Njohole aeleza sababu ya kuondoka Simba SC

Mabadiliko makubwa katika muuondo wa uendeshaji wa soka nchini umekuwa na manufaa makubwa kwa wachezaji wa sasa, hasa wenye fursa za kutoka nje ya nchi tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma enzi za Chama cha Soka Tanzania (FAT) kulikokuwa na mizengwe na ukiritimba mkubwa.

Mmoja ya wahanga wa mizengwe na ukiritimba huo, ni Nico Njohole, kiungo mahiri wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kuwika na Simba, aliyekosa dili za kukipiga Ligi Kuu ya England (EPL) aliyefanya mahojiano maalumu na Mwananchi na kufichua safari yake kisoka na maisha kwa ujumla. Endelea naye…!

Alijiunga Simba B mwishoni mwaka 1977 akiwa mwanafunzi wa sekondari.

Alisema kuwa mtu aliyempa ushawishi mkubwa ni mchezaji wa zamani wa Simba, George Kulagwa ambaye alicheza kuanzia shule ya msingi na baadaye sekondari.

Alifafanua kuwa kipindi hicho, hakuwa anacheza naye timu moja, lakini kutokana na uwezo wake, Kulagwa alimshawishi kujiunga na klabu ya Simba, lakini timu B.

“Zamani kulikuwa na mashindano ya shule za msingi kwa Tanzania nzima, ambapo tulikuwa tunacheza michezo mbalimbali,  sikumbuki mwaka yalivyokuwa yamefanyika Singida, ila kiwango nilichokionyesha Kulagwa aliniambia hivi kwa nini usichezee Simba.

“Baada ya kuingia sekondari bado aliendelea kuniambia hilo neno, wakati huo Kulagwa alikuwa anacheza Simba B, basi nikakubali kwenda kujiunga na timu hiyo.

“Haikuwa rahisi kupandishwa kucheza timu ya wakubwa, kwani kulikuwa na wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu kama Rahim Lumelezi, Abbas Kuka na wengineo. Baada ya miaka miwili, mastaa wengi walipata timu Uarabuni, ndipo tukapandishwa na tulipoonyesha uwezo mkubwa hatukuwahi kurudi nyuma.”

Anasema kwa muda ambao alicheza Simba, kipaji chake kilionekana kwa ukubwa, ingawa kwa upande wa maslahi kwa wakati huo yalikuwa ya chini sana.

Anasema, wachezaji wengi walizichezea klabu hiyo na hata kwa wapinzani wao, Yanga kwa mapenzi na asilimia kubwa wachezaji walikuwa wanafanya kazi zao, kwa upande wake alikuwa Tanzania Elimu Supplies.

“Kuanzia miaka ya 1980 angalau wachezaji ndiyo walioanza kuonja matunda ya soka, kipindi chetu hapakuwa na fedha, ingawa kulikuwa na vipaji vikubwa, burudani laiti kama zingekuwa zinahifadhiwa video kama ilivyo sasa, kingeonekana kile ambacho tulikifanya,” anasema.

Baada ya kuona Simba imesajili vijana wengi, alitambua akiendelea kusalia hawatapata nafasi mbele yake ndani ya miaka saba, akaona busara ni kuwapisha  na kuamua kuondoka.

“Zamani ilikuwa ngumu sana, kikosi cha wakubwa cha Simba kumtoa mchezaji, walikuwa na uwezo mkubwa, kila mtu alikuwa anapigania namba, nikaona nilichokionyesha kinatosha acha wacheze wengine, ili nikapate changamoto mpya nje,” anasema.

Anasema, kutokana na uchezaji wake kuwavutia mashabiki wengi, alijitokeza mmoja wao, Mzee Maulid ambaye alikuwa anafanyakazi katika kampuni ya madini ya hapa nchini na kumpa’ dili’ la kwenda Uingereza.

