapatanishi wa mataifa ya Kiarabu ya Misri na Qatar walitarajiwa kukutana wiki hii mjini Cairo katika duru mpya ya mazungumzo, lakini bado hakuna uthibitisho wowote. Siku ya Jumatano, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alihitimisha ziara yake Mashariki ya Kati, iliyokuwa na lengo la kukamilisha makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza, ingawa haijaleta mafanikio yoyote.
Jumatano usiku, Rais wa Marekani Joe Biden alizungumza kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na kumshinikiza kuhusu udharura na umuhimu wa kusainiwa makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza na kuachiliwa kwa mateka.
Ama kwa upande mwingine, magari ya Jeshi la Israel, IDF yameonekana yakipiga doria katika kambi ya wakimbizi kwenye eneo inalolikalia kimabavu la Ukingo wa Magharibi, baada ya watu watatu kuuawa katika shambulizi la Israel. Wizara ya Afya ya Kipalestina imesema kuwa shambulizi hilo limefanyika usiku wa kuamkia leo katika kambi ya wakimbizi ya Tulkarem.
Aidha, msemaji wa serikali ya Israel, David Mencer amesema IDF imewaua zaidi ya wapiganaji 17,000 wa Hamas, ndiyo maana njia ya Philadelphi, mpaka kati ya Misri na Israel, inayotumiwa zaidi na Hamas kufanya biashara ya magendo ya kigaidi ni muhimu.
Israel yaongeza shinikizo kwa Hamas
”Sisi, kwa upande wetu tunaweka shinikizo la kijeshi kwa Hamas. Tunajua hilo ndilo jambo linalofanya kazi. Ni pale tu tunapofanikiwa kupambana nao, ndiyo watakuwa makini kuhusu mpango huu wa kuachiliwa mateka, na tunaendelea kufanya hivyo,” alifafanua Mencer.
Wakati huo huo, vikosi vya usalama vya Israel vimewakamata watuhumiwa wanne kufuatia shambulizi lililofanywa na wanamgambo walowezi wa Kiisrael katika kijiji cha Jit, katika Ukingo wa Magharibi. Shirika la Ujasusi la Israel, Shin Bet limeliita shambulizi hilo kama ”tukio la kigaidi.” Maafisa wa Israel wamesema watuhumiwa hao wanahojiwa na kwamba uchunguzi unaendelea.
Shambulizi hilo lilitokea Alhamisi iliyopita, wakati ambapo mwanaume wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 23 alipouawa na mkaazi mwingine kujeruhiwa baada ya walowezi kadhaa waliokuwa wamejifunika nyuso zao kushambulia kijiji chao. Wakaazi wamesema takribani walowezi 100 waliokuwa na visu na silaha za moto walichomo moto nyumba na magari. Shambulizi hilo lilikosolewa vikali na maafisa wa Israel, pamoja na Marekani, Umoja wa Mataifa na nchi za Ulaya.
Mabaharia walioshambuliwa na Wahouthi waokolewa
Huku hayo yakijiri, meli ya Ufaransa imewaokoa mabaharia 29 ambao meli yao ya mafuta iliyoshambuliwa na waasi wa Kitouthi wa Yemen wakati ikipita Bahari ya Shamu.
Maafisa wamesema leo kuwa meli hiyo iliyokuwa sehemu ya ujumbe wa Ulaya kulinda usalama katika eneo hilo, pia imeharibu droni la baharini.
Meli hiyo iliyokuwa na bendera ya Ugiriki inayoitwa Sounion, ilitelekezwa kutokana na matatizo ya injini, lakini itahamishwa na kupelekwa sehemu salama zaidi. Wahouthi wamesema wamefanya shambulizi hilo kuonesha mshikamano na kundi la wanamgambo la Hamas huko Gaza na kueleza kuwa wataacha kufanya mashambulizi yao dhidi ya usafiri wa baharini iwapo vita vitasitishwa huko Gaza.
(AP, AFP, DPA, Reuters)