Mapya yaibuka kesi ya mauaji ya Asimwe

Bukoba. Baadhi ya washtakiwa katika kesi ya mauaji ya mtoto Asimwe wamedai hawajui kosa linalowakabili mahakamani licha ya kusota rumande kwa siku 57.

Washtakiwa tisa walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya Bukoba kwa mara ya kwanza Juni 28, 2024 na kusomewa shtaka moja katika kesi namba 17740/2024, wakidaiwa kumuua kwa kukusudia mtoto mwenye ualbino Asimwe Novath (2).

Kesi hiyo imetajwa kwa mara ya tano mahakamani hapo leo Agosti 23, 2024. Washtakiwa wote tisa waliokuwapo mahakamani ni pamoja na  Padri Elpidius Rwegoshora, Novath Venath (baba mzazi wa Asimwe), Nurdini Masudi, Ramadhani Selestine, Rweyangira Alphonce, Dastan Bruchard, Faswiu Athuman, Gozbert Alikad na Desdery Everigist.

Awali, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Erick Mabagala mbele ya Hakimu Mkazi, Eliapokea Wilson, amedai Jamhuri ilipeleka maombi Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba kupitia kesi namba 17740/2024 mbele ya Jaji Lameck Mlacha ili iweze kuruhusu kuhamishwa kwa shtaka hilo.

Wakili Mabagala amesema pia waliwasilisha hoja sita   zikiwamo za kuomba mashahidi wanaotarajia kuwatumia katika kesi hiyo taarifa zao zisitolewe kwa umma wakati wa mwenendo wa kukabidhi na usikilizwaji wa shauri hilo.

Pia nyaraka zenye taarifa zote za mashahidi, maelezo na taarifa zinazoonyesha makazi ya mashahidi kutoruhusiwi kutolewa kwa umma, kesi kusikilizwa faragha, na kutoruhisiwa kutumia vinasa sauti wakati wa kusikiliza kesi hiyo.

Mabagala amesema Jaji Mlacha aliridhia ombi hilo hivyo anaomba mahakama hiyo iridhie tarehe nyingine ili kesi itajwe na kusikilizwa.

Hakimu Wilson ameridhia ombi la wakili Mabagala akisema kesi itatajwa Septemba 6, 2024.

Wakili wa utetezi Mathias Rweyemamu anayemwakilisha mshtakiwa wa kwanza, Rwegoshora amesema wanakubaliana na uamuzi wa mahakama wa kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya shauri hilo kutajwa.

Washtakiwa walipofikishwa mahakamani walionyesha hali ya unyonge baadhi wakitokwa machozi walipoingia chumba cha mahakama.

Wakiwa wamesimama kizimbani wakili Mabagala alipokamilisha maelezo yake kuhusu mwenendo wa kesi, mshtakiwa wa tatu, Nurdini Masudi alinyoosha mkono.

Aliporuhusiwa kuzungumza  aliiomba mahakama kumweleza kwa nini yupo mahakamani hapo kwa sababu amefikishwa hapo bila kujua kesi inayomkabili.

Mshtakiwa wa tano, Rweyangira Alphonce naye alinyoosha mkono, alipoulizwa na hakimu shida yake, kwa shida huku akitokwa machozi aliomba kujua ni kwa nini yupo mahakamani, akitaka aelezwe nini kinamsibu.

Kwa upande wake, mshtakiwa wa sita, Dastan Bruchard, huku akilia kwa sauti aliomba mahakama iwasaidie kujua ni lini hatima ya wao kuendelea kusota rumande, huku wakifikishwa mahakamani na kesi kupigwa kalenda.

Pia aliomba kujulishwa ni kwa nini yupo mahakamani swali ambalo alikuwa akiliuliza mara nyingi.

Kwa mara kadhaa washtakiwa walionekana kuinamisha vichwa huku wakitokwa na machozi.

Kutokana na hatua hiyo, wakili Mabagala aliwakumbusha kuhusu kesi iliyofunguliwa na Jamhuri dhidi yao kuwa wanadaiwa kumuua mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath (2), kesi iliyofikishwa mahakamani hapo Juni 28, 2024.

Hakimu alijibu maswali yao akisema watayawasilisha wakati wa kusikilizwa kesi inayowakabili kwa sababu kwa muda huo mahakama haiwezi kufanya hivyo kutokana na sababu za kisheria.

Washtakiwa wote tisa wamerudishwa rumande hadi Septemba 6, 2024 kesi itakapotajwa.

Related Posts