Benchikha na wenzake shida iko hapa

Baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha kuondoka jana, hatimaye timu hiyo sasa imebaki chini ya Juma Mgunda na Selemani Matola, lakini kuna maswali mengi ya kujiuliza ambayo yanatia shaka juu ya muenendo wa kikosi hicho.

Tetesi za kuondoka kwa Benchikha zilianza kuzagaa kwa muda mrefu, huku mara chache uongozi wa timu hiyo ukikanusha kuhusu suala hilo.

Benchikha mwenye wasifu mkubwa kuliko makocha wote ambao wamewahi kuifundisha timu hiyo, ameondoka kwenye timu hiyo baada ya kudumu kwa siku 157 pekee, akiwa ndiye kocha kwa miaka ya hivi karibuni aliyekaa kwenye timu hiyo kwa muda mfupi zaidi.

Taarifa ya klabu hiyo imesema kuwa kocha huyo aliomba kuvunja mkataba kutokana na kusumbuliwa na matatizo ya kifamilia, huku ikienda mbali zaidi ikisema anakwenda kumuuguza mke wake.

Hata hivyo, kumekuwa na maswali mengi kuhusu taarifa hiyo ya Simba, kwa kuwa wengine wanaamini kuwa suala la kumuuguza mke wake lilikuwa linaweza kubaki kwa kocha mkuu peke yake, kama ana mapenzi na Simba wasaidizi wake wangebaki hadi atakapomaliza matatizo yake na kurejea.

Lakini swali lingine ni je? Wakati Benchikha anaunguza wasaidizi wake watakuwa hawana kazi na atauguza kwa muda gani? Kinachoonekana ni kwamba Simba na Benchikha walishindwana kwa mambo mengine na suala la kuuguza ni ishu ya ziada kabisa kwa kuwa angeweza kuondoka baada ya kumalizika kwa msimu jambo ambalo lingeisaidia timu hiyo kutafuta kocha bora sokoni.

Moja ya jambo linalotajwa kumuondoa kocha huyo ni gharama kubwa ambazo wamekuwa wakitumia kwa kocha huyo ikiwemo kuishi hotelini, lakini mshahara mkubwa aliokuwa analipwa wakati ambapo hakuna chochote Simba wanatarajia kuvuna kwa sasa hadi mwisho wa msimu.

Katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali kati ya Simba na Al Ahly, uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, Benchikha alionyesha hadharani kutoridhishiwa na kikosi cha timu hiyo baada ya kulala kwa bao 1-0.

Kocha huyo raia wa Algeria baada ya mchezo huo alisema: “Ninasikitika kwa kuwa Simba ina kikosi kidogo sana, ni wachezaji wachache ambao wana uwezo wa kuitumikia timu hii.” Kauli hii ambayo ilitolewa na kocha huyo ilionyesha kuwa ameshakata tamaa na kikosi hicho chenye makombe 22 ya Ligi Kuu Bara.

Huu ulikuwa mchezo mwingine wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Liti Singida, Aprili 13, baada ya kubaki uwanjani peke yake kwa zaidi ya dakika saba baada ya mchezo kati ya timu hizo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Hali hii ilionyesha dalili kuwa kocha huyo ameshaanza kukata tamaa juu ya mwenendo wa timu hiyo na baada ya kuhojiwa alijibu:

“Ni hali ya kawaida, kubaki mwenyewe ni kitu cha kawaida kabisa kwangu nilikuwa natakafakari kwa kuwa sikuridhishwa na safu yangu ya ushambuliaji, tulikosa mabao mengi, nafikiri wakati mwingine tunatakiwa kuwa makini, lakini mwenendo wetu kwenye eneo hilo siyo mzuri, tazama tunatengeneza nafasi lakini tunashindwa kuzitumia,” hii ilikuwa kauli ya kocha huyo ya kuonyesha kukata tamaa.

