Ngorongoro. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ngorongoro, Murtallah Mbillu amesema baada ya Mahakama kuzuia tamko la Serikali la kufuta kata, vijiji na vitongoji, vikiwamo vya wilayani Ngorongoro, maandalizi ya uchaguzi yanaendelea kama kawaida.
Mbillu amesema hayo leo Alhamisi, Agosti 22, 2024 wakati akizungumza na Mwananchi ikiwa ni saa chache kupita tangu, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha itoe zuio la utekelezaji wa tamko hilo namba 673 la Agosti 2, 2024.
Agosti 2, 2024 lilitolewa tangazo la Serikali chini ya kifungu cha 30 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya, lililotoa tamko la kufuta vijiji, kata na vitongoji kutoka wilaya za Ngorongoro, Bahi, Chemba, Kasulu, Kakonko, Hai na Rombo.
Uamuzi huo wa mahakama umetolewa na Jaji Ayoub Mwenda, aliyesikiliza maombi madogo ya zuio hilo yaliyowasilishwa na mmoja wa wananchi wa Ngorongoro, Isaya Ole Pose kupitia wakili Peter Njau.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Mwenda aliridhia maombi hayo madogo na kukubali zuio la kusimamisha tamko hilo kupisha usikilizaji wa maombi ya msingi.
Akizungumza na Mwananchi, Mbillu amesema, lile tangazo la kuwahamisha lilikuwa la Wizara ya Maliasili na Utalii ambalo lilisababisha kutolewa kwa tangazo la Serikali (GN).
“Baada ya zuio hilo, mimi kama mkurugenzi nimeanza kutekeleza yale yanayotekelezwa na wizara za kisekta, kwa sababu Mahakama imeamua na kusitisha,” amesema Mbillu na kuongeza:
“Mimi kama mkurugenzi wa Ngorongoro taratibu zingine kama maandalizi ya uchaguzi na uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, zinaendelea kama kawaida.”