ALIYEKUWA nahodha wa Geita Gold, Elias Maguri amejiunga na Biashara United inayoshiriki Ligi ya Championship, ili kuongeza nguvu kuipigania kupanda Ligi Kuu msimu ujao.
Japokuwa Biashara United bado haijatangaza kikosi cha msimu, lakini Mwanaspoti inafahamu tayari imemalizana na Maguri.
Mmoja wa viongozi wa timu hiyo ambaye hakutaka kuweka wazi jina lake amesema wamemalizana na mchezaji huyo na hakutaka kufafanua wachezaji wengine waliowachukua kutoka Ligi Kuu.
“Tumewasajili wachezaji wengi, ila nimekujibu uliyeniuliza. Hao wengine tunasubiri muda ukifika wa kuwatangaza, tutafanya hivyo. Kwa sasa tumeweka nguvu zetu kumalizana na kocha. Hatuwezi kutangaza kikosi kabla ya kumpata,” amesema kiongozi huyo.
Alipotafutwa Maguri kuzungumzia hilo, amegoma, lakini akasema: “Timu ndizo zina wajibu wa kutangaza wachezaji na siyo wachezaji kutangaza wanaenda wapi, hivyo sina jibu katika hilo swali lako.”