Serikali yachukua hatua kupunguza mrundikano wa kesi

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini amesema Serikali imeendelea kufanya maboresho ya sera katika kuchochea uanzishwaji wa taasisi mbalimbali za usuluhishi wa migogoro katika sekta mbalimbali ili kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani.

Amesema jitihada hizo zinafanyika kwa kutambua migogoro ikimalizwa nje ya mahakama inachukua muda mfupi na inaondoa vinyongo na hasira na wananchi kubaki katika mazingira ya amani na upendo.

Hayo ameibanisha  Dar es Salaam leo, Agosti 23, 2024 alipokuwa mgeni rasmi  kwenye mkutano wa mwaka uliandaliwa na Taasisi ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara Tanzania (TIArb) uliowakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.

“Baada ya kufanya maboresho ya sera taasisi za usuluhishi zimekuwa zikiongezeka na sasa zimefikia saba zinazotambuliwa baada ya kusajiliwa na wizara ikiwemo TIArb.

“Serikali tunaridhishwa kwa namna wasuluhishi wanavyotekeleza majukumu yao na uzoefu unaonyesha mashauri mengi ya migogoro ya kimkataba ya uwekezaji na ujenzi ikipelekwa mahakamani inachukua muda mrefu lakini wakikutana na kuzungumza kwa kuwashirikisha waliobobea katika usuluhishi yanaisha mapema,” amesema Sagini

Sagini ambaye ni Mbunge wa Butiama, amesema kesi zikifikishwa mahakamani zinachukua muda mrefu kutokana na michakato yake kuwa mingi ikiwemo kupeleka ushahidi na wengine kukata rufaa.

“Hata katika mahakama zetu Jaji Mkuu ni kiongozi anayesisitiza twende katika utaratibu wa kusuluhisha migogoro kwa njia mbadala ya mazungumzo kisera na kisheria inakubalika,” amesema

Sagini katika maelezo yake amebainisha serikali kujikita katika sera ya kuvutia uwekezaji wa watu kutoka ndani na nje ni sababu ya kuendelea kuhamasisha taasisi hizo ili wawekezaji wakija kufanya shughuli zao wawe na uhakika migogoro ikijitokeza wanamaliza kwa mfumo wa mazungumzo.

 Katibu wa taasisi ya (TIArb), Usajo Mwambene amesema wadawa wasiogope kupeleke migogoro kwa wasuluhishi kwani moja ya mambo wanayozingatia ni usiri ili pande zinazokinzana ziweze kuuisha mahusiano yao.

“Kuendesha kesi mahakamani ni gharama, vipato kama watanzania tunajuana, ni muhimu kumaliza migogoro inayowasibu kwa njia ya mazungumzo kwa kuwashirikisha wabobevu ili kudumisha amani katika shughuli tunazofanya,” amesema.

Akizungumzia mkutano huo, Mwambene amesema ulikuwa mkutano wa saba tangu kuanzishwa na taasisi hiyo na ulijumuisha wadau kutoka eneo hilo na sekta zingine walikutana na kupeana elimu ya usuluhishi migogoro kwenye sekta ya ujenzi na uwekezaji wa kimataifa.

Tuliweka eneo la ujenzi kwa sababu nchini kwetu kila eneo unalopita unakutana na ujenzi unaendelea na kumekuwa na migogoro mingi tunataka na wao wasiende mahakamani wamalize nje ya mahakama,” amesema Mwambene.

Related Posts