WAPENDWA wasomaji wetu, hii ni makala ya 100 katika safu hii ya Nionavyo. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa hatua hii, maana kwa zaidi ya majuma 100 ametuwezesha kuifanya kazi hii.
Mrejesho na msukumo kutoka kwenu wasomaji ndio umewezesha kufanikiwa katika yote. Udhaifu wa safu hii unabaki kuwa wa kwangu binafsi. Ahsanteni sana!
Wiki iliyopita tulishuhudia klabu tano za soka zikiiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Shirikisho la Soka Africa (CAF) ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika. Yanga, Azam FC na JKU ya Zanzibar zilicheza mechi za mkondo wa kwanza za Ligi ya Mabingwa, wakati Coastal Union na Uhamiaji zenyewe zilicheza mechi za Kombe la Shirikisho. Yanga iliifunga Vital’O ya Burundi iliyokuwa wenyeji jijini Dar es Salaam kwa mabao 4-0, Azam ikaicharaza APR kwa bao 1-0 ikiwa nyumbani, wakati Coastal ikiwa ugenini Angola ilifungwa mabao 3-0 na Bravo d Maquis, ilihali JKU na Uhamiaji kutoka Zanzibar zilicheza mechi zao za nyumbani zikiwa ugenini na kila moja kupokea kipigo cha mabao 6-0 na 2-0 mtawalia. JKU ilifungwa na Pyramids ya Misri kwa mabao 6-0 jijini Cairo Misri na Uhamiaji ililala 2-0 kwa Al Ahli Tripoli ya Libya, jijini Tripoli. Wikiendi hii timu hizo za wawakilishi wengine wa Tanzania watarudiana na wapinzani wao ili kuamua timu za kufuzu raundi inayofuata kutafuta tiketi ya kucheza hatua ya makundi.
Licha ya kusononeshwa na matokeo ya vipigo kwa timu hizo, lakini kilichoniumiza zaidi ni michezo ya nyumbani ya JKU na Uhamiaji yote kuchezwa ugenini.
Acha mbali matokeo, maumivu makali yalikuwa kwa timu zetu mbili za kutoka Ligi ya Zanzibar yaani JKU na Uhamiaji zilizocheza Misri na Libya mtawalia. Klabu hizo ziliingia makubaliano na wenyeji wao ili michezo yao yote ifanyike ugenini. Kwa maana nyingine haki yao ya kuwa nyumbani waliigawa kwa wenyeji wao na matokeo hayakuwa mazuri kwao.
Mara nyingi nimeandika katika safu hii kuhusu faida ambayo Tanzania inapata kutokana na kuwakilishwa na timu 6 katika mashindano ya Afrika.
Hata hivyo, hadi hivi karibuni kuwakilishwa kwetu na timu sita bado hakuonekani kwani timu zetu zimekuwa zikitolewa mapema na matumaini ya wapenzi wa mpira kubaki kwenye wawakilishi wawili yaani Simba na Yanga.
Sikumbuki ni lini ilitokea timu ya Tanzania ikacheza mechi zote za nyumbani katika viwanja vya ugenini. Serikali ya Jamhuri ya Tanzania na ile ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zimefanikisha ujenzi wa miundombinu ya kuchezea mpira wa miguu kiasi kwamba viwanja vyetu vimekuwa ni kimbilio kwa klabu na timu za taifa za mataifa mengine.
Kumekuwa na taarifa za klabu hivi sasa kupata ‘udhamini’ kutoka Libya na Misri. Haileti maana sana kupata udhamini kutoka kwa unayekwenda kukabiliana naye, achilia mbali ukweli kwamba michezo yote inakwenda kufanyika nyumbani kwa adui.
Pamoja na kuwepo kwa changamoto za rasilimali fedha, bado naamini kuwa zingeweza kutafutwa njia mbadala za kukabiliana na changamoto hii bila kujipeleka mikononi mwa adui.
Kwa muda mrefu Zanzibar imekuwa na nafasi katika CAF kama mwanachama mshiriki. Ushiriki mzuri wa Zanzibar ndio unaweza kutuhakikishia kuendelea kuwepo kwa nafasi mbili za klabu na hata kuongezewa nafasi.
Ni muhimu sana nafasi hizo zikalindwa kwa wivu. Tutajuta tutakapokuwa tumezipoteza japo sasa tunazo na ushiriki wetu haujazitendea haki.
Michezo ya marudiano kwa JKU na Uhamiaji huko Misri na Libya, inavyoelekea itakuwa ya kuweka rekodi sawa kwani mazingira ya nyumbani ugenini yanaonekana tayari kutokuwakubali. Tuombe michezo yao hii ipite salama, lakini itafutwe dawa kuhakikisha hili halijirudii.
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.