Anasema kuwa Maulid wakati huo alihamishiwa Uingereza na kufanya ‘dili’ lake la kwenda huko kuwa rahisi sana.

“Safari yangu ya Ulaya ilikuwa rahisi sana kwani utaratibu wote ulifanyika ‘connection’ zote za huko zilikuwa tayari.

Maulid aliandaa mpango yote ya huko na kazi yangu mimi ni kuonyesha kipaji changu tu,” anasema.

Anasema, alipofika England alianza kufanya mazoezi na timu ya AFC Bournemouth.

Njohole anasema alifanya vizuri sana akiwa na timu hiyo na uongozi pamoja na benchi la ufundi  walimkubali sana.

“Baada ya kukubaliwa, viongozi walianza kufuatilia taratibu za kujiunga na timu hiyo. Jambo la kwanza ni kupata kibali (Clearance) kutoka Chama cha Soka Tanzania (FAT).

Hatua ya kuomba kibali ilinipa faraja kubwa sana na kuamini ndoto zangu za kucheza Ulaya sasa zimetimia.

Hii ilitokana na kuamini kuwa suala la kupata kibali lilikuwa jambo dogo na rahisi sana na hasa ukizingatia kuwa kuna baadhi ya wachezaji wa Tanzania kama  ukoo wa Manara ulikuwa umepata nafasi ya kucheza huko,” anasema.

Anafafanua, ghafla aliona ndoto hizo zinaanza kufifia kwani muda ulikwenda na hakuwa na jibu la uhakika kutoka FAT.

“Hali ya ucheleweshwaji iliendelea na kufikia hatua ya timu kubadili maamuzi na ndoto kufa kabisa,” anasema kwa masikitiko Njohole.

Anafafanua baada ya kushindikana kwa AFC Bournemouth, Maulid hakuchoka na kumtafutia nafasi klabu ya Arsenal.

Anasema kuwa walipokuwa Brazil na Simba mwaka 1982 ambapo walikaa siku 45,  alipata bahati ya kupiga picha na wachezaji wengi nyota na ambao walikuwa wanafahamika duniani kote.

Anasema kuwa akiwa Arsenal, aliwaonyesha picha za huko  Brazil na pia walikwisha jua uwezo wangu kupitia mazoezi ya AFC Bournemouth na kurahisisha mambo.

“Nikuwa nimepiga picha na wachezaji wengi maarufu wa Brazil na kuwaelezea jinsi gani nilivyo na uwezo wa ndani ya uwanja.

Arsenal hawakuwa na shida na mimi, walikubali, lakini kwa masharti ya kuwasilisha kibali. Hapa sasa ndiyo nikaona safari ya kucheza Uingereza imemalizika na hakuna tena.

Nikashauriana na Maulid na kupata wazo la kwenda Austria ambapo Kassim Manara alikuwa anacheza huko.

Tulitafuta mawasiliano na kumpata na yeye bila kuwa na hiana, alikutukaribisha,” anasema.

Baada ya kufika Austria nilizichezea timu za SV Wernberg 1982/83 na baadaye kuhamia klabu ya ASKÖ Raika Fürnitz na kustaafu mpira mwaka 1998 akiwa na klabu hiyo.

UMRI NA MUONEKANO TOFAUTI

Ukimuona unaweza ukadhani ana umri kuanzia miaka 50 hivi, lakini anataja kwa kinywa chake ana  miaka 63, kinachomfanya asizeeke ni kuzingatia ulaji mzuri, mazoezi na kuepuka ulevi.

“Kinachonisaidia  nje na mazoezi, kazi ninazozifanya  ambazo ni za mizunguko, pia mimi na vyakula vya mafuta ni tofauti kabisa, zamani nilikuwa nakunywa pombe, lakini sasa nimeacha.

Kinywaji changu kikubwa sasa ni maji na kuzingatia muda wa kupumzika, ukifanya hivyo, lazima mwili utakaa vizuri,” anasema.

