Zijue sababu za mtoto kuchelewa kuongea

Dar es Salaam. Moja kati ya mambo yanayompa furaha mzazi ni pamoja na kusikia sauti ya mtoto wake akitamka neno kwa mara ya kwanza.

Mara nyingi watoto wengi wanapotaka kuzungumza huanza kutamka maneno kama baba, dada, mama, kaka, tata, mma na mengine ambayo wakati mwingine hawayatamki vizuri kwa sababu wanakuwa katika hatua za awali za kujifunza.

Hata hivyo, kadiri siku zinavyozidi kwenda, mzazi anatarajia mtoto wake ataendelea kujifunza na kuzungumza maneno mengine na kuongeza idadi ya misamiati anayojifunza kila siku ili baadaye waweze kuzungumza na kuwasiliana vizuri.

Hata hivyo, hatua hii ya ukuaji hutofautiana kati ya mtoto mmoja na mwingine kwa kuwahi kuanza kuzungumza na wengine huchelewa.

Inapotokea mtoto amechelewa kuzungumza, husababisha wasiwasi pengine mtoto wake ana changamoto za kiafya zinazosababisha kuchelewa kuzungumza.

Baadhi yao huwa wanajiuliza, mtoto anapofika umri gani akiwa bado hajaanza kuongea ndio tunaweza kusema amechelewa?

Yvonne Sanga, mama wa watoto wawili anasema mtoto wake wa pili alichelewa kuzungumza hadi alipofikisha miaka mitatu, kama ilivyo kwa watoto wengine katika umri huo. Hata hivyo, Yvonne anasema baada ya kumpeleka hospitali aligundulika kuwa na usonji.

Sunday Mgalula, baba wa watoto wanne anasema mtoto wake wa mwisho ambaye sasa ana umri wa mwaka mmoja na miezi minane, ndiyo ameanza kujifunza kutamka maneno machache kama vile baba, mama, bibi dada huku watoto wake watatu wangine wakiwa katika umri huo walikuwa wakizungumza vizuri.

“Nafikiri ni kutokana na nyumba tuliyohamia sasa haina watoto wa kucheza naye, dada yake na kaka zake muda mwingi wanakuwa shuleni, nasubiri akifika miaka miwili nikamuanzishe shule ili aweze kuchangamana na wenzake,” anasema Sunday.

Wakati wazazi hao wakilalamika watoto wao kuchelewa kuanza kuongea, Rehema Singano ambaye ni mama wa mtoto mmoja anasema, mwanaye alianza kuongea na kuunganisha sentensi vizuri akiwa na mwaka na miezi tisa hadi baadhi ya watu walikuwa wakimshangaa.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanabainisha kuwa hali hiyo hutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo zile za kimazingira, maumbile, magonjwa pamoja na urithi.

Akizungumza kuhusu sababu za kimazingira, Mtaalamu wa saikolojia, Modesta Kimonga anasema mazingira yana nafasi kubwa katika kumfanya mtoto awahi au kuchelewa kuongea.

Kimonga anatolea mfano kama mtoto amelelewa katika mazingira ambayo yamezungukwa na watu wengi, humsaidia kusikia watu wakizungumza mara kwa mara, humfanya pia awe mwepesi wa kujifunza, hivyo kama hana changamoto nyingine ya kiafya anaweza kuwahi kuzungumza kuliko yule ambaye anaishi katika mazingira ambayo hachangamani na watu au watoto wa rika lake.

“Ni muhimu kujiuliza ni vitu gani vimemzunguka mtoto kama mazingira ni ya ukimya sana, hayamruhusu kuchangamana na watu wengine au kupata mtu wa kuongea naye, inaweza kumfanya achelewe kuongea,” anasema.

Kauli ya Kimonga inaungwa mkono na Ofisa Mkunga Msaidizi kutoka Hospitali ya Wilaya ya Bahi, Anitha Mganga anayesema mtoto anayepata fursa ya kucheza na watoto wenzake ni rahisi kujifunza lugha.

Hivyo kama hana changamoto nyingine ana nafasi kubwa ya kuwahi kuanza kuzungumza kuliko yule ambaye anafungiwa ndani.

“Kama mtoto mdogo hachezi na watoto wenzake yeye ni amefungiwa ndani tu hakuna wa kuongea naye mara kwa mara, muda wake mwingi anaangalia tu runinga au kuchezea simu akiwa katika umri mdogo, inaweza kumfanya kuchelewa kuongea,” anasema.

Anasema mtoto anapocheza na wenzie huwa ni njia mojawapo ambayo hujifunza maneno mapya, huyabeba na kuyatumia kila siku.

Mtaalamu wa masuala ya chakula na lishe na meneja mradi wa afya ya mama na mtoto kutoka Shirika la World Vision, Dk Daud Gambo anakubaliana na hoja hiyo, huku akiongeza kuwa mtoto huzungumza kutegemeana na watu wanaomzunguka.

Mwanasaikolojia Kimonga pia anagusia masuala ya asili na urithi katika familia, kuwa nazo zinaweza kuchangia mtoto kuchelewa au kuwahi kuzungumza.

Anasema kama katika familia ama upande wa baba au mama katika hatua za ukuaji huwa wanachelewa katika kuzungumza, hata mtoto anaweza kurithi na kusababisha naye kuchelewa kupitia hatua hiyo ambayo ni muhimu katika ukuaji wa mtoto.

“Pia kama mtoto ameugua sana katika utoto wake, nayo huweza kusababisha mtoto kuchelewa kuzungumza,” anaongeza.

Dk Gambo pia anabainisha namna changamoto mbalimbali za kiafya au kimaumbile zinavyoweza kusababisha mtoto kuchelewa kuanza kuongea.

Akitolea mfano, anasema mtoto mwenye changamoto ya kutosikia inaweza kusababisha kuchelewa kuzungumza kwa baadhi yao.

Pia changamoto mbalimbali katika ulimi, akitolea mfano ulimi kuungana na kujishikiza chini ya mdomo ambayo hujulikana kama ‘tongue-tie’.

Kwa upande wake Dk Samweli Msingwa, ambaye ni mtaalamu wa mishipa ya fahamu, anasema kuwa mtoto kuchelewa kuzungumza kunaweza kusababishwa na kuchelewa pia kwa hatua nyingine za ukuaji kabla ya kufikia kuongea.

“Kama hatua nyingine za ukuaji zilizopita zilichelewa, kuna uwezekano wa mtoto huyo kuchelewa kuanza kuzungumza,” anasema.

Pia anasema changamoto za kiafya au matatizo katika ubongo yanaweza kusababisha kutokea kwa hali hiyo.

Dk Msigwa anashauri kama mtoto amepatwa na changamoto hiyo ni vyema mzazi kumpeleka hospitali ili afanyiwe uchunguzi wa kitaalamu, kubaini nini kinasababisha hali hiyo ili hatua mbalimbali za kimatibabu ziweze kuchukuliwa kama atabainika kuwa na tatizo.

Kwa upande wake mtaalamu wa saikolojia Kimonga, anashauri wazazi kuwapa fursa watoto kujumuika na kucheza na wenzao, huku wakizingatia usalama, pia kutenga muda kwa ajili ya kuzungumza nao.

Related Posts