Timu ya Israel ilikuwa mjini Cairo “kujadili kuendeleza makubaliano (ya kuachiliwa) mateka,” msemaji wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu Omer Dostri aliambia AFP siku ya Alhamisi.
Lakini wawakilishi wa Hamas hawakushiriki na afisa kutoka vuguvugu hilo la Kiislamu, Hossam Badran, aliiambia AFP siku ya Ijumaa kwamba msisitizo wa Netanyahu kwamba wanajeshi wabaki kwenye ukanda wa mpaka wa Philadelphia unaonyesha “kukataa kwake kufikia makubaliano ya mwisho”.
Misri na wapatanishi wenza Qatar na Marekani zimejaribu kwa miezi kadhaa kufikia mpango wa kumaliza vita vya zaidi ya miezi 10 na vuguvugu la Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Mwanadiplomasia wa juu wa Marekani Antony Blinken alizuru kanda ya Mashariki ya Kati wiki hii kusisitiza umuhimu wa kufikia makubaliano haraka.
Mashuhuda wameripoti Ijumaa kuwepo na mapambano makali katika upande wa kaskazini wa ukanda huo, mashambulizi makali katikati na mashambulizi ya vifaru katika mji wa kusini wa Rafah.
UN yasema raia wamechoka
Umoja wa Mataifa umesema maelfu ya raia wamelaazimika kuhama tena wiki hii kutoka Deir el-Balah na mji wa kusini wa Khan Yunis, baada ya jeshi la Israel kutoa maagizo kwao wahame, ambayo yanatangulia operesheni za kijeshi.
Soma pia: Wapalestina wakubaliana kuunda serikali ya maridhiano itakayohusisha Hamas na Fatah
UN inasema vita hivyo vimewahamisha takribani asilimia 90 ya wakaazi wa Gaza, na hali hii imekuwa ikijirudia mara kadhaa, na kuwaacha wakiwa hawana pa kujihifadhi, maji salama na mahitaji mengine huku magojwa yakisambaa.
Mratibu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Maeneo ya Wapaletina, alisema siku ya Alhamisi kwamba raia wamechoka na kuogopeshwa, wakikimbia kutoka eneo moja lililoharibiwa kwenda jengine, kukiwa hakuna dalili ya kukoma kwa hali hii, na kuogeza kuwa “hii haiwezi kuendelea.”
Jeshi la Israel siku ya Ijumaa lilisema kuwa katika siku iliyopita wanajeshi wake “wamewaangamiza makumi” ya wanamgambo karibu na Khan Yunis na Deir el-Balah, katikati mwa Gaza.
Mwezi Aprili jeshi liliwaondoa wanajeshi kutoka Khan Yunis baada ya miezi kadhaa ya mapigano mabaya, lakini wamejikuta wakilazimika kuanza tena operesheni huko, na kuwaacha raia wakihisi hawana pa kukimbilia. “Hakuna namna ya kuishi,” alisema Haitham Abdelaal.
China yaitaka Israel kuheshimu maazimio ya UN
China pia imeitolea wito Israel kusitisha mara moja operesheni zake za kijeshi Gaza, na kuahidi uugwaji mkono wake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kuchukuwa hatua zinazohitajika kufanikisha mpango wa kusitisha vita.
Balozi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Fu Cong, alitoa taarifa kwenye mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu Mashariki ya Kati na mzozo wa Israel na Palestina, akisema imepita zaidi ya miezi miwili tangu kupitishwa kwa azimio la baraza la usalama Nambari 2735, lakini operesheni za jeshi la Israel limeendelea, na kusababisha upotevu mkubwa wa maisha kila siku.
Soma pia: Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lashindwa kupitisha azimio la kusitisha mapigano Gaza
“China inaitaka Israel kusitisha mara moja operesheni zote za kijeshi Gaza, kusitisha vitendo vyovyote vinavyoweza kuchochea hali ya mambo katika eneo hilo, na kuacha mara moja kuweka vizuizi kwa usitishaji vita,” alisema Balozi Fu.
“Tunazitaka nchi zenye ushawishi mkubwa kuchukua msimamo wa dhati. Mtazamo wa haki na wa kuwajibika kuilazimisha Israel kusitisha operesheni zake za kijeshi na mauaji ya raia haraka iwezekanavyo.”
Fu amekariri kuwa usalama endelevu unaweza kupatikana tu kwa kushikilia kanuni ya usalama wa pamoja, na kwamba amani ya kikanda inapaswa kujenga kupitia ushirikiano wenye kuwajibika kwa pande zote zinazohusika.
Aliongeza kuwa kupatikana kwa uhuru wa taifa la Palestina na utekelezaji wa suluhisho la mataifa mawili ndiyo njia pekee za kisiasa kuelekea utatuzi wa mzozo huo.