Anatoa raia kwa wachezaji wa zamani kuzingatia mazoezi na kuepuka ulaji mbaya, ili kuepukana na magonjwa yanayoweza kuepukika.

Tanzania imepanda hadi nafasi ya saba katika viwango vya ubora baada ya klabu za Simba na Yanga kutinga robo fainali ya michuano ya CAF, hata hivyo Njohole anaona ni kitu kizuri, ila anaishauri TFF ifanye jambo.

“Ukiangalia vikosi vya timu hizo, ambavyo vinapangwa mara kwa mara, wazawa ni wachache, hivyo waliofanya kazi kubwa ni wageni, kuna haja sasa TFF kuliona hilo kwa jicho la kipekee, ili wachezaji wazawa wawe wengi na kuleta tija kwa taifa.

“Simba, Yanga na  Azam FC ndio vinara wa kutoa wachezaji wa kuunda timu za taifa, sasa katika timu hizo wazawa hawana nafasi kubwa kama ilivyo kwa wachezaji wa kigeni.”

Japo hakumbuki vizuri mwaka, kuna wakati Simba ilikwenda kucheza Msumbiji, mazingira ya Uwanja wa Maputo kwa wakati huo, ulikuwa mbali na vyoo vilipo.

Anasema, kulikuwa na umbali kidogo kuanzia eneo la kuchezea na choo, pia anaongeza kutokana na umbali huo, mchezaji akibanwa na haja, itambidi achukue muda kidogo mpaka kufika kwenye choo.

Anasema, wakati wa mechi, akajikuta amebanwa na haja ndogo, hivyo kujistili akaenda nyumba ya goli, ambako baada ya kukutwa na mmoja ya kiongozi akakuta anadhalilika.

“Balozi wa nchi hiyo, alikuwa amesoma mambo ya habari na alikuwa mwanajeshi, sasa wakati nakojoa nyuma ya goli, aliniona, hivyo nikaandikiwa ripoti na tukio likaenda hewani, kila mtu alijua hadi nikafungiwa mechi kadha kucheza za mashindano ya kimataifa.

“Kama unavyojua utani wa jadi, mashabiki wa Yanga walikuwa wakiniona walikuwa wananiita kikojozi, kikojozi, unajua ni fedhea,  maana una ndugu, jamaa na marafiki, lakini sikuwa na njia nyingine zaidi ya kuishi na ukweli wa vyoo kuwa mbali, sikustahimili kwenda hadi eneo linalotakiwa.

“Nilitafuta njia moja ya kuuzima utani wa Yanga, tulikuwa tukikutana kwenye mechi, nilikuwa nawasumbua na kuwafunga, hivyo wakaacha kunitania badala yake wakawa wanazungumzia kipaji changu.”

Jina la Mapafu ya Mbwa, lilitokana na wachezaji wenzake wa Simba ambao walikuwa wakimuita katika mazoezi na mechi.

Hii ilitokana na uchezaji wake wa kutochoka na kusaidia wenzake katika kila eneo ili kupata matokeo chanya.

“Nilikuwa na pumzi ya kutosha iliyokuwa inaniwezesha kucheza kila eneo la uwanja, hivyo katika mazoezi walikuwa wananiambia wewe ni Mapafu ya Mbwa, walifahamu watu wachache ndio maana katika vyombo vya habari halikuwa kutajwa katika magazeti nilikuwa naandikwa jina langu halisi,” anasema.

Anaulizwa siri ilikuwa ni ipi ya uwezo wa kuzunguka kila eneo la uwanja wakati wa mechi? Anajibu “Kipaji pekee hakiwezi kukufanya ufanye maajabu, nidhamu, kujituma, vilinisaidia walioniona nacheza nionekane bora.”

Anasema kila anapotazama Ligi Kuu ya sasa na zamani, hajaona uwezo wa wachezaji kama ilivyokuwa enzi hizo.

