SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema litaendeleza ushirikiano baina yake na Ofisi ya Rais TAMISEMI katika kuboresha hudma za afya nchini ili kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga kwa kuhimarisha huduma za afya ya msingi na utoaji wa elimu juu ya ulinzi wa mtoto.
Katika mkutano wa pamoja baina ya maafisa wa idara ya Afya na Elimu OR – TAMISEMI na maafisa kutoka UNICEF hapa nchini kujadili juu ya ushirikiano baina ya pande hizo mbili, Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania, Bi. Elke Wisch, amesema shirika hilo litaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa kutoa misaada na kufadhiri miradi inayo endelea ili iweze kukamilika kwa wakati na kuwa na matokeo yaliyo kusudiwa.
“UNICEF itaendelea kufadhiri miradi inayolenga kuboresha mifumo ya utoaji huduma za afya na kugharamia masuala ya kibajeti na program zinazoendelea nchini kutokana na misingi ya shirika letu ambayo ni kusaidia katika maendeleo ya watoto na wanawake hasa kwa nchi wanachama wa umoja wa mataifa” alisema Bi.Wisch.
Katika mkutano huo mkurugenzi wa huduma za afya, ustawi wa jamii na lishe ofisi ya Rais – TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amesema, kupitia ufadhiri na misaada inayotolewa na UNICEF ikilenga kuboresha huduma za afya msingi imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya mama wajwazito na vichanga katika mikoa ya Kigoma, Songwe, Mbeya, Iringa na Njombe.