Dodoma. Washtakiwa kesi ya ubakaji na kumwingilia kinyume cha maumbile binti, mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Salaam, wamefikishwa mahakamani kuendelea na usikilizwaji wa shauri hilo.
Leo Agosti 23, 2024 ni siku ya tano tangu walipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma ambako walisomewa mashtaka mawili.
Hakimu Mkazi Mkuu, Zabibu Mpangule anayesikiliza kesi hiyo alipanga kuisikiliza kwa siku tano mfululizo.
Washtakiwa walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Jumatatu, Agosti 19, 2024 na kusomewa mashtaka ya kumbaka na kumwingilia kinyume cha maumbile binti huyo anayetajwa mahakamani kwa jina la XY. Baada ya kusomewa mashtaka walikana.
Katika kesi hiyo inayosikilizwa faragha, washtakiwa ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105 Clinton Damas maarufu Nyundo, askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba.
Washtakiwa wamefikishwa mahakamani saa tatu asubuhi wakitokea mahabusu.
Binti anayedaiwa kubakwa na kuingiliwa kinyume cha maumbile, akiwa shahidi wa tatu wa upande wa Jamhuri alitoa ushahidi jana Agosti 22, 2024 mbele ya hakimu Mpangule.
Binti huyo (XY) aliingia katika jengo la Kituo Jumuishi cha Kutoa Haki cha Dodoma akiwa amevaa mavazi meusi yaliyoficha sura yake akiongozana na wanawake wawili.
Alitoa ushahidi kuanzia saa nane mchana hadi saa 12.00 jioni katika kesi hiyo ya jinai namba 23476 ya mwaka 2024.
Akizungumza baada ya kesi kuahirishwa jana, wakili wa utetezi, Meshack Ngamando alisema, “Tumemaliza kumsikiliza shahidi huyu na kesi imeahirishwa hadi kesho (Agosti 23) saa 4.00 asubuhi. Mwenendo wa kesi unaendelea vizuri,” alisema.
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Renatus Mkude alisema wataendelea kupokea ushahidi, lakini idadi ya mashahidi katika kesi hiyo itaendana na mwenendo wa kesi ulivyo.
“Siku ya kwanza nilisema kesi hii itasikilizwa kwa siku tano mfululizo. Idadi ya mashahidi inategemea mwenendo wa kesi husika,” alisema.
Wengine waliotoa ushahidi ni shahidi wa kwanza, mtaalamu wa uchunguzi wa mambo ya sayansi ya simu na vifaa vya kielektroniki kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi na shahidi wa pili, ni daktari kutoka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.