“Ingawa hakukuwa na fedha kama ilivyo sasa ambapo wachezaji ni wanalipwa fedha nyingi na ni matajiri, lakini wanacheza kawaida na kulewa sifa.

Pamoja na kucheza kwa kiwango cha juu soka la Tanzania, bado Njohole anasema hakuwa kupata fedha za kujiinua kimaisha.

Anasema, alikuwa anapata fedha za kujikimu yeye na familia yake na kuongeza kuwa, alipata mafanikio makubwa na kujenga nyuma akiwa Austria.

Ukoo wa Njohole kwa sasa bado ni maarufu na mashabiki wengi walidhani kuwa kuna mtu nyuma yao alikuwa anawashawishi.

Kuna Deo, Renatus na Boniface ambao ni maarufu, anasema hakuwahi kuwashawishi, anaamini yalikuwa mapenzi na machaguzi yao kuitumikia timu hiyo.

Njohole anasema kuwa  kila mtoto alikuwa na ndoto ya kucheza mpira na hakuwa na ushawishi zaidi ya utashi wao tu.

Kwa sasa, nina watoto, lakini hawataki kucheza mpira, ila kwa Renatus, wapo wanaocheza, lakini siyo sana,” anasema.

“Ujue watoto waliozaliwa Ulaya wana uhuru wa kuchagua vitu wanavyovitaka wenyewe, maana mifumo ni tofauti na huku.

“Nadhani walipenda wenyewe kucheza Simba, pia hatuna ndugu wengine ambao wanacheza soka, labda watoto wa wadogo zangu,” anasema.

Kutokana na kiwango chake anaulizwa kama anatamani kusomea ukocha? Anajibu”Siyo lazima mchezaji mwenye kipaji kikubwa uwanjani akawa kocha, kiukweli kwangu mimi najiona sina kabisa kipaji cha ukocha, ila nikiangalia mchezo naweza nikashauri nini kifanyike ili timu iweze kufanya vizuri.”

Anasema amefanikiwa kutazama mchezo wa Simba dhidi ya Tabora United, anaona kuna udhaifu kwa kila nafasi, hivyo ni juu ya wachezaji wenyewe kujitathimini na kuamua kuonyesha ubora wao.

“Ujue kuna wakati unaweza ukaona labda kocha siyo mzuri, lakini kama mchezaji ni mzuri, bidii yake itaonekana anachokifanya uwanjani, lazima atajituma, sisi zamani kuna wakati tulikuwa tunaambiana kwamba lazima mchezo fulani tufunge iwe mvua ama jua, katika mazoezi kila mtu alijituma na kufanya jukumu lake bila kutegemea na tuliweza kufanikiwa, wao wanashindwa wapi na wanapata kila kitu, “ anasema na kuongeza;

“Ifikie hatua wachezaji wa Simba wajiulize kwa nini wachezaji wa Yanga wanafanya vizuri, wana umoja na kuipambania timu kitu ambacho kinakosekana kwao, hata kama kikosi ni kipya, mfano unaona juzi wanakosa nafasi za juu ambazo wangefunga mabao mengi zaidi kwa aina ya wapinzani wao walivyokuwa wanacheza.”

Nicodumus “Nico” Njohole alizaliwa Desemba 12, 1960, eneo la Chang’ombe jijini Dar es Salaam akiwa mtoto wa kwanza wa familia ya Mzee Njohole.

Alipata elimu ya Msingi katika Shule ya Msimbazi Wavulana (Msimbazi Boys), baadaye Sekondari ya Kinondoni Muslim ambako alisoma kidato cha kwanza na baadaye kuhamisha shule ya sekondari ya Forodhani na kumaliza elimu yake ya sekondari.

Kutokana na kipaji chake, Njohole alikuwa maarufu tangu akiwa kija mdogo kuanzia timu za mitaa aliyoishi Chang’ombe na Ilala, baadaye timu ya Msimbazi Rovers maarufu kwa jina la Pentagon.

Related Posts