Taarifa zinasema kuwa wiki mbili za mwisho kocha huyo alionyesha mabadiliko makubwa sana mazoezini, akiwa haongei kama kawaida yake na wakati mwingine anafika na kuwapa programu wasaidizi wake na kukaa kwenye kiti nje.

“Alianza kuonyesha dalili kuwa hana furaha, kama ni ishu ya mke wake au hakuridhishwa na timu sijui, lakini tofauti na awali alikuwa anafika mazoezini muda mwingi anakaa nje na kuwapa programu ya mazoezi wasaidizi wake na Matola wasimamie.

“Wakati mwingine mwanzoni alikuwa anafanya hivyo, lakini anakuja uwanjani mara moja moja kuelekeza jambo, dakika za mwisho alikuwa hafiki kabisa kwenye uwanja hadi wakati ambapo wachezaji wamemaliza mazoezi, ikiwemo kambi ya Zanzibar na maandalizi ya Kombe la Muungano,” kilisema chanzo.

Historia yake kwenye timu:

Rekodi zinaonyesha kuwa Benchikha hana rekodi ya kukaa kwenye timu moja kwa muda mrefu, lakini pia kusema kuwa anaondoka kwa ajili ya matatizo ya kifamilia ni jambo la kawaida kwake.

Inaonekana kuwa pamoja na wasifu mkubwa alionao lakini hana uwezo sana wa kuishi kwenye presha kubwa au timu ikianza kuyumba.

Mwaka 2011, akiwa kocha mkuu wa Algeria alijiuzulu saa chache baada ya timu hiyo kufungwa mabao 4-0 na Morocco, jambo ambalo liliwashangaza wengi kutokana na jinsi alivyokuwa ameitengeneza timu hiyo.

Lakini pia mwaka jana akiitumikia USM Algier, ambayo aliipa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuitoa Yanga na kuipa timu hiyo ubingwa wa African Super Cup, alijiuzulu baada ya mashabiki kumzomea kwenye mchezo wa ligi, jambo ambalo wengi hawakuwa wanalitarajia kutokana na umaarufu na rekodi ambazo alikuwa ameziweka kwenye timu hiyo kwa muda mfupi.

Hapa pamoja na mambo mengine alisema anataka kwenda kushughulikia matatizo ya kifamilia yanayomkabili.

Simba kuna tatizo, makocha tisa miaka saba

Kuondoka kwa Benchikha siyo jambo la kushtua sana kwa mashabiki wa Simba kwa kuwa kwa miaka ya hivi karibuni ni kitu ambacho kimeshazoeleka na kinaonekana cha kawaida.

Mwenendo wa makocha kwa zaidi ya miaka saba iliyopita umekuwa siyo wa kuridhisha, huku wote wakiwa na wastani wa kudumu kwenye timu hiyo kwa mwaka mmoja au nusu ya hapo, jambo ambalo linashtua kwenye mwendelezo wa timu hiyo.

Kuanzia mwaka 2018, makocha tisa wamepita kwenye timu hiyo, huku kukiwa hakuna hata mmoja ambaye alimaliza mkataba wa miaka miwili ambao alisaini na timu hiyo.

Pierre Lechantre alijiunga na timu hiyo Januari 2018 na kuondoka kwenye timu hiyo Juni 2018, akiwa amedumu kwenye kikosi hicho kwa kipindi cha miezi sita pekee.

Patrick Aussems, mmoja wa makocha waliokuwa kipenzi cha mashabiki wa timu, alijiunga na Simba Julai 2018 na kudumu hapo kwa mwaka mmoja na miezi miwili akatimka Novemba 2019, akiwa alianzisha safari ya robo fainali za Ligi ya Mabingwa kwa Simba.

Baada ya kuondoka kwa kocha huyo, Simba ilimshusha Sven Vandenbroeck ambaye alikaa kwenye timu hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja na mwezi mmoja, baada yake alitua Didier Gomes, naye hakudumu pamoja na sifa zote alikaa kwenye timu hiyo kwa miezi kumi pekee na kutimka zake.

