Binti kesi ya ‘waliotumwa na afande’ atoa ushahidi

Dodoma. Binti anayedaiwa kubakwa na kuingiliwa kinyume cha maumbile, mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Salaam aliyepewa jina la XY ametoa ushahidi mahakamani.

Akiwa shahidi wa tatu wa upande wa Jamhuri ametoa ushahidi leo Agosti 22, 2024 mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi, Zabibu Mpangule katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma.

Binti huyo (XY) aliingia katika jengo la Kituo Jumuishi cha Kutoa Haki cha Dodoma akiwa amevaa mavazi meusi yaliyoficha sura yake akiongozana na wanawake wawili.

Ametoa ushahidi kuanzia saa nane mchana hadi saa 12.00 jioni katika kesi hiyo ya jinai namba 23476 ya mwaka 2024.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105 Clinton Damas maarufu Nyundo, askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba.

Akizungumza baada ya kesi kuahirishwa jana, wakili wa utetezi, Meshack Ngamando amesema leo wamesikiliza ushahidi wa shahidi mmoja aitwaye XY.

“Tumemaliza kumsikiliza shahidi huyu na kesi imeahirishwa hadi kesho (Agosti 23) saa 4.00 asubuhi. Mwenendo wa kesi unaendelea vizuri,” amesema.

Kesi hiyo ilipoahirishwa jana Agosti 21, ilipangwa kuendelea kusikilizwa leo saa nne asubuhi lakini kwa mujibu wa wakili Ngamando ilianza saa nane mchana.

Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Renatus Mkude amesema wataendelea kupokea ushahidi, lakini idadi ya mashahidi katika kesi hiyo itaendana na mwenendo wa kesi ulivyo.

“Siku ya kwanza nilisema kesi hii itasikilizwa kwa siku tano mfululizo. Idadi ya mashahidi inategemea mwenendo wa kesi husika,” amesema.

Wengine waliotoa ushahidi ni shahidi wa kwanza, mtaalamu wa uchunguzi wa mambo ya sayansi ya simu na vifaa vya kielektroniki kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi na shahidi wa pili, ni daktari kutoka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

Related Posts