Bwawa lapasua kingo nchini Kenya, watu 24 wapoteza maisha – DW – 29.04.2024

Bwawa hilo la Kijabe linakiswa kuvunja kingo zake mwendo wa saa nane usiku wa kuamkia leo jumatatu baada ya kushiba mvua kubwa inayozidi kunyesha.

Maji hayo yalisambaa kwenye mitaa iliyo karibu na kusababisha mauti na uharibifu mkubwa. Aidha maji hayo yameharibu barabara kuu ya Nairobi- Nakuru na kuyasomba magari ya uchukuzi.

Magari matano ya uchukuzi yalisombwa likiwemo basi la kampuni ya Easy Coach lililokuwa na watu 60. Hatma ya abiria hao haijulikani huku shughuli za uokozi zikiendelea.

Hali hiyo imesababisha msongamano mkubwa wa magari ambayo yamekwama kwenye barabara hiyo kuu ambayo huwa na shughuli nyingi.

Kamanda wa Polisi wa Naivasha Stephen Kirui amesema kuwa manasura wamepelekwa kwenye hospitali ya Naivasha na Mai Mahiu kwa matibabu. 

Watu 23 wahofiwa kufa maji baada ya boti kuzama Tana River

Sehemu kadhaa nchini Kenya, maji ya mafuriko yalifikia viwango vya kutisha.
Sehemu kadhaa nchini Kenya, maji ya mafuriko yalifikia viwango vya kutisha.Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Kwingineko hali ya huzuni na majonzi imetanda huku shughuli za uokozi za kuwatafuta watu 23 waliokuwa kwenye boti zikishika kasi eneo la Kuna Punda kaunti ya Tana River.

Shughuli hizo zinaongozwa na Shirika la Msalaba Mwekundu zilifanikiwa kuwaokoa watu 20. Mkasa huo ulijiri saa kumi na mbili Jumapili jioni wakati boti mbili zilipokuwa zikifuatana kutoka eneo la Madogo kuelekea Moroa.

Hata hivyo boti ya kwanza haikusalimika kwenye mkasa huo baada ya kuzama na watu. Kina mama na watoto wakiwa waathiriwa wakuu.

Inasemekana kuwa boti hiyo ilikuwa imebeba kupita kiasi kwa mujibu wa mashuhuda. Kwa kawaida ilistahili kuwabeba watu 20 ila ilizidisha maradufu. Maeneo pana ya Tana River na Garissa  yamefunikwa na mafuriko hivyo kuathiri uchukuzi wa barabara. 

Maporomoko yasababisha vifo Murang´a, ufunguzi wa shule wapigwa kalenda

Mafuriko mji mkuu Nairobi
Mvua kubwa zilizonyesha karibuni, zimesababisha vifo na uharibifu wa mali nchini Kenya.Picha: LUIS TATO/AFP/Getty Images

Huku hayo yakiripotiwa, familia ya watu watano imeangamia katika kaunti ya Murang’a kufuatia maporomoko ya ardhi.

Maporomoko hayo yamesababishwa na mvua kubwa zinazokunya kote nchini Kenya. Katika shule ya msingi ya Sikinga eneo la Nambale iliyoko kaunti ya Busia mvua hizo zimeharibu miundo msingi.

Kufuatia hali hiyo serikali imeahirisha mpango wa kuzifungua shule kote nchini hadi tarehe sita mwezi ujao. Shule zilitarajiwa kufunguliwa leo.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, serikali imewataka maafisa wake wote wa elimu walioko nyanjani kutathmini hali ilivyo na kuwasilisha taarifa zao.

Mamlaka nchini Kenya zinasema kuwa idadi ya watu waliofariki kote nchini kwa sasa imefikia 100 huku watu wengine elfu 60 wakiyapoteza makazi. Hata hivyo athari za mvua kubwa huenda yakabainishwa wazi mvua hizo zikatakapokatika.

Related Posts