Baada ya huyo, Simba ilimleta Pablo Franco, msela flani kutokea nchini Hispania, ambaye alipewa sifa nyingi ikiwemo kuwahi kuifundisha timu kubwa ya La Liga, Getafe, naye alidumu kwenye kikosi hicho kwa miezi sita pekee na kutimkia nchini Afrika Kusini.

Baada ya kocha huyo alitua Zoran Maki, huyu aliweka rekodi baada ya kudumu Simba kwa miezi miwili tu akiwa ndiye aliyekaa kwenye timu hiyo kwa muda mfupi zaidi, alipotua hapo Juni 2022 hadi Septemba 2022.

Baada ya Zoran Maki, Simba ilimchukua Juma Mgunda ambaye alisafiri nayo kwenda Angola kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambaye pamoja na utata wa masuala ya vyeti ambao ulimkuta, alidumu hapo kwa miezi mitatu kuanzia Septemba 2022 hadi Januari 2023, akaondolewa na timu akapewa Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’, ambaye alidumu kwa miezi 11 na kusepa, nafasi yake akachukua Abdelhak Benchikha.

Kiuhalisia makocha wengi waliotoka Simba walikwenda kufundisha timu za juu zaidi, hali ambayo inaonyesha kuwa kuna tatizo kwenye uongozi wa timu hiyo kuhusu jinsi wanavyoishi na makocha wao, au aina ya makocha wanaowachukua siyo wale wanaotakiwa kuwa kwenye timu hiyo.

Kauli zao wakiondoka zashtua:

Robertinho, wakati anaondoka Simba alisema timu hiyo haina wachezaji bora, huku akifika mbali zaidi kwa kusema kuwa wachezaji sahihi ni wawili tu.

Zoran Maki, taarifa ilisema kuwa ameomba kuvunja mkataba, lakini akiwa uwanja wa ndege alisema Simba inatakiwa kufanyia kazi mapungufu yake.

Aussems, aliishukia Bodi ya ukurugenzi ya timu hiyo na kusema inatakiwa kufanya kazi yake ipasavyo na kuna watu hawatakiwi kuwa pale, akisema ni waongo.

Sven, yeye hakuongea jambo lolote alipoulizwa uwanja wa ndege, lakini alikuwa kocha pekee ambaye alisindikizwa na Mtendaji Mkuu wa timu hiyo wakati huo, Barbara Gonzalez hadi uwanja wa ndege na kutimka.

Pablo, yeye aliondolewa na Simba baada ya timu kutoka kwenye Kombe la Shirikisho ambapo alisema hakuwa anataka kuondoka, kwa kuwa tayari alishaleta familia yake hapa na amepewa barua lakini ameikataa, lakini kama uongozi umeamua hana jinsi.

Juma Mgunda, Matola kila siku:

Hii ni mara ya pili Mgunda anarudi Simba, lakini kwa kipindi chote timu hiyo imekuwa chini ya Matola kila makocha wanapoondoka.

Chanzo cha ndani kutoka Simba kinasema kuwa timu hiyo imemsomesha Matola kwa nia moja kuwa asaidie kwenye kikosi hicho ndiyo maana kila wanapokuja makocha lazima naye awepo kwenye benchi la timu hiyo, lakini pia uwezo wake unatajwa kuwa mkubwa sana wa kufundisha.

“Tanzania ukitaja makocha wazawa bora basi huwezi kumuacha Matola, timu alizofundisha ukiachana na Simba zinaonyesha ni jinsi gani ana ubora wa hali ya juu.

“Sikumbuki, lakini nafikiri ni makocha wawili tu au watatu wazawa ambao wamefika fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, akiwemo yeye wakati anaiongoza Lipuli ya Iringa, lakini pia wale wasomi wenye Leseni A, huyu ni mmoja wao, hivyo nafikiri Simba wamekuwa wakimuangalia kwa mtazamo huo.

