PIRAMIDI YA AFYA: Dondoo za matumizi ya mipira ya kiume

Matumizi ya mipira ya kiume ni moja ya njia za kuzuia maambukizi yanayoenea kwa njia ya kujamiiana, ikiwamo virusi vya Ukimwi (VVU), kaswende, kisonono, virusi vya homa ya ini, hepes na papilloma vinavyosababisha saratani ya shingo ya kizazi.

Vilevile hutumiwa kama njia ya uzazi wa mpango na tiba ya tatizo la kuwahi kufika mshindo.

Watumiaji wengi wa sasa huwa na lengo la kujikinga na maambukizi ya VVU, huku mipira ya kiume ndiyo inayotumiwa zaidi kuliko ya kike.

Mipira hii inayojulikana zaidi kama ‘condom’ hutumiwa na wale walioshindwa kujizuia kuwa na mpenzi mmoja mwaminifu asiye na maambukizi.

Leo tutapata ufahamu wa dondoo muhimu katika kutumia mipira ya kiume, ambayo ikitumiwa ufanisi wake wa kuzuia maambukizi ni asilimia 90 hadi 95.

Kwanza fahamu mipira hii inaponunuliwa au kupatikana, hii inakusaidia kupata kitu chenye ubora na ufanisi kwa wakati.

Mipira hii inapatikana katika maduka ya dawa na ya kawaida, vituo vya afya vya Serikali na binafsi. Kumbuka hapa unalinda maisha yako, hivyo huna haja ya kuona aibu kwenda kuinunua au kuchukua bure.

Mbili, unapoipata tazama tarehe ya mwisho wa matumizi na ikague kama iko salama haina mipasuko na kasha lake limefungwa vizuri. Kumbuka mipira iliyopita muda wake huchanika kirahisi.

Tatu, kama umeshapata hifadhi mahali pasipo na joto kali, wapo baadhi ya watu huinunua mipira hiyo na kuiweka katika vyombo vya usafiri sehemu ambako kuna joto kali.

Wapo wanaohatarisha ubora wake kwa kuiweka katika waleti na kuikalia kwa muda mrefu pasipo kuitumia, hivyo kugandamizwa na kupata joto kali.

Nne, unapofikia hatua ya kuitumia hakikisha kuwa kiu ya kujamiiana, isifubaze malengo ya kuitumia kwa usahihi.

Ongea na mwenza wako kuwa mnaitumia kulinda afya zenu, hivyo ni vyema kushirikiana kuitumia kwa usahihi.

Tano, itoe katika boksi na soma maelekezo yaliyoandikwa na fungua kwa ncha za vidole vyako na usithubutu kutumia meno, kwani unaweza kuupasua mpira wenyewe.

Sita, visha katika sehemu ya kiume ikiwa imesimama na finya chuchu ya mpira kwa ubapa wa dole gumba na kidole cha kuonya. Lengo ni kuacha nafasi ya hewa ili isipasuke.

Katika hatua hii mwenza anaweza kukusaidia pia kufinya chuchu ya mpira ila mhakikishe kucha zenu ni bapa zisizo na ncha.

Hakikisha mviringo wa mpira unatazama nje kisha viringisha kuelekea shina la uume, ukikosea ukaweka nje ndani tupa na tumia nyingine mpya.

Saba, kumbuka kuwa mipira hii imewekwa kwa ajili ya matumizi ya mshindo mmoja, mpira mmoja.

Usiibadili na kuunganisha kwenda mshindo wa pili, huweza kusababisha mpira huo kuvuka na inaweza kupotelea ukeni, hivyo kuhitaji kutolewa kitabibu.

Nane, kuwa rafiki wa mazingira kwa kuitupa mahala salama kila unapomaliza na ifunge kwa fundo moja na weka ndani ya tishu, karatasi au kipande cha gazeti, kisha kaitupe katika pipa la taka.

Tisa, usivae mbili mbili kwa wakati mmoja, usiweke kilainishi cha ziada, yaani mafuta na itumiwe katika njia iliyokusudiwa.

Kumi, mipira ina kiwango cha kushindwa kati ya asilimia 10 hadi 15, hivyo njia pekee ni kutulia na mwenza mmoja mwaminifu asiye na maambukizi.

Jitafutie elimu ya afya kila mara kupata taarifa mpya za mipira hii na elimu ya afya kwani muda, vitu na watu vinabadilika.

Related Posts