“Kwa upande wa Mgunda, huyu ni mtu wao amekuwa akiitwa anakubali bila shida yoyote lakini pia kocha mwingine mwenye ubora kama wake asingekubali kushushwa timu ya wanawake, hivyo nafikiri ni nidhamu ndiyo inambeba zaidi.

“Hata hapa hawezi kudumu, labda ataondoka yeye au Matola baada ya kocha mpya kuja, tusubiri tuone,” kilisema chanzo.

Kocha na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Abdallah ‘King’ Kibadeni alisema suala la Kocha, Benchikha kuondoka lina mambo mengi yaliyokuwa nyuma yake licha ya sababu kuelezwa kwenda kwao Algeria kwa ajili ya kutatua changamoto za kifamilia.

“Huenda angeenda na kurudi tena ila ameona CV (wasifu) wake unazidi kushuka jambo ambalo anaona ni bora kuondoka mapema, suala la matokeo pia ni changamoto kwa sababu kama timu haifanyi vizuri yeye ni mtu wa kwanza kulaumiwa,” alisema.

Kwa upande wa nyota wa zamani wa timu hiyo, Mtemi Ramadhan alisema, binafsi anaona shida kubwa iko kwa viongozi na wachezaji kwa sababu licha ya makocha wengi waliopita kuonekana bora ila bado changamoto kwao imekuwa kutodumu kwa muda mrefu.

“Mimi naweza kusema hata kama akija kocha mkubwa lakini ikiwa wachezaji hawajitumi ni kazi bure, Benchikha hakuna ambaye hajui uwezo wake, sasa ukiniambia ni kutokana na matatizo ya kifamilia pekee yaliyoanishwa sikubaliani nalo kabisa.”

Mtemi aliongeza, kuna muda unaona wachezaji hawajitumi kabisa yaani wanacheza michezo ya kimashindano kama mechi za kirafiki.

“Kuna makocha walikuja Simba na wakaondoka kwenye mazingira ya aina hii ila walikokwenda wanafanya vizuri, mimi naona shida iko labda kwa viongozi kwa sababu kama hawapati mahitaji yao kwa wakati ni lazima tu watacheza chini ya kiwango.”

Matarajio makubwa kwa Mgunda

Baada ya timu hiyo kuwa chini ya Mgunda na Matola, mashabiki wamekuwa na matarajio makubwa kutokana na kile ambacho makocha hao walikifanya baada ya kuondoka Zoran Maki wakaachiwa timu.

Mgunda ni kati ya makocha waliounda benchi la ufundi la Simba lililoifikisha timu hiyo Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita akiwa na Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ raia wa Brazil lakini baadaye aliondolewa na kupelekwa timu ya Wanawake, Simba Queens.

Kwa kipindi cha miezi mitatu ambacho alikaa na timu hiyo, ilionyesha soka safi huku akiwa kipenzi cha mashabiki kwa kauli yake ya ‘Acha Boli Litembee.”

Mgunda alionyesha kiwango cha juu sana akiwa na Simba ambapo kwenye michezo tisa alipoteza mmoja tu dhidi ya Azam ilipochapwa bao 1-0, huku akilazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Yanga.

Lakini pia aliweka rekodi ya kocha wa kwanza mzawa kuifikisha timu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998, alipoziondoa Nyassa Bullets kwa jumla ya mabao 4-0, De Agosto kwa jumla ya mabao 4-1.

Kwenye ligi katika michezo mitano alipoteza mmoja tu, akifunga mabao 10 na kufungwa mabao mawili, rekodi ambazo mashabiki wa Simba wanatakiwa kuzisubiri kwa sasa wakati inaelezwa timu hiyo itakuwa chini yake hadi mwishoni mwa msimu.

Anaanza kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Namungo kesho, baada ya hapo ataendelea kwenye michezo mingine nane ya ligi iliyobaki ukiwemo dhidi ya Azam, hili ni jambo la kusubiri.

Related Posts